Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania, Marekani zasaini makubaliano ya afya ya Sh8 trilioni

Muktasari:

  • Fedha hizo ambazo zaidi ya dola 3.14 bilioni (Sh8.164 trilioni) ni fedha kwa ajili ya kushughulikia afya kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2026-2030.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na ya Marekani leo Jumatano, Julai 1, 2026 zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya (MoU) ya miaka mitano yenye thamani ya zaidi ya dola 3.14 bilioni (Sh8.164 trilioni) hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa afya nchini na kuweka msingi wa ushirikiano mpya unaolenga kujitegemea.

Makubaliano hayo yatatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030 kupitia uwekezaji wa pamoja wa Serikali ya Tanzania na Marekani, yakihusisha maeneo ya usalama wa afya, bima ya afya kwa wote, matumizi ya teknolojia za kidijitali, uzalishaji wa ndani wa bidhaa tiba, utafiti na uimarishaji wa mifumo ya afya.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, Julai Mosi, 2026 Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Marekani imekusudia kuwekeza takribani dola za Marekani bilioni 1.34 (Sh3.48 trilioni) huku Tanzania ikichangia zaidi ya dola bilioni 1.8 (Sh4.68 trilioni) katika kipindi chote cha utekelezaji wa makubaliano hayo.

“Hatutakuwa tena na utaratibu wa kubadilishana sampuli kwa sababu kama nchi tunaamini tuna uwezo wa kufanya kazi hizo wenyewe. Ubora wa makubaliano haya umetokana na ushiriki wa wataalamu wetu pamoja na wizara mbalimbali zilizoshirikiana kuandaa.

“Tunaamini yatakuwa mfano kwa bara letu na tunatamani nchi nyingine za Afrika zije kujifunza namna ambavyo Tanzania na Serikali ya Marekani zimejenga ushirikiano huu. Vilevile, makubaliano haya yanaendana na dira ya nchi ya kuingia katika uchumi wa viwanda kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani na kujenga uwezo wa kujitegemea katika sekta ya afya,” amesema Mchengerwa.

Amesema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kwa kujengwa katika misingi ya usawa, uwajibikaji na kujitegemea, tofauti na mfumo wa utegemezi wa muda mrefu uliokuwapo hapo awali.

“Makubaliano haya si mwendelezo wa utegemezi bali ni ramani ya kutuondoa kwenye utegemezi. Ifikapo mwaka 2030 Tanzania ndiyo itakayobeba sehemu kubwa ya gharama za mfumo wake wa afya,” amesema Mchengerwa.

Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kugharamia mishahara ya watumishi wa afya, ununuzi wa dawa, huduma za maabara pamoja na huduma nyingine muhimu kupitia rasilimali za ndani, hatua aliyoeleza kuwa inatekeleza kwa vitendo falsafa ya kujitegemea iliyoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mchengerwa amesema makubaliano hayo ni ya kipekee kwa sababu yameandaliwa kwa ushirikiano wa wataalamu kutoka sekta mbalimbali na wizara tofauti, hali iliyowezesha kupatikana kwa hati inayolinda masilahi ya Taifa na kuendana na viwango vya kimataifa.

“Makubaliano haya yatakuwa bora barani Afrika na hatutakuwa tena na utaratibu wa kubadilishana sampuli. Sisi kama nchi tunaamini uwezo wa kufanya haya tunao kama Taifa,” amesema.

Ameongeza: “Makubaliano haya ni bora kabisa ukizingatia wataalamu wetu walioshiriki na Wizara zote zilizokaa kwa pamoja. Tunaamini haya ni makubaliano bora kabisa barani Afrika. Tunatamani nchi nyingine za Afrika zije zijifunze kwetu kwa namna ambavyo tumekubaliana sisi na Serikali ya Marekani.”

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ushirikiano huo utaongeza uwezo wa Tanzania katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa, kuimarisha maabara za kisasa, kuendeleza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utoaji wa huduma za afya na kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya.

Amesema hatua hiyo pia inaendana na azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda kwa kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya dawa na bidhaa tiba, hatua itakayopunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mchengerwa pia ameishukuru Serikali na wananchi wa Marekani kwa ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya afya, akitaja mchango mkubwa uliotolewa kupitia programu mbalimbali, ikiwemo Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), ambao umechangia kuimarisha huduma za kinga, tiba na matunzo ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kwa zaidi ya miongo miwili.

Kusainiwa kwa makubaliano hayo kunafuatia mazungumzo yaliyoanza Mei 18, 2026 mjini Geneva, Uswisi, ambapo Mchengerwa alikutana na Ofisa wa Marekani wa Shirika la Global Health, Brad Smith.

Katika kikao hicho, pande zote mbili zilikubaliana kuharakisha maandalizi ya hati ya ushirikiano wa afya wa muda mrefu, huku zikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote na unaozingatia sheria za kitaifa pamoja na wajibu wa kimataifa.

Wakati wa mazungumzo hayo, Tanzania iliweka bayana dhamira yake ya kujenga mfumo imara wa afya unaojitegemea na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.

Serikali ilisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuchochea uhamishaji wa teknolojia, kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani na kuimarisha uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa tiba.

Kupitia MOU hiyo mpya, Tanzania inatarajia kuimarisha zaidi mfumo wa afya, kuongeza uwezo wa kujitegemea kifedha na kiufundi, pamoja na kuwa kitovu cha ushirikiano wa afya barani Afrika, huku Serikali ikieleza kuwa makubaliano hayo yanaweza kuwa mfano wa ushirikiano wa kimkakati kwa nchi nyingine za Afrika.