Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sindano mpya ya uzazi wa mpango kwa wanaume yazua matumaini, hofu

Muktasari:

  • Kwa sasa ADAM ipo katika hatua ya pili ya majaribio ya kitabibu kwa binadamu (Phase II clinical trial), hatua inayolenga kuthibitisha usalama, ufanisi na muda wa kufanya kazi kwa idadi kubwa zaidi ya washiriki kabla ya kupewa idhini ya matumizi kwa umma.



Dar es Salaam. Kwa miongo mingi, jukumu la uzazi wa mpango limeendelea kubebwa zaidi na wanawake kupitia matumizi ya vidonge, sindano, vipandikizi na vifaa vya ndani ya kizazi (IUD) huku wanaume wakiendelea kuwa na chaguo la uzazi wa mpango kwa kutumia kondomu au upasuaji wa kufunga mirija ya mbegu za kiume (vasectomy).

Hata hivyo, maendeleo mapya ya kisayansi yanaashiria uwezekano wa kubadili hali hiyo baada ya Kampuni ya Teknolojia ya Afya ya Contraline kutangaza mafanikio ya awali ya kifaa chake kipya cha uzazi wa mpango kwa wanaume, kinachoitwa ADAM ambacho hakitumii homoni na kimeundwa kutoa uzazi wa mpango wa muda unaoweza kurejeshwa.

ADAM ni hidrojeli (hydrogel) inayodungwa kwenye mirija inayosafirisha mbegu za kiume (vas deferens) kupitia utaratibu mfupi unaofanyika hospitalini bila kumlaza mgonjwa.

Badala ya kuzuia uzalishaji wa mbegu au kubadili mfumo wa homoni, hidrojeli hiyo huziba njia ya mbegu ili zisiweze kutoka wakati wa kumwaga shahawa.

Kwa mujibu wa Kampuni ya Contraline mwanamume huendelea kutoa shahawa kama kawaida, lakini hazibebi mbegu za uzazi.

Tofauti na vasectomy, hidrojeli hiyo imeundwa kuvunjika yenyewe taratibu baada ya muda, hatua inayotarajiwa kurejesha uwezo wa kupata watoto bila upasuaji mwingine, ingawa suala hilo bado linaendelea kuthibitishwa kupitia tafiti.

Matokeo ya awali yaliyowasilishwa katika mkutano wa mwaka wa American Urological Association yanaonesha kuwa idadi ya mbegu za uzazi za mwanaume aliyefanyiwa utaratibu wa kuchomwa sindano hiyo ilipungua kwa kiwango kikubwa ndani ya takribani mwezi mmoja.

Aidha, washiriki wawili wa utafiti waliendelea kuwa na kiwango cha sifuri cha mbegu za uzazi hadi miezi 24 bila kuripoti madhara makubwa yanayohusishwa na kifaa hicho.

Kwa sasa ADAM ipo katika hatua ya pili ya majaribio ya kitabibu kwa binadamu (Phase II clinical trial), hatua inayolenga kuthibitisha usalama, ufanisi na muda wa kufanya kazi kwa idadi kubwa zaidi ya washiriki kabla ya kupewa idhini ya matumizi kwa umma.

Pamoja na matumaini hayo, mjadala mkubwa umeibuka katika mitandao ya kijamii kuhusu iwapo wanaume wako tayari kutumia njia hiyo.

Baadhi ya wanaume wameeleza bado wana hofu ya madhara ya muda mrefu ambayo hayajathibitishwa kikamilifu, huku wengine wakisema wangependa kusubiri matokeo ya tafiti za muda mrefu kabla ya kufanya uamuzi.

"Wazo la kuwa na sindano inayozuia mbegu za kiume kwa miaka miwili linavutia, lakini ningependa kuona tafiti za muda mrefu kwanza," ameandika mmoja wa wachangiaji katika mjadala ulioibuka mtandaoni baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya utafiti.

Wengine wamehoji kama uwezo wa kupata watoto utarejea kwa watumiaji wote baada ya hidrojeli kuvunjika, wakitaka ushahidi zaidi kabla ya teknolojia hiyo kuanza kutumika kwa umma.

Hata hivyo, wapo wanaoona maendeleo hayo yanaweza kuwa hatua muhimu ya kuwapa wanaume nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika upangaji uzazi na kupunguza utegemezi wa wanawake kutumia njia za homoni ambazo wakati mwingine huambatana na madhara kama kutokwa damu isivyo kawaida, maumivu ya kichwa au mabadiliko ya homoni.

Akizungumza leo Julai mosi, 2026 Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Isaya Mhando amesema uzazi wa mpango unapaswa kuwa uamuzi wa wanandoa wote, badala ya kumwachia mwanamke peke yake.

Amesema hata katika njia zilizopo sasa, ushiriki wa mwanaume ni muhimu.

"Njia ya kalenda, kwa mfano, mwanamume akielewa mzunguko wa hedhi wa mwenza wake anaweza kumkumbusha kama ni kipindi salama au si salama. Hata matumizi ya kondomu yanahitaji maamuzi ya pamoja," amesema.

Dk Mhando amesema pamoja na vasectomy kuwapo kwa muda mrefu, bado haijapokewa kwa kiwango kikubwa kutokana na mitazamo mbalimbali ya jamii.

Kuhusu teknolojia mpya kama ADAM, amesema jambo la msingi ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi.

"Katika afya hatumlazimishi mgonjwa kutumia huduma fulani. Kazi ya mtaalamu ni kumweleza inafanyaje kazi, faida zake, changamoto zake na kumruhusu aamue kwa hiari yake. Teknolojia kama hizi haziji kuchukua nafasi ya uchaguzi wa mtu bali kuongeza chaguo," amesema.

Ameeleza uwezo wa mbegu kutunga mimba hutegemea ubora wake, idadi na uwezo wake wa kuogelea kuelekea kwenye yai.

"Ikiwa teknolojia itaweza kupunguza uwezo wa mbegu kusafiri au kuzifanya zisifike kwenye yai bila kuathiri afya ya mwanamume, basi inaweza kuwa chaguo jingine la uzazi wa mpango, lakini hilo lazima lithibitishwe kisayansi," amesema.

Kwa mujibu wa tafiti za awali zilizochapishwa mwaka 2025 ikiwamo ya Preclinical Development of a Novel Injectable Hydrogel for Vas-Occlusion, hidrojeli hiyo ilionesha matokeo mazuri katika majaribio ya maabara na kwa wanyama.

Watafiti walibaini hidrojeli hiyo hujigandisha ndani ya sekunde 30 baada ya kudungwa na ina uwezo wa kuhimili shinikizo linalotokea wakati wa kumwaga shahawa. Vipimo vya usalama pia vilionesha haikusababisha sumu kwa seli, mzio, muwasho wala mabadiliko ya kijenetiki.

Aidha, utafiti wa miaka miwili kwa mbwa ulionesha mwitikio mdogo wa tishu katika eneo lililodungwa bila madhara makubwa yaliyoripotiwa.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa, matokeo ya majaribio kwa wanyama hayawezi kutosha kuthibitisha usalama kwa binadamu, ndiyo maana hatua zote za majaribio ya kitabibu ni muhimu kabla ya teknolojia yoyote kuidhinishwa.

Kwa zaidi ya miaka 50, wanasayansi wamekuwa wakitafuta njia salama na zinazoweza kurejeshwa za uzazi wa mpango kwa wanaume.

Mwaka 2016, utafiti mkubwa uliofadhiliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ulijaribu sindano ya homoni kwa wanaume zaidi ya 300, lakini ulisitishwa mapema kutokana na madhara yaliyoripotiwa, ikiwamo chunusi, mabadiliko ya hisia na maumivu sehemu ya sindano.

Baadaye tafiti zilielekezwa kwenye geli za homoni pamoja na dawa zisizo za homoni, lakini nyingi bado zipo katika hatua za majaribio.

Iwapo ADAM itathibitishwa kuwa salama, yenye ufanisi na inayoweza kurejesha uwezo wa uzazi baada ya kukamilika kwa majaribio yote ya kitabibu, inaweza kuwa moja ya maendeleo makubwa zaidi katika afya ya uzazi kwa wanaume katika miongo ya hivi karibuni.