GGML yaimarisha ushiriki wa Watanzania sekta ya madini
Kamishina wa Madini, Dk Abdulrahman Mwanga(katikati) akitoa tuzo udhamini wa Jukwaa la tano la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini(LCCF 2026) kwa meneja rasilimali watu wa mgodi wa Geita Gold Mining Limited(GGML) Dominic Marandu.
Muktasari:
- Ni baada ya uwepo wa kilio kikubwa cha Watanzania kukosa fursa za ushirikishwaji katika sekta ya madini, ambacho Serikali imekitatua.
Mwanza. Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) umeendelea kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini kupitia ajira, ukuzaji wa viongozi wazawa, mafunzo kwa vitendo na kuongeza manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za ndani, hatua inayochochea maendeleo ya sekta hiyo na uchumi wa Taifa.
Hayo yalisemwa jana, Jumamosi, Julai 25, 2026, jijini Mwanza katika kongamano la tano la uzingatiaji wa maudhui ya ndani (Local Content Compliance Forum – LCCF 2026) na Ofisa Manunuzi Mwandamizi wa GGML, Cyprian Mtweve.
Amesema kampuni hiyo imeweka mkazo katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, utoaji wa huduma na uongozi wa sekta ya madini.
Mtweve amesema matokeo ya mkakati huo yanaonekana wazi, ambapo asilimia 98 ya wafanyakazi wa GGML na wakandarasi wake ni Watanzania, huku idadi ya wafanyakazi na wakandarasi ikifikia 7,089.
Amesema zaidi ya asilimia 80 ya nafasi za uongozi ndani ya kampuni zinashikiliwa na Watanzania, jambo linaloonesha dhamira ya kampuni ya kuwakuza wazawa katika nafasi za uamuzi.
"Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi za ajira, wanapanda katika ngazi za uongozi na wanakuwa sehemu ya maendeleo ya sekta ya madini. Tunaamini rasilimali za madini zinapaswa kuwanufaisha Watanzania kupitia ajira, ujuzi na fursa za biashara," amesema Mtweve.
Kuhusu utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani, amesema katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, asilimia 95 ya malipo yote ya manunuzi yaliyofanywa na GGML yalielekezwa kwa kampuni za Kitanzania, huku asilimia tano pekee zikielekezwa kwa kampuni za nje.
Amesema hatua hiyo imeongeza fursa za biashara kwa wazawa, imeimarisha uchumi wa ndani na kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
"Tunataka kuona kampuni nyingi zaidi za Kitanzania zinakua na kushindana katika soko la sekta ya madini. Hii ndiyo maana ya maudhui ya ndani, siyo tu kununua bidhaa, bali kujenga uwezo wa wazawa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini," amesisitiza.
Mbali na ajira na manunuzi, Mtweve amesema GGML imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema programu hizo zinawapa vijana nafasi ya kupata uzoefu wa kazi, kufanya tafiti na kukuza ujuzi unaohitajika katika sekta ya madini.
Wafanyakazi wa mgodi wa Geita Gold Mining Limited( GGML) wakiwa wamebaba tuzo ya udhamini wa Jukwaa la tano la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini(LCCF 2026) wakati wa kufunga jukwaa hilo hivi karibuni jijini Mwanza.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo katika elimu na mafunzo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha Watanzania wanakuwa na utaalamu unaohitajika ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji na huduma zinazohusiana na sekta hiyo.
Katika eneo la matumizi ya nishati, Mtweve amesema mwaka 2024 GGML iliunganishwa na huduma ya umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia Gridi ya Taifa, hatua iliyosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mafuta yaliyokuwa yakitumika kuzalisha umeme mgodini.
Amesema hatua hiyo imepunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha juhudi za kampuni katika kulinda mazingira.
Aidha, amesema GGML imeendelea kuzipa nafasi kampuni za Kitanzania kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, akitaja Blue Coast, inayotoa huduma za usafirishaji, pamoja na State Oil Company, kama baadhi ya washirika wa ndani wanaonufaika na fursa zinazotolewa na kampuni hiyo.
Akifungua kongamano hilo Julai 22, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema Watanzania wameongeza ushiriki wao katika sekta ya madini, wakishika nafasi mbalimbali za ajira, uongozi na utoaji wa bidhaa na huduma, hatua aliyosema ni matokeo ya utekelezaji wa sera na sheria za ushirikishwaji wa wazawa.
Mavunde alisema hali ilivyo sasa ni tofauti na miaka ya nyuma, ambapo Watanzania walikuwa wakinufaika kwa kiwango kidogo na rasilimali za madini.
Alisema kwa miaka mingi kulikuwa na malalamiko kwamba kampuni za madini zilitegemea bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, hata kwa mahitaji ambayo yanaweza kupatikana nchini.
Kuhusu malalamiko ya baadhi ya wawekezaji kuhusu mabadiliko ya sheria, alisema hakuna sheria mpya iliyotungwa, bali Serikali inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini ya mwaka 2017, hususan Kifungu cha 133 kinachohusu ushirikishwaji wa Watanzania na uwajibikaji kwa jamii.
Alisema Serikali imebaini baadhi ya wawekezaji walikuwa wakitumia mianya ya sheria kwa kuingia ubia na Watanzania ambao hawakuwa na shughuli zinazofanana na kampuni zao ili kukidhi matakwa ya kisheria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo, alisema utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji wa wazawa umeendelea kuimarika, akibainisha kuwa idadi ya kampuni zilizowasilisha mipango ya ushirikishwaji imeongezeka kutoka 51 mwaka 2018 hadi 1,312 mwaka 2025.