Hakuna hasara inayopata Tanzania kujitoa Comesa

Muktasari:

  • Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe ametaka kufanya utafiti kuhusu hasara na athari za kujitoa kwenye Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) huku Serikali ikitetea uamuzi huo.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema kabla ya kujitoa katika Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa), ilijiridhisha kuwa hakuna hasara inayoipata Taifa kwa kitendo hicho.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Januari 31, 2023, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Momba (CCM) Condester Sichalwe.

Mbunge huyo amehoji Serikali inaonaje kuwa tangu ijitoe Comesa mwaka 2000, haijakutana na wafanyabiashara kufanya utafiti kama kujitoa huko kuna faida au la.

“Serikali ilitakiwa kukaa na wafanyabiashara ili kujua zipi faida walizozipata wakati wakiwa katika soko hilo na zipi hasara wamezipata katika kipindi cha miaka 13 tangu kujitoa katika soko hilo,”amesema.

Akijibu swali hilo, Mbarouk amesema kabla ya kujitoa katika soko hilo walifanya utafiti mkubwa sasa juu ya uamuzi huo na kubaini hakuna hasara wala athari yoyote ya kujitoa katika soko hilo.

Comesa ilianzishwa Desemba 1994 kuchukua nafasi ya Eneo la Upendeleo wa Biashara (Preferential Trade Area-PTA) ambalo lilikuwepo tangu mwaka 1981.

Mwaka 2008, COMESA ilikubaliana kupanua eneo la biashara huru kwa kuongeza kanda mbili za kibiashara za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (Sadc).

Lengo ya Comesa ni kuendeleza eneo huru la biashara kwa kuondoa ushuru na vikwazo kwa wafanyabiashara.

Nchi wanachama wa Comesa ni Uganda, Zambia, Zimbabwe, Somalia, Sudan, Tunisia, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Libya, Madagascar, Malawi, Eswatini, Ethiopia,  Kenya, Djibouti, Eritrea, Misri, Burundi , Comoros , Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).