Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ileje kuja na mkakati ujenzi masoko ya kisasa kuimarisha kilimo

Mkuu wa wilaya ya Ileje, Farida Mgomi akiwa na mmoja wa wananchi katika katika Kijiji Cha Ilulu wilayani humo wakati wa Uzinduzi wa soko la mazao mchanganyiko.

Muktasari:

  • Mpango huo wa Serikali umebainishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Farid Mgomi wakati wa uzinduzi wa soko la mazao na bidhaa mchanganyiko katika Kijiji cha Ilulu, kata ya Isongole wilayani humo.

Ileje. Serikali ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imepanga kuja na mkakati wa ujenzi wa masoko ya kisasa ya mazao pamoja na kuimarisha mfumo wa ushirika, lengo likiwa ni kuongeza thamani ya bei za mazao yanayozalishwa na wakulima ikiwemo mahindi.

Mpango huo umebainishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Farid Mgomi wakati wa uzinduzi wa soko la mazao na bidhaa mchanganyiko katika Kijiji cha Ilulu, kata ya Isongole wilayani humo.

Mgomi amesema Wilaya ya Ileje itakuja na mpango wa kuweka mazingira rafiki yatakayosaidia ukuaji wa sekta ya kilimo na biashara kupitia ujenzi wa masoko ya kisasa pamoja na kuimarisha mfumo wa ushirika ili kuboresha masilahi yao na kuongeza faida katika shughuli za kilimo.

“Awali, mlikuwa mnatumia soko la mazao lililopo Isongole na sasa fursa imekuja hapa kwenu Ilulu, hivyo nawahimiza wananchi litumieni kikamilifu soko hilo jipya kama chachu ya maendeleo ya uchumi wa Wilaya ya Ileje.

“Kuzinduliwa kwa soko hili ni mwanzo mpya wa kuanza kuboresha mazingira ya ndani ya kukuza biashara ya mazao mchanganyiko yanayozalishwa na wakulima ndani ya wilaya yetu na mkoa mzima, hivyo tutaendelea kuanzisha na kujenga masoko mengine katika maeneo yatakayokuwa sehemu ya kuwakusanya pamoja wakulima,” ameongeza Mgomi.

Mgomi amewataka wafanyabiashara na wananchi watakaotumia soko hilo kuzingatia kanuni za usafi na utunzaji wa mazingira ili kuzuia magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha soko linabaki salama na lenye mazingira bora kwa wafanyabiashara na wanunuzi.

Ameeleza kuwa uwepo wa soko hilo utasaidia kutokomeza biashara holela ya mazao kwa kuweka mfumo rasmi wa biashara unaozingatia sheria na taratibu za Serikali.

“Kufuatia uwepo wa soko hilo, niwasisitize wafanyabiashara kutumia vipimo vya mizani vilivyothibitishwa na Serikali kupitia Wakala wa Vipimo Tanzania ili kulinda haki za wanunuzi na wauzaji pamoja na kujenga mazingira ya biashara yenye uaminifu,” amesema Mgomi.

Ameongeza kuwa kutokana na soko hilo kuwa karibu na mpaka wa Tanzania na Malawi, wananchi wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zote wanaposhirikiana na raia wa nchi jirani katika shughuli za biashara na uzalishaji mali.

Amesema wakulima wilayani humo wanatakiwa kujiunga na Vyama vya Ushirika wa Msingi (Amcos) ili kuboresha maslahi yao na kuongeza faida katika shughuli za kilimo pamoja na biashara ya mazao.

Mgomi amesema vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika kuwaunganisha wakulima ili kuwa na nguvu ya pamoja ya kujadiliana bei za mazao, kupata masoko ya uhakika, huduma za kifedha, pembejeo za kilimo kwa gharama nafuu pamoja na mafunzo ya kuongeza tija katika uzalishaji. 

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ilulu, Christina Makere amesema kuwa uwepo wa soko la mazao na bidhaa mchanganyiko katika kijiji hicho utakuwa chachu ya kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwawezesha kupata soko la uhakika la bidhaa na mazao yao.

Amesema soko hilo, pia, linatarajiwa kuongeza mapato ya halmashauri kupitia ukusanyaji wa ushuru na tozo mbalimbali, kuongeza ajira kwa vijana pamoja na kuimarisha shughuli za biashara katika eneo hilo.

Richard Simkoko, mkazi wa kijiji cha Ilulu amesema soko hilo limekuwa likisubiriwa kwa muda mrefu, hivyo kuanzishwa kwake litaleta tija kwa wakulima kuuzia mazao yao kwa karibu kwani awali walikuwa wakifuata umbali mrefu katika soko la mazao Isongole.

Amesema kuanzishwa kwa soko hili kutasaidia kuongeza mzunguko wa fedha huku akipongeza viongozi wa halmashauri ya Ileje waliokubali wazo la kuanzishwa kwa soko hilo ambapo wamesaidia kusogeza huduma kwa wananchi.