Jinsi ya kukabiliana na uhaba wa dola nchini

Nchi mbalimbali duniani kwa sasa zinapitia kadhia ya uhaba wa Dola ya Marekani ambayo ni sarafu muhimu inayotumika kwa kiasi kikubwa katika malipo ya biashara kimataifa.

Jambo hili limeibua changamoto ya kiuchumi zaidi kwa nchi zinazoendelea na zinazoagiza kwa wingi bidhaa kutoka nje ya nchi.

Katika nadharia kiuchumi uhaba wa sarafu yoyote kwa mfano dola unaweza kutokea ikiwa nakisi katika uwiano wa mahitaji ya nchi kati ya uagizaji wa bidhaa na huduma yameongezeka mtawalia ikilinganishwa na mauzo yake kwenda nje ya nchi.

Mfano, mauzo ya bidhaa kama korosho, chai, pamba, na shughuli za utalii yataongezeka, uingiaji wa fedha za kigeni nchini utaongezeka kupitia malipo yanayofanyika, hali kadhalika kama uwekezaji kutoka nje ya nchi utaongezeka.

Kutokana na kuwa dola ndiyo sarafu kubwa ya kibiashara, tunaweza kusema pia itaongeza kiasi cha sarafu hiyo kinachoingia katika uchumi wa nchi.

Kwa upande wa mwingine uagizaji wa bidhaa kama nguo, mafuta, vifaa vya ujenzi, malipo ya madeni ya Serikali na mengine, inaongeza matumizi ya sarafu za kigeni kwenda nje ya nchi, na kwa sababu malipo yake mengi yanafanyika kwa kutumia dola, tunaweza kusema yanapunguza akiba ya dola.

Kwa ujumla, uhaba unaweza kutafsiriwa ikiwa itatokea kupungua kiasi cha dola kinachoingia nchini, au kuongezeka kwa bei ya sarafu ya dola dhidi ya Shilingi ya Tanzania, hali ambayo inaongeza matumizi ya shilingi ili kununua dola chache.

Taarifa za BoT kuhusu tathmini ya mwenendo wa kiuchumi kwa Aprili 2023 zinaonyesha kiasi cha jumla cha akiba ya fedha za kigeni kimepungua kwa asilimia 10.2 ambayo ni sawa na kiasi cha dola milioni 569.1, kutoka dola 5.581.6 kilichorikodiwa muda kama huo Aprili mwaka jana kufikia dola bilioni 5.012.5 Aprili 2023.

Wakati huohuo nakisi katika uwiano wa biashara ya kimataifa (current account deficit) imeongezeka kwa Dola bilioni 2.5. Kinachoweza kufanyika ni nchi yenye uhaba wa dola kutumia sarafu za nchi washirika ili kufanikisha malipo ya biashara na kuepuka mahitaji ya Dola.

Mfano mzuri hivi karibuni nchi za Tanzania na India zimekubaliana mtindo mpya wa kufanya malipo ya biashara baina yao kupitia utaratibu ulioitwa vostro account, ambapo sarafu ya Indian Rupee na Shilingi ya Tanzania ndizo zitatumika kufanya malipo ya biashara kati ya nchi hizi mbili moja kwa moja bila kuhitaji Dola.

Utaratibu kama huo unasaidia kupunguza kuhitaji dola, na msukumo wa kuongezeka bei na sarafu ya dola dhidi ya shilingi utapungua.

Pia jambo lingine la muhimu ni kuwa na mkakati mahususi wa kupunguza uagizaji wa bidhaa kwa bidhaa zinazoweza kuzalishwa ndani ya nchi, kwa mfano mafuta ya kula, sukari, nguo na bidhaa nyingine ambazo zinatumia fedha ya kigeni kama dola katika uagizaji, na itaweza kusaidia kupunguza matumizi ya dola katika baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuepukika tukiwekeza.

Kwa sasa akiba yetu ya fedha za kigeni inatosha kuhudumia uagizaji wa bidhaa kwa angalau kipindi cha miezi 4.5 ijayo, kwa mujibu wa malengo ya sera ya fedha.

Hata hivyo, mfuko huo unaweza kutunishwa kwa kuongeza mauzo ya bidhaa mbalimbali kwenda nje ili kuingiza fedha za kigeni nchini.