Usikope kwa sababu unakopesheka benki

Mtweve Malima ni mfanyabiashara wa nafaka katika maduka yaliyopo Ubungo, Dar es Salaam. Malima ni kijana ambaye anafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha anahudumia wateja wake waridhike na yeye apate faida kuendesha maisha yake na familia.

Kutokana na mzunguko wa pesa kuwa mgumu, mara nyingi amejikuta akiingia katika mikopo ambayo inampa shida kuilipa. Kila kukicha hali yake imeendelea kuwa mbaya, wadeni wanashinda dukani kwake kudai pesa.

Pesa zote anazofanya mauzo, Malima anajikuta anawalipa wanaomdai papo kwa papo hadi kufikia hatua ya kukosa pesa ya kuagiza bidhaa nyingine.

Anachanganyikiwa wakati biashara yake inazidi kuyumba. Mikopo imekuwa mwiba kwake kiasi cha kufikia kutangazwa kwa mnada wa nyumba yake anayoishi.

Akiwa katika harakati za kufufua duka lake, anakutana na mtaalamu wa fedha binafsi na kumueleza changamoto ya madeni aliyonayo.

Mtaalamu anamwambia kuwa sio kila mkopo huwa unamaana ya kumsaidia mkopaji. Ipo mikopo ambayo haimsaidii mkopaji bali mkopeshaji. Mkopaji unatakiwa kuangalia kama kweli unahitaji kukopa na sio kukopa kwa kuwa unakopesheka.

Kila mkopo huwa na taratibu na mahitaji yake. Ni lazima mkopaji ajihakikishie mahitaji ya mkopo husika kama yanaendana na malengo yake ya kukopa. Kinyume cha hapo huna sababu ya kokopa.

Mshauri akaendelea, kama unataka kukopa pesa kwa ajili ya kuwekeza shambani, unatakiwa kuchukua mkopo ambao marejesho yake yatasubiri mpaka kipindi cha mavuno. Ukichukua mkopo wa kupeleka shamba wakati masharti yake ni kuanza kulipa baada ya mwezi mmoja, hapo lazima uingie katika matatizo ya kulipa madeni bila kuzalisha.

Mkopo mzuri ni ule ambao unakidhi mahitaji ya biashara, unarejesha deni husika na kubakiza faida. Kwa kuwa na mkopo kama huu, kila wakati mkopaji anapomaliza kurejesha mkopo wake, anakuwa katika hali bora kuliko kabla hajachukua mkopo.

Pia mkopaji anatakiwa kuangalia riba ya kurejesha mkopo husika na faida itakayozalishwa katika biashara kutokana na mkopo husika.

Ikiwa faida inayopatikana ni kubwa kuliko riba ya mkopo. Ikiwa faida inakuwa ndogo kuliko faida, mkopaji ataishia katika hali mbaya kuliko alivyokuwa kabla hajaamua kukopa.

Hili tatizo lipo zaidi pia kwa wafanyakazi, wengi wanaingia kwenye mikopo kwa sababu wanakopesheka, hivyo baadaye fedha za mkopo zinakwisha kwa matumizi ya kawaida yasiyo na tija.