Kampuni ya Old Mutual yauza hisa zote

Muktasari:
- Hisa zimeuzwa kwa kikundi cha wanahisa wenye hisa chache ndani ya kampuni ya UAP Insurance.
Dar es Salaam. Kampuni ya kimataifa ya Old Mutual Limited imetangaza kuuza hisa zake zote za bima kwa kampuni ya UAP Insurance Tanzania.
Zimeuzwa kwa kikundi cha wanahisa wenye hisa chache ndani ya kampuni ya UAP Insurance.
Mauzo ya hisa hizo yaliyofanyika hivi karibuni yatakuwa rasmi baada ya kuidhinishwa na mamlaka, ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira).
Uamuzi huo unatokana na mapitio ya kina ya kimkakati ya biashara kwa kuzingatia malengo ya muda mfupi na mrefu ya kampuni ya Old Mutual.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Old Mutual Holdings, Arthur Oginga amesema: “Tangu tuinunue UAP Insurance Tanzania mwaka 2015, imekuwa ni dhamira yetu kukuza biashara kwa lengo la kuifanya kampuni iwe miongoni mwa watoa huduma za kifedha wanaoongoza kwenye soko la huduma hizo nchini Tanzania.”
Katika kutekeleza hilo, amesema wamefanya uwekezaji wa kimkakati kuhakikisha biashara inabaki kwenye msingi imara na kuweza kushindana kwa mafanikio.
“Hata hivyo, biashara nchini Tanzania imekabiliwa na changamoto katika kurudisha mtaji kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji na kimazingira. Tumetathmini mikakati ya kupata uongozi wa soko nchini Tanzania lakini hatuoni tena njia ya kufikia lengo hili la kimkakati,” amesema.
Amesema tathmini yao imeonyesha watahitaji kufanya uwekezaji mkubwa zaidi ili kuwa kampuni inayoongoza sokoni.
“Kutokana na hali hiyo, tumeamua kuuza hisa zetu kwa Strategic Ventures Company Limited ambayo ni muungano wa wanahisa wachache wa UAP Insurance Tanzania Limited,” amesema.
Amesema UAP Insurance Tanzania imesema huduma na mahusiano na wateja na wadau wake nchini Tanzania yatabaki vilevile na itashirikiana na wamiliki wanaoingia ili kuendeleza huduma thabiti kwa wateja.
"Tunatumia fursa hii kuwataarifu wateja wetu na wadau wetu kwamba watarajie kuendelea kupata huduma bora zaidi," amesema.
Amesema uwekezaji wa Old Mutual kwenye ukanda wa Afrika Mashariki bado ni thabiti. Hata hivyo, ukuaji huo unahitaji kuwa endelevu, kwa masilahi mapana ya wadau.
"Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tuliamua kutumia jina la Old Mutual kuimarisha chapa yetu Afrika Mashariki. Katika mwaka ujao, zoezi hili litaendelea na tutaimarisha uwekezaji ili kukuza biashara na kuendelea kuwa bora katika huduma jumuishi za kifedha," amesema Oginga.