Maeneo mawili ya kukupa utajiri Tanzania
Muktasari:
- Shughuli za kifedha na bima zinaongoza kwa ukuaji kwenye Pato la Taifa katika robo ya tatu ya mwaka 2023, ambapo Sh34 trilioni zimewekwa katika sekta hiyo inayohusika na ulipaji wa fidia katika majanga.
Dar es Salaam. Umewahi kufikiria kuwekeza katika huduma za kifedha na bima? Kama bado anza sasa, ripoti ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) katika robo ya tatu ya mwaka 2023 imeonyesha sekta hiyo ndio iliyokua zaidi.
Licha ya kukua zaidi, sekta ya fedha na bima imekuwa ya pili katika kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa kwenye kipindi hicho.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Januari 2024, inaonyesha ukuaji wa sekta hiyo inayohusika na huduma za fidia nchini ni asilimia 18.7 katika robo ya tatu ya mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 8.7 katika robo kama hiyo mwaka 2022.
“Ukuaji huo ulichangiwa na kuongezeka kwa kiwango cha amana kwa asilimia 24.8 kutoka Sh27.7 trilioni katika robo ya tatu 2022 hadi Sh34.6 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2023,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Hii ina maana kuwa amana iliyopo katika shughuli za kifedha na bima ni asilimia 78 au zaidi ya robo tatu ya Bajeti Kuu ya Tanzania ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo ni Sh44.39 trilioni.
Ripoti inabainisha kuwa huduma za kifedha na bima zinajumuisha huduma za kifedha, bima, ufadhili wa pensheni wa hiari, msaidizi wa huduma ya kifedha. Pia, inajumuisha shughuli za umiliki wa mali, kama vile kampuni miliki, amana, fedha na mashirika kama hayo ya kifedha.
Mchumi mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema ongezeko kubwa la ukuaji kwa sekta hiyo linamaanisha Watanzania wameelewa umuhimu wa bima katika ulinzi wa mali zao tofauti na miaka ya nyuma.
“Bima kukua kwa kiwango kikubwa inaonyesha ni namna gani watu wameelewa umuhimu wake na wanaenda kuzikatia mali zao na vitu vingine.
“Pia, unaweza kuwa mfano mzuri wa Watanzania wanaomiliki mali za thamani ikiwamo nyumba na vyombo vya usafiri wameongezeka,” amesema Profesa Kamuzora.
Profesa Kamuzora amesema ongezeko hilo linachochea ukuaji wa uchumi kwani mzunguko wa fedha unaongezeka kwa sababu kampuni za bima zinafanya uwekezaji tofauti.
“Fedha zinazokusanywa na kampuni za bima haziwekwi tu ndani bali zinaendelea kufanya uwekezaji wa aina tofauti kitu kinachosaidia kuongeza mzunguko wa fedha,”ameongeza.
Naye Agnes Mroso, mkazi wa Kijichi, jijini hapa mali zake amezikatia bima kwa kuogopa majanga.
“Binafsi mali zangu (nyumba na gari) nimezikatia bima kwa sababu majanga hutokea muda wowote, Watanzania wengi sasa hivi wanajua umuhimu wa bima katika kufidiwa.
“Kuna wakati bima ya gari ikiisha mpaka unaogopa kutoka nayo kwa sababu unahofia kikitokea kitu chochote kibaya labda ajali itakuwa ngumu kufidiwa,” amesema na kuongeza Agnes.
Kwa upande wake, Mack Patrick ambaye ni mchumi amesema ongezeko hilo katika huduma za kifedha na bima ni ushahidi wa kuongezeka kwa mzunguko wa fedha na uchumi nchini.
“Katika upande wa huduma za kifedha, hii inamaanisha fedha zilizunguka sana mifukoni mwa wananchi na hapa faida yake ni kuimarika kwa uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja,” amesema Mack.
Mzunguko wa fedha
Kuhusu mzunguko wa fedha kuongezeka, kati ya Januari hadi Novemba 2023 kulikuwa na mwenendo chanya wa mzunguko wa fedha ambapo wastani wa ongezeko lilikuwa asilimia 13.8.
Hii maana yake ni kuwa vyuma vililegea zaidi mwaka 2023, kwani ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha Novemba 2023, jumla ya fedha za ndani zilizokuwa kwenye mzunguko wa uchumi nchini na nje ya nchi (M3) zilikuwa na thamani ya Sh43.58 trilioni ikilinganishwa na Sh38.33 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022.
Kwa mujibu wa BoT, kati ya fedha hizo zilizopo kwenye mzunguko, Sh10.14 trilioni ni fedha za kigeni na zilizosalia ni sarafu za ndani ambazo zipo kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na akaunti za miamala na fedha taslimu zilizopo mifukoni mwa watu.
Ripoti hiyo inayoangaza mwenendo wa kiuchumi wa kila mwezi inaonyesha Novemba 2023 fedha zilizozunguka mifukoni mwa watu zilikuwa na thamani ya Sh6.3 trilioni ikilinganishwa na Novemba 2022 ambapo mifukoni kwa watu kulikuwa na Sh5.6 trilioni.
Unapataje fedha sekta ya bima
Mchumi ambaye pia ni mtaalamu wa bima, Oscar Mkude amesema ili unufaike moja kwa moja katika sekta ya bima ni lazima uwe mwanataaluma au wakala wa bima fulani.
“Biashara ya bima inahitaji kuwa na mtaji mkubwa sana watu wengi wanaweza kunufaika na mnyororo wake wa thamani kwa kuajiriwa kama mtaalamu wa bima au awe wakala wa kampuni Fulani.
“Mara nyingi watu wengi wanapata fedha kwa kuwa mawakala kwasababu kampuni hizi hazijajitanua katika ngazi ya jamii hivyo mawakala wao ni wanufaika wa mfumo huu,” amesema Mkude.
Shughuli nyingine zinazochangia ukuaji wa GDP
Shughuli nyingine zinazochangia ukuaji wa Pato la Taifa ni Habari na mawasiliano (asilimia 11.3), Madini na uchimbaji mawe (asilimia 10.2) na umeme (asilimia 9.7).
Mamlaka ya bima ya Taifa (inafanya nini)
Shughuli zote za bima nchini zinasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) ambayo majukumu yake makubwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za bima.
“Majukumu ya Mamlaka ni pamoja na Kutoa elimu ya bima kwa umma, kusajili kampuni za bima nchini, kusimamia na kukagua mwenendo wa kampuni za bima nchini.
“Kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya huduma za bima na kusimamia biashara ya bima na masula yanayohusika na bima kwa mujibu wa sheria,” majukumu hayo yameainishwa katika tovuti ya Tira.
Kutoka mtandaoni