Wadau wataka magari ya Serikali yakatiwe bima

Kamishna wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware, akizungumzia juu ya wajibu wa serikali kulipia magari yake bima.

Muktasari:

  • Kutokana kutokukatia bima magari ya Serikali kumekuwa na usumbufu kulipwa fidia waathirika wanapopatwa majanga yatokanayo na ajali magari ya Serikali.

Arusha. Wadau wa bima nchini wameiomba Serikali kukatia magari yake bima ili kusaidia wananchi kulipwa fidia yanapowasababishiwa majanga.

 Wamesema kuwa mlolongo wa kulipwa fidia kwa majanga yanayosababishwa na magari ya Serikali ni mrefu hali ambayo baadhi yao hujikuta wanakata tamaa ya kudai haki yao.

Wadau hao wamesema hayo katika mkutano wa kupokea na kusikiliza maoni na malalamiko ya bima Kanda ya kaskazini ilioandaliwa na mamlaka ya usimamizi wa bima Tanzania iliyofanyika jijini Arusha.

"Katika sekta binafsi fidia hulipwa ndani ya siku 45 ukikidhi vigezo, lakini kwa Serikali mlolongo wa kudai fidia ni mrefu kwa sababu lazima ofisi ya mwanasheria mkuu iandae mashtaka ya kwenda mahakamani hadi kesi itakapokamilika zaidi ya miaka ndipo mhusika alipwe fidia hivyo wengi wanachoka na kukata tamaa na kupelekea kukosa haki zao," Alisema Elizabeth Shirima.

Meneja wa Bima tawi la Arusha, Iddi Mbogo Meticulous General alisema kuwa wanapokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja wakidai kulipwa fidia na magari ya Serikali lakini wanashindwa kutokana na hali hiyo.

"Tunaiomba Serikali kuona namna ya kuyafanyia kazi malalamiko haya kwa kuweka mifumo mizuri ya fidia, lengo ikiwa ni kuwasaidia wananchi kupata haki zao kwa wakati kama ilivyo kwa Zanzibar ambao magari yote ya umma yana bima," alisema Mbogo.

Akizungumzia hilo Kamishna wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware alisema kuwa mtu akisababisha ajali na dereva wa Serikali ana haki ya kulipwa fidia kulingana na madhara.


"Serikali ina jukumu la kulinda maslahi ya walipakodi, hivyo endapo dereva wake atasababisha ajali, wahusika wana haki ya kulipwa fidia," alisema Dk Saqware.

Alisema kuwa Wizara ya Fedha kupitia hazina inatakiwa kuwajibika kwa niaba ya taasisi ya umma iliyosababisha ajali hivyo watende haki kuondoa kero hiyo kwa wananchi.

Naye Meneja wa Bima Kanda ya Kaskazini, Gladness Lema amesema kuwa mkutano huo uliowakutanisha wadau wa bima zaidi ya 250 wametoka mikoa ya Kanda ya kaskazini ikiwemo Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

"Leo tumekuja kupata maoni ya maswala ya bima lakini pia kusikiliza malalamiko ili kuboresha zaidi huduma hizi katika soko la tasnia yetu," alisema Lema.