Tira yazitaka taasisi kujiunga na huduma ya dhamana kupata leseni

Muktasari:

  • Tira yazitaka taasisi za bima kuweka asilimia 50 ya mtaji wake Tira kulinda amana za wateja wake pindi changamato za kiuendeshaji zinapojitokeza kupungukiwa na fedha au kufirisika.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Saqware amesema kampuni zinazotoa huduma ya bima zitakazoshindwa kuweka asilimia 50 ya mtaji wake kwenye akaunti ya ‘Tira Trust’ zitanyimwa leseni ya kufanya shughuli hizo.

Akizungumza Dar es Salaam, leo Desemba 4, 2023 baada ya Tira kuingia makubaliano na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), kwa ajili ya kutoa huduma ya Tira Trust, Dk Baghayo amesema akaunti hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa kanuni namba 20 ya sheria za bima iliyoanzishwa mwaka 2009.

"Sheria inataka makampuni yote ya bima nchini yawekeze kiasi kisichopungua asilimia 50 ya mitaji yao kwenye akaunti ya dhamana itakayoanzishwa na Tira kuweka asilimia hiyo haihitaji hamasa bali ni utekelezwaji wa sheria na kampuni ambazo hazitafanya hivyo zitanyimwa leseni," amesema.

Amesema fedha zinazowekwa kwenye akaunti hiyo zinalenga kumlinda mteja wa bima pindi kampuni itakapokuwa imepungukiwa fedha kwa sababu mbalimbali za kiuendeshaji au kufirisika.

"Tira imeanzishwa kwa sheria sura namba 394, moja kati ya majukumu yake ni kulinda haki za mteja kwahiyo akaunti hiyo ambayo PBZ imetimiza masharti yake kati ya mabenki mengine matano yaliyofanya hivyo inatumika na mamlaka hiyo kama sehemu ya kumlinda mteja," amesema.

Pia, Dk Baghayo amezisisitiza benki zinazotoa huduma hiyo waangalie na wapaswa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na akaunti hiyo.

Amesema masharti hayo ni pamoja na fedha hizo za amana zimewekwa kwa jina la Kamshina wa Tira na haziwezi kutolewa na kampuni yeyote ya bila idhini ya kamshna wa taasisi hiyo. 

"Masharti mengine ni akaunti hiyo haitegemei kutozwa kodi yeyote kwa sababu ni dhamana na masharti mengine, malipo na miamala yote inatakiwa kufanyika kwa mfumo wa dijitali," amesema.

Amesema kwa msingi huo ni lazima benki zinazoanzisha akaunti hiyo ni muhimu kuwa na mfumo wa kidijitali utakaowezesha kuwasiliana na mamlaka ya bima nchini pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mifumo inatakiwa isomane kwa kuwa hakuna kuonana ana kwa ana.

"Fedha zilizopo kwenye akaunti ya amana ya Tira ni fedha za bima isipokuwa mtu anaruhusiwa kuwekeza Benki Kuu au kuzibakiza kwenye akaunti hiyo," amesema.

Amesema kila zikitolewa anapaswa kuzipeleka kwenye hati fungani za BoT na zikiiva zinakuwa na fedha za ziada kampuni ya bima ikizihitaji zitachukuliwa kwa idhini ya Kamshina wa bima.

Ofisa Masoko na Mahusiano wa Benki ya BPZ, Salim Hassan Iddi amesema pamoja na uzinduzi huo walikuwa na mafunzo kwa wadau mbalimbali wa bima kupata ufahamu kuhusiana na Tira akaunti.

"Na namna wanavyoweza kuitumia benki ya watu wa Zanzibar katika Tira Trust akaunti kwa mantiki hiyo huduma hiyo ina masharti yake na taasisi yetu ipo tayari kutekeleza masharti yote," amesema.

Amesema fedha hizo zitakuwa dhamana ya mteja wa bima na taratibu zake zimeeleza namna fedha zitakavyokuwa zinaingizwa kwenye akaunti hiyo ambazo zinaweza kunufaisha makampuni ya bima kimtaji na uwekezaji.

"Benki yetu itakuwa inatoa misaada kwa makampuni yatakayotumia huduma hiyo kupitia benki hiyo kutafuta fursa za kuwekeza Benki Kuu tutaweka utaratibu mzuri," amesema.