2023 mzunguko wa fedha uliongezeka Tanzania, wewe ulikugusa?

Muktasari:

  • Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha Novemba 2023, jumla ya fedha zilizokuwa kwenye mzunguko wa uchumi ndani ya nje (M3) zilikuwa na thamani ya Sh43.58 trilioni ikilinganishwa na Sh38.33 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022.

Dar es Salaam.  Inawezekana hukulishuhudia hilo katika shughuli zako za kila siku, lakini takwimu zilizopo zinaonyesha mzunguko wa fedha ulikuwa mkubwa mwaka uliopita ikilinganishwa na mwaka 2022.

Kati ya Januari hadi Novemba 2023 kulikuwa na mwenendo chanya wa mzunguko wa fedha ambapo wastani wa ongezeko lilikuwa asilimia 13.8.

Hii maana yake ni kuwa vyuma vililegea zaidi mwaka 2023, kwani ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha Novemba 2023, jumla ya fedha za ndani zilizokuwa kwenye mzunguko wa uchumi nchini na nje ya nchi (M3) zilikuwa na thamani ya Sh43.58 trilioni ikilinganishwa na Sh38.33 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022.

Kwa mujibu wa BoT, kati ya fedha hizo zilizopo kwenye mzunguko, Sh10.14 trilioni ni fedha za kigeni na zilizosalia ni sarafu za ndani ambazo zipo kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na akaunti za miamala na fedha taslimu zilizopo mifukoni mwa watu.

Ripoti hiyo inayoangaza mwenendo wa kiuchumi wa kila mwezi inaonyesha Novemba 2023 fedha zilizozunguka mifukoni mwa watu zilikuwa na thamani ya Sh6.3 trilioni ikilinganishwa na Novemba 2022 ambapo mifukoni kwa watu kulikuwa na Sh5.6 trilioni.

Kwa makadirio ya idadi ya watu milioni 63 mwaka 2023, ina maana katika kipindi husika kila Mtanzania alikuwa na wastani wa Sh100,000 mbali na fedha zilizopo kwenye akaunti za miamala na uwekezaji wao kwenye masoko ya fedha akiba zao zilizopo kwenye akaunti za nje ya nchi.