Asilimia 60 fedha za BoT zinabaki kwenye mzunguko

Naibu Gavana wa Benki Kuu (BoT),Dk Yamungu Kayandabila akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited  (MCL) baada ya kumalizika semina kwa wabunge iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

BoT imeeleza hayo leo ilipokutana na wabunge na kuwaeleza kwa kina kuhusu shughuli za benki hiyo mjini Dodoma leo


Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema takribani asilimia 60 ya fedha wanazozitoa zinabaki kwenye mzunguko nje ya benki za biashara.

Akiwasilisha mada ya majukumu ya BoT kwa wabunge leo Jumamosi Septemba 8, 2018, naibu Gavana wa benki hiyo,  Yamungu Kayandabila amesema hali hiyo imechangia kupunguza ufanisi kwenye utekelezaji wa sera.

“Matarajio ni kwamba maendeleo ya teknolojia ya mifumo ya malipo pamoja na baadhi ya benki za biashara kuendelea kutoa huduma za kibenki kupitia uwakala,” amesema.

“Maendeleo hayo yatawezesha watanzania wengi kupata huduma za kibenki kwa gharama nafuu na hivyo kusaidia kupunguza kiasi cha fedha zilizotolewa mikononi nje ya benki za biashara.”

Pia,  amesema benki hiyo inakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha malipo yote yanafanyika kwa usalama bila wizi wa kiteknolojia kwenye akaunti za mabenki, ATM na mawakala wa huduma za kifedha.

"Pia kumekuwa na chamgamoto ya noti bandia kadri teknolojia inavyoboreshwa na hivyo kufika mikononi mwa wahalifu na kusababisha uwepo wa noti bandia," amesema.

Amesema chamgamoto hiyo imesababisha BoT kuongeza alama za usalama za siri kwenye fedha ambayo ni gharama ya ziada ili kusambaza na uhalifu huo.