Bima za magari kutolea kwenye vituo vya mafuta

Muktasari:

  • Kampuni ya Bima ya Jubilee inatarajia kuanza kutoa huduma za bima za magari katika vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Ili kurahisisha upatikanaji wa bima za magari, kampuni ya Bima ya Jubilee imetangaza kuanza kutoa huduma katika vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam.

Imesema hatua hiyo itawaondolea wananchi usumbufu wa kufuata huduma hiyo katika matawi ya kampuni hiyo, badala yake watazipata pale watakapokwenda kuweka mafuta.

Hayo yameelezwa leo, Oktoba 11, 2023 na Mkurugenzi wa Jubilee Allianz, Dipankar Acharya wakati wa hafla ya makubaliano ya ushirikiano wa utoaji huduma kati ya kampuni hiyo na vituo vya mafuta vya Total Energies na Benki ya NBC.

Amesema lengo la ushirikiano huo ni kusogeza karibu huduma za bima na kurahisisha upatikanaji wake.

“Tunatarajia kufanya hivi nchi nzima kwa sasa tumeanza kutoa huduma za bima katika vituo vya mafuta vya Total Energies vya Dar es Salaam,” amesema.

Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Total Energies, Getrude Mbangile amesema huduma hizo zitapatikana katika vituo vitano jijini hapa.

Amevitaja vituo hivyo ni Oyster bay, Morocco, Malimani City, Kariakoo na Samora.

“Tunacholenga ni kuhakikisha tunatoa huduma jumuishi katika vituo vya mafuta, badala ya mafuta pekee mwananchi akija akutane na huduma nyingine,” amesema.

Elibariki Kasuke kutoka NBC, amesema jukumu lao katika ushirikiano huo ni kuhakikisha wanamwezesha mteja ambaye hatakuwa na fedha ya inayotosheleza kupata huduma hiyo.

“Kinachofanywa ni kulinda hasara inayosababishwa na ajali, tutatoa bima kubwa ambayo gharama yake itakuwa ni asilimia 3.5 ya gharama halisi ya gari husika, lakini tutatoa bima ndogo pia,” amesema.

Amesema benki hiyo inatoa mikopo ya ada ya bima kwa ajili ya kumwezesha muhitaji kulipia bima na marejesho ni kuanzia miezi minne hadi 10.