Kapinga: Bidhaa za Tanzania zimepiga hatua kwa ubora
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga (kulia), akitembelea mabanda ya biashara kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu sabasaba ikiwa ni mara ya pili kwa msimu huu wa Maonesho hayo. Picha na Said Powa
Muktasari:
- Maonyesha ya mwaka huu yamedhihirisha hatua kubwa iliyopigwa na wazalishaji wa ndani, hasa katika usindikaji wa mazao ya kilimo na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora wa juu.
Dar es Salaam. Serikali imesema Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yameonyesha maendeleo makubwa ya sekta ya viwanda nchini hususan katika kuongeza thamani na ubora wa bidhaa pamoja na vifungashio.
Hali hiyo inazifanya bidhaa zinazozalishwa nchini kuendelea kuwa na ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga aliyasema hayo jana Jumatano, Julai 8, 2026 baada ya kufanya ziara ndani ya viwanja hivyo na kushuhudia shughuli mbalimbali zinazoendelea.
Amesema maonesho ya mwaka huu yamedhihirisha hatua kubwa iliyopigwa na wazalishaji wa ndani hasa katika usindikaji wa mazao ya kilimo na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora wa juu.
“Wazalishaji wetu wamepiga hatua kubwa. Sasa tunaona bidhaa nyingi za ndani zenye ubora wa hali ya juu, hasa zile zilizoongezwa thamani. Hata vifungashio vimeboreshwa kwa kiwango kikubwa, jambo linalotia moyo katika ukuaji wa viwanda vyetu,” amesema.
Akizungumza baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo, Kapinga aliwahimiza Watanzania kuendelea kutembelea Sabasaba ili kujifunza teknolojia mpya, kubaini fursa za uwekezaji na kujenga mitandao ya biashara.
Amesema waonyeshaji wapatao 3,800 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanashiriki katika maonesho ya mwaka huu, hali inayoonyesha kukua kwa kasi kwa sekta ya viwanda na uzalishaji nchini.
Miongoni mwa mabanda yaliyotombelewa ni la Nida Textiles, ambapo wageni wanajifunza kuhusu mchakato wa uzalishaji wa nguo na fursa zilizopo katika sekta ya nguo inayozidi kukua.
Waziri huyo pia aliwapongeza vijana wabunifu wanaozalisha matofali ya ujenzi kwa kutumia miamba, akisema ubunifu huo unaonyesha uwezo mkubwa wa vijana wa Tanzania katika kuibua suluhisho za maendeleo ya viwanda.
Katika banda la Suma JKT, waoneshaji wanaonyesha bidhaa na teknolojia mbalimbali, ikiwemo samani zinazozalishwa nchini na mifumo ya kisasa ya ufugaji wa samaki, huku wengine wakionyesha ubunifu unaolenga kuongeza tija katika sekta za kilimo, viwanda na ujenzi.
Kapinga pia alieleza maendeleo yanayopatikana katika sekta ya usafiri safi kupitia banda la BYD, ambapo wageni wanapata fursa ya kuona magari ya umeme, magari mseto na yale yanayotumia gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG).
“Unaweza kuona magari ya umeme, magari mseto na hata yale yanayotumia CNG ambayo yana uwezo wa kusafiri hadi kilomita 600 kwa tanki moja. Pia kuna mashine za uchimbaji zinazotumia umeme, jambo linaloonyesha namna teknolojia inavyobadilisha sekta ya usafiri na ujenzi,” amesema.
Mmoja wa watembeleaji wa maonesho hayo, Rehema Mwakalinga amesema maonesho ya mwaka huu yameonyesha mabadiliko makubwa katika ubora wa bidhaa za ndani na kumpa matumaini kuhusu uwezo wa viwanda vya Tanzania.
“Kwa kweli nimevutiwa sana. Bidhaa nyingi nilizoziona zina ubora mkubwa na vifungashio vyake vinaweza kushindana na vya bidhaa kutoka nje ya nchi. Hii inaonyesha kwamba viwanda vyetu vinakua na vina uwezo wa kutengeneza bidhaa bora zaidi,” amesema.