Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yapanda nafasi tatu kwa mazingira bora ya uwekezaji Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Kupanda kwa Tanzania katika viwango vya mazingira bora ya uwekezaji Afrika Mashariki ndani ya miaka miwili kumeendelea kuvutia wawekezaji, huku Mkoa wa Pwani ukiongoza kwa viwanda na kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi.

Mkuranga. Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya 9 kwa nchi za Afrika Mashariki zenye mazingira bora ya uwekezaji ndani ya kipindi cha miaka miwili, hatua inayoendelea kuvutia wawekezaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Akizungumza Machi 17, 2026 wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza magodoro cha FEDERAL INDUSTRY LIMITED wilayani Mkuranga, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema mafanikio hayo yanatokana na jitihada za serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Amesema Mkoa wa Pwani unaongoza kwa kuwa na viwanda vingi nchini, ukiwa na jumla ya viwanda 1,688 vinavyoendelea kuchochea uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Amesema hali hiyo inasaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi, huku mkoa huo ukiwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2026 hadi 2046.

"Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili wazalishe kwa tija, kulipa kodi stahiki na kuongeza ajira kwa Watanzania"amesema

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally amesema uzinduzi wa kiwanda hicho umeifanya Mkuranga kufikia jumla ya viwanda 286.

“Mkuranga tuna mazingira rafiki na ya kutosha kwa uwekezaji wa viwanda, hivyo tunawakaribisha wawekezaji zaidi kuja kuwekeza hapa,” amesema.

Naibu Waziri wa Viwanda, Dennis Londo amesema uzinduzi wa kiwanda hicho unaifanya Tanzania kuwa mshindani mkubwa wa uzalishaji wa bidhaa za viwandani kikanda.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha fursa za kiuchumi na maendeleo.

Kwa upande wake, mmoja wa wamiliki wa kiwanda hicho, Paul Zhang amesema wamevutiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini na kuahidi kuendelea kuwahamasisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza Tanzania.

Amesema wataendelea kuzingatia sheria zote za nchi ikiwemo kulipa kodi kwa wakati na kuheshimu sheria za ajira kwa wafanyakazi wao.

Kiwanda hicho chenye uwekezaji wa dola milioni 20 kinatajwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa Afrika katika uzalishaji wa magodoro na kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 500 kwa wananchi wa eneo hilo.

Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa inayoongoza nchini kwa uwekezaji wa viwanda, ukichangiwa na ukaribu wake na Jiji la Dar es Salaam pamoja na uwepo wa miundombinu ya barabara, bandari na nishati inayorahisisha shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali imeendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda kupitia sera ya uchumi wa viwanda, hali iliyowezesha mkoa huo kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Ukuaji wa viwanda mkoani humo umeendelea kuleta manufaa mbalimbali kwa serikali na jamii kwa ujumla. Kwa upande wa serikali, viwanda vinachangia ongezeko la mapato kupitia kodi na tozo mbalimbali pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.

Kwa upande wa jamii, uwepo wa viwanda umeongeza ajira kwa wananchi, kuinua kipato cha kaya na kuboresha maisha yao, huku pia vikichochea ukuaji wa shughuli nyingine za kiuchumi zikiwemo biashara ndogondogo, usafirishaji na huduma mbalimbali.