Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kodi mpya Kenya yaibua hofu kwa wazalishaji wa marumaru Tanzania

Wafanyakazi wa wakitengeneza bidhaa za malumalu katika hatua mbalimbali za uzalishaji.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Xie, ukokotoaji wa kodi kwa kuzingatia uzito unaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za kuuza bidhaa za Tanzania nchini Kenya, huku mabadiliko ya msingi wa ukadiriaji wa kodi yakiongeza kutokuwa na uhakika kwa wauzaji kuhusu gharama halisi za kuingiza bidhaa nchini humo.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya mfumo wa kodi nchini Kenya yameibua hofu miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa za marumaru nchini Tanzania, huku Serikali ikisema inaendelea na mashauriano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutafuta suluhisho litakalolinda biashara ya kikanda na maslahi ya wazalishaji wa ndani.

Wasiwasi huo umetolewa na Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Co. Ltd, ambayo imeonya kuwa utaratibu mpya wa kodi ya excise duty kwa bidhaa za marumaru na vifaa vya usafi vinavyoingizwa Kenya unaweza kupunguza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania na kudhoofisha biashara ndani ya EAC.

Meneja wa biashara wa kampuni hiyo, Justin Xie, akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Julai 19, 2026, amesema mabadiliko hayo yanaweza kuathiri uwezo wa wazalishaji wa Tanzania kushindana katika soko la Kenya, ambalo ni miongoni mwa masoko muhimu ya bidhaa hizo zinazozalishwa nchini.

“Tunaunga mkono ushirikiano wa kikanda na tunaamini soko la Afrika Mashariki linapaswa kuwa wazi, lenye utabirika na manufaa kwa wazalishaji wote. Wasiwasi wetu ni kwamba hatua hizi zinaweza kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika kujenga biashara ya kikanda,” amesema.

Chini ya mfumo mpya, marumaru zinazoagizwa Kenya zinatozwa kodi ya excise duty ya asilimia tano ya thamani inayotozwa kodi hiyo au Sh50 za Kenya kwa kila kilo, kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa zaidi.

Mfumo huo umechukua nafasi ya utaratibu wa awali uliokuwa ukitumia thamani ya forodha au kipimo cha mita za mraba katika kukokotoa kodi.

Kwa mujibu wa Xie, ukokotoaji wa kodi kwa kuzingatia uzito unaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za kuuza bidhaa za Tanzania nchini Kenya, huku mabadiliko ya msingi wa ukadiriaji wa kodi yakiongeza kutokuwa na uhakika kwa wauzaji kuhusu gharama halisi za kuingiza bidhaa nchini humo.

Wafanyakazi wa wakitengeneza bidhaa za malumalu katika hatua mbalimbali za uzalishaji.

Amesema hali hiyo inaweza kupunguza mauzo ya nje, uzalishaji viwandani, ajira na imani ya wawekezaji, huku athari zikigusa pia wasafirishaji, wasambazaji wa malighafi na watoa huduma wanaotegemea biashara hiyo.

“Hatuombi upendeleo maalumu, bali utekelezaji wa haki wa kanuni za biashara ambazo tayari zimekubaliwa na nchi wanachama wa EAC. Mazingira yenye utabirika ndiyo yanayowezesha uwekezaji, kuongeza uzalishaji na kuunda ajira zaidi,” amesema.

Kampuni hiyo imeitaka Serikali ya Tanzania kuendelea na mazungumzo na Serikali ya Kenya pamoja na taasisi za EAC ili kupata suluhisho la haraka kupitia mifumo ya kikanda iliyopo.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali inaendelea na mazungumzo ndani ya EAC kuhusu changamoto zinazokabili bidhaa za Tanzania zinazoingia katika soko la Kenya.

Amesema suala hilo haliwahusu wazalishaji wa marumaru pekee, bali pia bidhaa nyingine za Tanzania, ikiwemo kioo.

“Ndani ya EAC kuna taratibu zinazolinda biashara kati ya nchi wanachama. Tunaendelea na mazungumzo, lakini wakati huohuo tunachukua hatua za uwiano zinazofanana na walizochukua wao kupitia Muswada wetu wa Sheria ya Fedha ulioanza kutumika mwezi huu,” amesema.

Kapinga amesema Serikali itaendelea kutumia mifumo ya kikanda kutafuta suluhisho litakalohakikisha bidhaa za Tanzania zinaendelea kupata fursa ya kuingia katika masoko ya EAC kwa usawa, huku ikiheshimu makubaliano ya jumuiya hiyo.

Amesisitiza kuwa Tanzania imejikita katika kuimarisha biashara ya kikanda na kulinda viwanda vya ndani kupitia ushirikiano na mazungumzo, akieleza kuwa Serikali inaamini mashauriano yanayoendelea yatazaa suluhisho litakalowanufaisha wafanyabiashara na watumiaji katika ukanda mzima.