Kwanini karibu nusu ya Watanzania ni tegemezi

Watoto wakiomba msaada wa fedha kutoka kwa madereva wa magari katika eneo la Maktaba ya Taifa jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Umewahi kujiuliza Tanzania kuna watu wangapi wapo katika umri wa kufanya kazi au kuzalisha mali na wangapi ambao kwa umri wao wanategemea kuhudumiwa na wengine.

Kwa mujibu wa viwango vya kimataifa ambavyo hutumika hata hapa nchini, umri wa kuzalisha mali ni kati ya miaka 15 hadi 64.

Kuanzia miaka 0 hadi 14 na wale wenye miaka 65 na zaidi wanakuwa katika kundi la wategemezi hata kama baadhi yao wana uwezo wa kuzalisha mali.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa asilimia 53.4 pekee ya Watanzania ndio walio katika umri wa kufanya kazi, mikoa ya Simiyu Tabora na Katavi inaongoza kwa kuwa na utegemezi ukilinganisha na maeneo mengine.

Kwa mujibu ripoti ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa umri na jinsi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha, watu milioni 33 ndio walio katika umri wa kuzalisha, huku wakibeba mzigo wa wategemezi milioni 28.74.

Ripoti hiyo ambayo ni uchambuzi wa matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agosti mwaka 2022 inaeleza kuwa kati ya watu walio na umri wa kuzalisha, wanawake ni asilimia 27.8 huku wanaume ni asilimia 25.6.

Mikoa inayoongoza kwa utegemezi ni Simiyu, Tabora, Katavi, Kigoma, Rukwa, Mara, Geita, Singida, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.

Takwimu zinaeleza kuwa mikoa iliyo na utegemezi mkubwa ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watoto wengi walio chini ya miaka 15 na Simiyu ikiwa kinara.

Idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 mkoani Simiyu ni asilimia 51.3 ya wakazi wote, Katavi inafuata kwa kuwa na asilimia 50, Rukwa asilimia 49.4, Tabora na Geita asilimia 49.2, Kigoma asilimia 48.7.

Aidha, kabla ya sensa ya mwaka 2022, kulikuwa na utafiti wa hali ya nguvu kazi nchini Tanzania uliofanyika mwaka 2021 ambao ulionyesha kuwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini walikuwa milioni 25.9 na kati ya hao, milioni 12.8 ni wanaume na milioni 13.1 ni wanawake.

Machi 13, 2022 Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa kati ya nguvukazi hiyo walio na ajira ni milioni 23.6 sawa na asilimia 91, huku wasio na ajira wakiwa ni milioni 2.3 sawa na asilimia 9.0.

Kwa mujibu wa utafiti huo, nguvukazi isiyo na ajira wanaume ni 725,096 na wanawake ni 1,596,792.

Kufuatia takwimu hizo, wataalamu wa uchumi wameshauri kuwa ni muhimu kudhibiti kasi ya ongezeko la watu ili kupunguza uwiano wa utegemezi ambao huathiri maendeleo ya nchi.

Vilevile wanazuoni hao wanashauri kupanuliwa kwa wigo wa uzalishaji ajira kwa kutoa elimu yenye tija inayowezesha watu kujiajiri baada ya kumaliza chuo, kutoa elimu inayohitajika katika soko la ajira.

Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) anasema kwa utafiti na takwimu zinazoelezwa kuna haja ya nchi kuongeza tija katika uzalishaji wa ajira zilizo na staha na mishahara ya kutosha ili kuwezesha watu kuhudumia walio nyuma yao.

Anasema ni vyema kuhakikisha wanatengenezwa wafanyakazi wenye uwezo wa kulipa kodi na si wazururaji ambao wataongeza utegemezi kwa wengine.

“Katika hili tuangalie namna ya kudhibiti mtoto kuzaa mtoto mwenzie, badala ya yeye kufika umri wa kufanya kazi azalishe mali anaongeza mtoto, mwisho wote wanakuwa tegemezi,” anasema Profesa Semboja.

Anasema pia ni vyema Serikali ihakikishe kundi la vijana walio katika umri wa kuzalisha wanapewa ujuzi stahiki kuendana na kazi zinazozalishwa.

“Tuwatengenezee fursa, waweze kuajirika na kujiajiri, uchumi wetu bado una nafasi ya kuajiri, lakini vijana wafundishwe vile vinavyoendana na dunia ya sasa, ikiwemo teknolojia,” anasema.

Mtaalamu mwingine wa uchumi, Oscar Mkude anasema: “Kuna kila sababu ya kuangalia namna ya kupunguza kasi ya watu kuzaliana ili kuondoa athari zinazoweza kutokea baadaye”.

Anasema ni muhimu kuongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu mbalimbali, ikiwemo afya, elimu iendane na kasi ya ongezeko la watu linalotokea ili kuwe na uwiano sawa, kwa sababu kiwango cha miundombinu iliyopo nchini hutekelezwa kulingana na watu waliopo na makadirio yanayofanyika kwa miaka michache ijayo.

“Serikali inaweza kuamua kurefusha muda wa shule, mfano kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita kuwa lazima, hii inawapa nafasi ya kuchelewa kuzaa na inawafanya kupata elimu ambayo itawasaidia katika soko la ajira na kuwafanya wawe na mchango katika uchumi,” anasema Mkude.

Aidha, Mkude anaongeza kuwa mbali na kuwa na idadi kubwa ya wategemezi kwa umri, vilevile wenye umri wa kuzalisha sio wote wanaozalisha, hivyo kutatua changamoto hiyo sekta binafsi inapaswa kupewa kipaumbele ili kuzalisha ajira nyingi.

“Tungekuwa na mazingira rafiki kwa wawekezaji na mitaji yao kutunzwa isaidie kuzalisha ajira nyingi zaidi ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa,” anasema Mkude.

Mkude anasema fursa za ajira zikiwa nyingi humfanya mtu kuchagua nini anachopenda kufanya, tofauti na kile alichoeleza kuwa sasa vijana wengi wanafanya kile wanachokipata lakini si wanachopenda.

Anasema uzoefu unaonyesha kuwa, baadhi ya watu wanaomaliza vyuo na kukosa ajira wamekuwa wakirudi nyumbani na kuendelea kuwa tegemezi kwa wazazi wao, jambo ambalo linaongeza utegemezi wakiwa katika umri wa kufanya kazi.

“Tuwape vijana elimu yenye ujuzi ndani yake siyo bora elimu, tuondoe ombwe lililopo la wanafunzi kumaliza hawajui kitu,” anasema Mkude na kuongeza kuwa masoko ya nje kwa ajili ya wabobevu katika maeneo fulani yapo wazi, lakini wananchi bado hawajachangamkia fursa hiyo kikamilifu.

Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Joel Silas anasema idadi kubwa ya watu sio jambo baya, lakini ukuaji wa haraka sana wa watu unaleta changamoto, kwani husababisha kuongezeka kwa mahitaji ya chakula, maji, nishati na huduma za kimsingi za kijamii.

Mchumi huyo anasema Tanzania inapaswa kuwekeza katika kuongeza kasi ya kupungua kwa uzazi kupitia uwekezaji katika afya ya uzazi na elimu ya watoto wa kike.

Vilevile anasema ni muhimu kuboresha elimu ya kiwango cha juu kukuza nguvu kazi iliyoelimika vizuri, yenye ujuzi, ubunifu na ushindani.

Dk Silas anasema kuwepo kwa sera za fedha na mageuzi ya kiutawala ni muhimu ili kuboresha matumizi ya ndani, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.

Kadhalika Dk Silas anasema inatakiwa urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ili kuongeza wigo wa ajira ili kusaidia kushughulikia suala hilo.

"Kunatakiwa kuwa na urasimishaji wa wa sekta isiyo rasmi, idadi kubwa ya watu siyo tatizo, lakini ubora wa nguvu kazi, maana wakati mwingine kuwa na idadi kubwa ya vijana kuna faida zake,” anasema.