Ajenda ya MSMEs ni endelevu- Machumu
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu amesema kongamano la wajasiriamali wachanga, wadogo na wa kati (MSMEs) litaendelea kufanyika kwa lengo la kuwanyanyua wafanyabiashara nchini.
Machumu ametoa ahadi hiyo leo Alhamisi Aprili 27, 2023 wakati akifunga kongamano hilo lililowakutanisha wajasiriamali, wadau wa masuala ya fedha na biashara lililofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
“Tutakachokifanya baada ya kongamano hili ni kukusanya maoni yote yaliyojadiliwa hapa, kuna mijadala ambayo ni maswali yaliyoulizwa na mapendekezo yaliyotolewa tutatengeneza ripoti na kuigawa kwa wadau wakiwemo Serikali ili kuona mapendekezo wanayoweza kuyafanyia kazi.
“Kama kampuni tutaendeleza hii ajenda kupitia mitandao yetu ya kijamii, tunaendeleza huu mjadala na nawahamasisha msiishie kwenye kongamano kuna Top 100 tutaendelea kuongea, dhima yetu baada ya hili jukwaa ni ngazi inayotupeleka kwenye mashindano ya Top 100 ninyi mnahusika hapa,” amesema.
Machumu amesema maoni yaliyotolewa katika kongamano hilo yamenukuliwa na kwamba makongamano ya wajasiriamali yatakuwa endelevu.
“Litakua la kwanza lakini halitakuwa la mwisho, tumepewa elimu namna ya kuanzisha biashara tujitahidi kuwa wafumbuzi na namna ya kuzitumia fursa za usafirishaji na tukapewa changamoto ya kuona ni jinsi gani tutazitatua, tunatakiwa kusonga mbele tukaenda mbele kwa kufikiri na kufikiri tusipofikiri wengine watafikiri kwa niaba yetu," amesema Machumu.
Machumu amesema Mwananchi ni chombo cha habari kinachotumia kaulimbiu ya ‘Tunawezesha Taifa’ na kuandaa kongamano hilo ni kuliwezesha Taifa.
"Sasa tunawezesha kwa njia gani? Ni taarifa peke yake, kazi yetu kubwa ni kutumia vyombo vya habari kuleta wadau tofauti kukaa pamoja na kuangalia changamoto ni nini na kutafuta suluhu pamoja, sisi tunafanya nini kujisaidia tulipo na tunasaidiaje nchi yetu," amesema Machumu.
Amesema kongamano hilo ni muhimu kwa wajasiriamali kushiriki majadiliano kama hayo na watunga sera kushiriki katika fursa hizo.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni pamoja na nafasi ya ubunifu na teknolojia katika kukuza mfumo wa biashara na kuongeza faida na miradi inayotolewa ufadhili, (Mahitaji na wigo wake).
Mada nyingine ni kujenga ustahmilivu, (mikakati ya kukabiliana na mtikisiko wa soko kiuchumi) na Mipango ya biashara na programu za kujiendeleza, mbinu bora na rasilimali zinazopatikana kwa biashara za chini, ndogo na za kati (MSEMs).
Kongamono hilo limedhaminiwa na Ashton, benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa mikutano wa Dome.