Matumizi ya gesi kwenye magari ni turufu ya uchumi

Muktasari:

Baadhi ya watumiaji wa magari wameanza kutumia nishati ya gesi asilia kama njia ya kupunguza gharama ya uendeshaji wa vyombo hivyo vinavyotegemea nishati ya petroli.

Dar es Salaam. Mabadiliko kutoka mfumo wa magari yanayotumia petroli kwenda kwenye mfumo wa gesi iliyogandamizwa, maarufu kama CNG ni jambo linaloendelea kushika kasi nchini, baadhi ya watumiaji wa magari wameanza kutumia mfumo huo kama njia ya kupunguza gharama ya uendeshaji wa vyombo hivyo vinavyotegemea nishati ya petroli.

Jambo hili inaweza kuleta athari chanya kiuchumi kwa Taifa na kusaidia kwa kuongeza vyanzo vya nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa nishati itokanayo na mafuta ya petroli au dizeli katika magari, uendeshaji mitambo na mengine. Hata hivyo, inahitaji mipango madhubuti, uwekezaji, na uratibu mzuri.


Jambo la kwanza muhimu, ni kuwekeza katika utafiti na uchimbaji wa gesi asilia ili kuwa na uhakika kuwa soko la mahitaji ya gesi litakapokua, wazalishaji wataweza kumudu mahitaji ya wateja.


Ni jambo litakalokosa tija kubwa kama uhamasishaji wa matumizi ya gesi katika magari kama nishati mbadala utafanyika, ikiwa uwezo wa kulisha mahitaji ni mdogo, bila hivyo inaweza kufaidisha makampuni ya nje ambayo yataona fursa hiyo na kuamua kuitumia.


Sambamba na hilo, ni muhimu kuwekeza katika miundombinu imara ya usambazaji wa gesi hiyo. Kwa mfano, kuwa na mtandao wa vituo vya usambazaji gesi hiyo, lakini pia gesi asilia iliyosafishwa LNG kwa ajili ya matumizi ya majumbani na mengine.


Gesi ni gharama nafuu ukilinganisha na petroli, kuimarisha miundombinu ya usambazaji ikiwemo vituo vya ujazaji mitungi, uwekaji mifumo ya gesi katika magari na mengine itarahisisha upatikanaji. Mtandao huo wa usambazaji ukiwepo utasaidia upatikanaji rahisi wa gesi, jambo hili linaweza kufanyika kwa ushirikiano aidha wa Serikali au sekta binafsi.


Sambamba na hilo, vituo hivyo vya usambazaji pia ndio vitasaidia kutoa huduma za kiufundi kwa kubadilisha magari ya petroli kwa mifumo ya gesi, mahitaji yatakapo kuwa mengi, vituo hivi vitahitajika zaidi kwaajili ya usambazaji na pia kutoa huduma za kiufundi.


Kwa Serikali inaweza kusaidia hilo kwa kuweka sera nzuri za kuwezesha, mfano kutoa nafuu zaidi ya ushuru katika uagizaji wa magari au vifaa vinavyotumia gesi kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo mbadala ambayo pia ni rafiki wa mazingira ukilinganisha na nyinginezo.


Lakini katika hatua ya kuhamasisha Serikali inaweza kuongeza ari ya jambo hilo kwa kiasi kikubwa, kwa mfano kama ikianza na magari yanayomilikiwa na taasisi za umma, kutoka mifumo ya petroli na kusimika mifumo inayotumia gesi, hatua hii inaweza pia kuwa sehemu ya ahueni kwa kupunguza gharama za uendeshaji wa magari jambo litakalosaidia kubana matumizi.


Lakini pia wenye magari na wananchi wa kawaida wanapaswa kupewa elimu kuhusu faida za magari yanayotumia gesi, elimu na uhamasishaji unaweza kufanywa kwa mfano kwa njia ya kampeni, matangazo na njia nyinginezo.


Nafahamu si jambo rahisi kupokewa, hususan na wadau wanaofaidika na biashara ya uagizaji na uuzaji wa mafuta, lakini kiuchumi Taifa lazima kuwa na njia mbadala za kuzalisha nishati ikiwa ni gesi, umeme wa maji, jua, mafuta ya petroli na mengine.


Uwepo wa njia mbadala za nishati unapunguza utegemezi, gharama za uzalishaji na changamoto zinazoweza kuibuka kutokana na kuadimika ghafla kwa nishati fulani.