Profesa Mbarawa ahimiza magari yanayotumia gesi
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ni vyema kununua na kuanza kutumia magari yenye mfumo wa nishati ya gesi kama njia ya kupunguza uharibifu wa mazingira, lakini pia kuendana na teknolojia ya sasa.
Profesa Mbarawa alisema hayo juzi, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kampuni ya usafirishaji ya Scania Tanzania ilipoanzisha ofisi yake nchini, ambapo pia kulifanyika uzinduzi wa magari yanayotumia gesi asilia.
Alisema ni jambo jema kwa wenye uwezo wa kununua magari wanunue ambayo yanatumia nishati hiyo, ili kuungana na dunia kupambana na uharibifu wa mazingira, hasa wa hewa ukaa inayotokana na moshi wa magari yanayotumia mfumo wa mafuta.
"Hii itasaidia kupunguza moshi unaozalishwa na magari yanayotumia mafuta, jambo ambalo limekua chanzo cha magonjwa ya mfumo wa hewa," alisema Mbarawa.
Vilevile alitumia nafasi hiyo kuishukuru kampuni ya Scania kwa mchango mkubwa nchini, ikiwemo ujenzi wa reli ya Tazara, ambapo magari ya Scania 200 yalitumika.
"Kama mnavyojua sekta ya usafirishaji inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi, Scania kama wadau wakubwa wamefanya kazi na sisi kama Serikali tunawashukuru sana," alisema Mbarawa.
Kwa upande wa msimamizi wa maendeleo ya biashara wa kampuni hiyo, Eliavera Timoth alisema kama kampuni wanajivunia kutoa huduma sekta ya usafirishaji, jambo linalochangia kwa namna moja ama nyingi kukuza uchumi.
"Tupo hapa tangu mwaka 1973, tumekuwa na magari ya kila namna na sasa tumeleta magari yenye mfumo wa gesi, watu wakinunua wanapunguza matumizi ya mafuta na anatumia gesi asilia ambayo ni ya hapahapa nchini," alisema Eliavera.
Naye Balozi wa Sweden nchini, Charlotta Macias alisema Serikali ya Sweden itazidi kuongeza ushirikiano wake na Tanzania katika nyanja ya kiuchumi.
"Moja ya malengo ya Serikali ya Sweden ni kutanua wigo wa biashara na uwekezaji nchini Tanzania, unaozingatia urafiki wa mazingira, mfano kama Scania inavyofanya," alisema Macias.