Sh3.05 trilioni na mageuzi ya umeme nchini

Waziri wa Nishati, January Makamba akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 leo Jumatano Mei, 31, 2023 jijini Dodoma.  Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Wizara ya Nishati imeelezea jinsi Sh3.05 trilioni za bajeti ya mwaka 2023/24 zitakavyotumika huku Sh1.5 trilioni kati ya hizo zikipelekwa kukamilisha Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

Pia, Sh2.96 trilioni kati ya fedha hizo ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 97.1 huku matumizi ya kawaida yakitengwa Sh87.92 bilioni sawa na asilimia 2.9 ya bajeti yote.

Wizara hiyo imekuwa na ongezeko la bajeti kutoka Sh2.91 trilioni kwa mwaka 2022/23 hadi Sh3.05 trilioni mwaka 2023/24, huku mkakati mkubwa ikiwa ni kuendeleza mageuzi kwenye sekta hiyo muhimu kwa uzalishaji.

Kutokana na ongezeko hilo, inakuwa wizara ya pili kupatiwa fedha nyingi tangu kuanza kuwasilishwa kwa bajeti za mwaka 2023/24, ya kwanza ikiwa ni ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) iliyopewa Sh9.14 trilioni.

Hata hivyo, bajeti ya Wizara ya Nishati ni kubwa kuliko ile ya Ujenzi na Uchukuzi iliyopewa Sh2.08 trilioni katika mwaka huo wa fedha.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema fedha hizo zinakwenda kutekeleza vipaumbele vikuu vya kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, kuimarisha upatikanaji wa nishati vijijini na vitongoji.

“Vipaumbele vingine ni kuendeleza shughuli za mafuta na gesi nchini na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia,” alisema January.

Pia, alisema mbali na utekelezaji wa miradi unaendelea, wametenga fedha kwa ajili ya miradi iliyopo hatua za utayarishaji ambayo ni njia ya kusafirisha umeme kV 400 Sumbawanga – Mpanda –Kigoma.

Miradi mingine ni njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma. Alisema pia bajeti hiyo itahusuhusu utayarishaji wa miradi ya njia kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya umeme (SGR) loti ya (kipande) tatu hadi ya tano.


Wabunge watema cheche

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula alitaka Serikali kulipa deni la Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) linaloendelea kuongezeka kutoka Sh526 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh720 bilioni.

“Kamati inashauri mwaka huu wa fedha 2023/24 deni hili lote lilipwe,” alisema Kitandula.

Alisema kumekuwa na utaratibu usiofaa wa baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa ankara za umeme hali inayosababisha deni kufikia Sh334.8 bilioni na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ili deni hilo lilipwe.

Kuhusu nishati mbadala, alisema Serikali ione namna ya kupunguza kodi za uingizwaji wa majiko ya umeme yenye presha.

Akichangia katika mjadala huo, mbunge wa viti maalumu, Jesca Kishoa alimuomba Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kuunda tume ya kwenda kuangalia ufanisi wa vitengo vyote vya Wizara ya Nishati vinavyohusika na ukaguzi wa makandarasi wanaopewa kazi kwenye miradi mbalimbali.

Alisema katika baadhi ya miradi ya Rea kunatia kichefuchefu.

“Tulienda Korogwe kukagua miradi ya Rea tukakuta mkandarasi amepewa Sh3.9 bilioni kama malipo ya awali kutekeleza mradi katika vijijini 54 lakini akathibitisha mbele ya Kamati (ya Bunge ya Nishati na Madini) kuwa fedha zile amezipiga kinyume na utaratibu, masharti ya kimkataba,” alisema.

Hata hivyo, alisema hajachukuliwa hatua badala yake Februari 14, mwaka huu amepewa tena mradi kwenye Gridi ya Taifa.

Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu alipongeza hatua zinazochukuliwa na watendaji wa wizara hiyo ya kusambaza umeme vijijini akitolea mfano kwenye jimbo lake ambalo umeme unawaka.

Kuhusu nishati mbadala, Kingu alimpongeza Makamba kufufua mazungomzo kuhusu mradi wa LNG ambako kwa sasa unatarajiwa kuanza kazi muda wowote.

Hata hivyo, aligusia hofu iliyopo miongoni mwa wafanyakazi wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Songas ambayo mkataba wake unakaribia ukingoni akishauri wapewe mkataba mpya.

“Ile ndio PPP (Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi) ya kwanza ambayo imeleta mafanikio kwa Taifa hili. Wanatuuzia umeme kwa bei ya senti sita na nasikia wako tayari kushuka zaidi, fanya nao mazungumzo ili kuondoa taharuki hii. Kama kuna vipengele kwenye mkataba havina maslahi kwa Taifa we vipige chini tutakutetea ,” alisema Kingu.