Mauzo ya hisa DSE yapaa ya hatifungani yakipungua
Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Peter Nalitolela
Dar es Salaam. Soko la mitaji nchini limeonesha kuongezeka kwa mauzo ya hisa na mtaji wa soko katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, ambapo thamani ya hisa imeendelea kuongezeka kwa kasi huku ukuaji wa hati fungani ukipungua.
Kwa mujibu wa takwimu za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), jumla ya thamani ya mtaji soko la hisa ilifikia Sh33.44 trilioni hadi mwisho wa robo hiyo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 39.38 ukilinganisha na robo ya nne ya mwaka 2025 ambapo thamani ilikuwa Sh24.00 trilioni.
Akizungumzia na waandishi wa habari Aprili 28, 2026 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela anasema ukuaji wa hisa umechochewa na ongezeko la shughuli za biashara sokoni pamoja na kuimarika kwa ushiriki wa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
“Tumeshuhudia ongezeko kubwa la miamala ya hisa na kuimarika kwa ukwasi sokoni, jambo ambalo limechangia kupanda kwa thamani ya soko la hisa kwa kasi kubwa,” anasema Nalitolela.
Kuhusu mauzo ya hisa (Total Equity Turnover) anasema yamefikia Sh571.1trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 320.86 ikilinganisha na robo ya nne ya mwaka 2025 iliyokuwa na Sh135.7 trilioni.
Katika upande wa hisa za ndani, Nalitolela anasema mauzo yalifikia Sh553.0 trilioni, kutoka Sh133.2 trilioni robo iliyopita, sawa na ongezeko la asilimia 315.17, huku ukuaji wa mwaka ukifikia asilimia 347.77.
Kwa upande wa hati fungani, anasema jumla ya mauzo yalifikia Sh1.65 trilioni, yakishuka kwa asilimia 4.2 ukilinganisha na robo iliyopita, lakini yakiongezeka kwa asilimia 70.70 ikilinganishwa na Sh966.61 bilioni za mwaka uliopita.
Naye Ofisa Mkuu wa Fedha DSE, Lucas Sinkala anasema kampuni ya soko la mitaji (DSC Group), imeendelea kuonyesha mwenendo mzuri wa kifedha baada ya kurekodi ongezeko la mapato na faida katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.
Anasema DSC Group ilipata mapato ya Sh6.81bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh3.93 bilioni zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana, sawa na ukuaji wa asilimia 7.73.
"Ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa biashara za hatifungani za Serikali, kuongezeka kwa ada mbalimbali, pamoja na kuimarika kwa shughuli za ununuzi na uuzaji wa hisa sokoni," anasema Sinkala.