Mfumo wa gesi katika gari lako utakavyokupunguzia maumivu

Muktasari:

  • Wakati mataifa makubwa na wazalishaji wa nishati duniani yakiwemo gesi na mafuta, wakiendelea kuvutana, Tanzania inaweza kuamua jambo litakalokwenda kupunguza makali ya bei za petrol na dizeli kwa wananchi wake.

Dar es Salaam. Mwaka 2024 umeanza na hamasa kubwa ya matumizi ya nishati ya gesi asilia kwenye magari (CNG) kwa lengo la kupunguza athari za kiuchumi zinazotokana na matumizi ya mafuta.

Matumizi ya petroli na dizeli yamesababisha mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa mbalimbali duniani. Kila nchi ilikuwa na uhaba mkubwa ama bei za mafuta kuwa juu na kuwafanya watumiaji kuanza kufikiria mbinu mbadala kupunguza makali.

Hata hivyo, hamasa na mwamko wa matumizi ya CNG ambayo kitalaamu ni gari kufungwa mtungi wa gesi yenye mgandamizo ili kuunganisha mfumo mwingine wa nishati ya kuendeshea tofauti na mafuta. Kwa hiyo gari huwa na mifumo miwili kwa wakati mmoja.

Hamasa hiyo ya matumizi ya CNG inachagizwa na mwenendo wa bei za soko la Dunia kuathiri bei ya bidhaa kwa muda mrefu katika mataifa mbalimbali ikiwamo Tanzania.  

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), mabadiliko ya bei hizo huamuliwa na kundi la mataifa 12 chini ya Jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji pamoja na gharama za uagizaji wa mafuta.

Hata hivyo wadau wa sekta ya nishati wanasema hakuna sababu ya Tanzania kuendelea kuathirika kiuchumi na kijamii huku ikiwa na utajiri wa nishati ya gesi asilia ulioanza kubadilisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. 

Kwa mujibu wa Ewura, matumizi ya gesi asilia huokoa gharama kwa zaidi ya asilimia 50 ya gharama mtu anazotumia kwenye dizeli na petroli.

Kwa mfano, mtungi wa kilogramu 15 wa CNG hujazwa kwa Sh23,000 na hutembea wastani wa kilometa 250 kwa gari aina ya Toyota IST ambazo zingegharimu wastani wa Sh70,000 kwa mafuta.

Ushahidi ni dereva wa usafiri mtandaoni aina ya IST, Linus Rugemalilra anayedai kuongeza faida kutoka Sh50, 000 hadi zaidi ya Sh100, 000 kwa siku baada ya kuanza kutumia CNG.

Rugemalira, ambaye ameanza kufanya kazi hiyo ya usafirishaji kwa zaidi ya miaka minane sasa jijini Dar es Salaam, anasema kabla ya kuunganisha mfumo wa gesi alikuwa akitumia takribani Sh40,000 kati ya mapato yote Sh100,000 kwa ajili ya petrol kwa makadirio ya kilometa 160 kwa siku lakini maisha yamebadilika.

“Kwa sasa ninatumia kama Sh14, 000 kujaza gesi mtungi wa kilo 11 kila siku pale Ubungo, ninapata mapato ya ziada karibu Sh90, 000 ikilinganishwa na makadirio ya Sh50, 000 niliyopata wakati nikitumia mafuta,” anasema Rugemalira. 

Uchambuzi wa gazeti hili kupitia takwimu za matumizi ya gesi asilia katika malori 256 ya kiwanda cha Saruji cha Dangote, unaonyesha kuokoa zaidi ya Sh10 bilioni ambazo zingetumika katika manunuzi ya mafuta ili kufanikisha usafirishaji wa bidhaa zake tangu Machi hadi Desemba, mwaka jana.

“Nilifunga mtungi kilo 17 kwa Sh2.8milioni Aprili mwaka jana, nikaanza kuingiza faida ya Sh750, 000 kwa mwezi kutoka Sh200, 000, kwanini usitumie?” anasema Juma Thomas.

Uchambuzi wa Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT Wazalendo unaonyesha Serikali inaweza kuokoa takribani Sh500 bilioni endapo magari yote ya Serikali yatatumia mfumo wa CNG huku Mabasi yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (Dart) ukiokoa pia zaidi ya Sh33 bilioni.

“Serikali ipo katika hatua za maandalizi, inakusudia kujenga vituo vya CNG katika Bohari za GPSA itakayowezesha magari ya Serikali kujaza gesi,” anajibu hoja hiyo Mkurugenzi wa Biashara za Mafuta na Gesi wa Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Emmanuel Gilbert huku akikiri manufaa kiuchumi.

Faida kimazingira

Gilbert anasema pamoja na unafuu huo wa gharama kiuchumi, Taifa litakuwa na usalama na uhakika wa nishati hiyo wakati wote katika bei inayotabirika zaidi kuliko ilivyo upande wa mafuta, kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza nje mafuta hayo na kupunguza hewa chafu kwa njia ya mafuta.

Kuhusu uchafuzi wa mazingira, ripoti ya Ewura ya mwaka 2021/22 inaonyesha mahitaji ya dizeli yalikuwa wastani wa lita 5,885,868 kwa siku ikifuatiwa na petroli lita 4,562,297. Mwaka 2021/22 kulikuwa na ongezeko la asilimia mbili kwa dizeli na petroli asilimia 11.

Tishio hilo linaakisi ripoti inayohusisha mabadiliko ya hali ya hewa ya Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC) kwa 2021, ikionyesha nishati ya petrol na dizeli ndio huchangia theluthi moja ya uzalishaji wa kaboni yote duniani.

Athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi katika eneo la ukame husababisha hasara wastani wa Sh1.3 trilioni kila mwaka na Sh65 bilioni kupitia mafuriko kila mwaka kama ilivyoelezwa na Mhandisi wa Viwanda, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Julius Enock. 

Uwezo na mahitaji

Wakati zikielezwa faida hizo kiuchumi, Ripoti ya Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Tanzania 2016-2045 inaonyesha futi za ujazo trilioni 8.8 za gesi zimetengwa kwenye umeme, futi za ujazo bilioni 500 kwenye kaya, futi za ujazo trilioni 3.6 kwenye viwanda na futi za ujazo bilioni 600 kwa magari.

Hata hivyo, wadau wa sekta hiyo wanasema kasi ya mahitaji ya CNG imeonekana kuielemea Serikali katika utoaji wa huduma hiyo ambayo haijatumia hata asilimia moja ya kiasi cha futi bilioni 600. Bei ya gesi kwa sasa ni Sh1, 550 kwa kilo wakati petroli imekuwa kati ya Sh2, 800 hadi 3,400 kwa lita moja. 

“Kilichoonekana hamasa imekuwa kubwa wakati Serikali haijajiandaa vizuri, nashauri iongeze kasi ya miunmbinu sio Dar es Salaam tu hadi mikoani,” anasema John Samwel, ambaye ni dereva usafiri mtandao.

Vituo vinavyotumika kujaza gesi kwenye magari ni kituo mama cha Ubungo kinachohumia zaidi ya magari 800 kwa siku, Tazara chini ya kampuni ya Enric Gas Technology Tanzania Limited kikihudumia magari 300 kwa siku na kituo cha Uwanja wa Ndege kinachohudumia magari 1,200 kwa siku.

Hatua hiyo inachagizwa na ongezeko la kampuni za ufungaji wa mifumo ya gesi kufikia nane ikiwamo Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) iliyofikia wastani wa magari 400 kwa siku ikilinganishwa na magari mawili miaka miwili iliyopita hatua iliyoifanya TPDC kutenga Sh20 bilioni za kuongeza vituo.

“Tunajenga kituo mama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitakachozalishaji kilogramu 70,000 za gesi kwa siku, sawa na magari 6,000 aina ya IST kujaza kila siku zenye ujazo wa mahitaji ya kilogramu 11. Tayari mkataba na mkadarasi umesainiwa, mradi utakamilika kabla ya Juni 2024,” amesema.

Kuhusu hoja ya usambazaji wa CNG kwa njia ya vituo vya mafuta vilivyopo nchini, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Mafuta ya Rejareja Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi anasema wako tayari ila suala hilo linabakia mikononi mwa kampuni husika.