Kituo kipya cha gesi ya magari chazinduliwa Dar

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Doto Biteko amezindua kituo cha kwanza cha kisasa cha kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG) pamoja na karakana ya kufunga mfumo wa gesi hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuchochea nishati safi na salama kwa mazingira.

Dar es Salaam. Gari lako limefungwa mfumo wa nishati ya gesi na unaendelea kusota foleni ya kujaza gesi (CNG)? Kuna habari njema.

 Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Doto Biteko amezindua kituo cha kwanza cha kisasa cha kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG) pamoja na karakana ya kufunga mfumo wa gesi hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuchochea nishati safi na salama kwa mazingira.

Kituo hicho cha ‘Master Gas’ kimezinduliwa leo Novemba 11, 2023 jijini Dar es Salaam, eneo la Pugu barabara ya uwanja wa ndege.

"Tuko kwenye jitihada za kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati nchini, tunakaribisha ufumbuzi kwa nishati endelevu,” amesema Biteko.

Kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia magari 800 kwa siku kwa ujazo wa kilogramu 11,000, sawa na uwezo wa kituo mama cha Ubungo katika huduma ya magari 800.

Hii inamaanisha kwamba, uwepo wa kituo hicho huenda ikapunguza foleni kali katika kituo hicho cha Ubungo na kituo kidogo cha Tazara kinachohudumia wastani wa magari 250 kwa siku.

Kituo hicho chini ya Kampuni ya TAQA Arabia na washirika wenza JCG Oil & Gas, kina pampu sita za kujaza magari kwa wakati mmoja na kila gari litahudumiwa kwa wastani wa dakika tatu.

Kuhusu ufungaji mfumo, kituo hicho kina uwezo wa kufunga magari wastani wa 1,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa TAQA Dalbit, inatarajia kujenga vituo 12 vya CNG jijini Dar es Salaam kwa uwekezaji wa zaidi ya dola 10 milioni siku zijazo ili kukuza matumizi kwa asilimia 50 nchini.

Biteko amesema kampuni hiyo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wapo kwenye majadiliano ili kujenga vituo vidogo vya gesi ya Kusindika (LNG) ili kusambaza mikoani.  

Mkurugenzi Mtendaji wa TAQA Arabia, Pakinam Kafafi, amesema: “Tunafurahi kuleta suluhisho hili la gharama nafuu na kirafiki kwa mazingira, kuimarisha ukuaji wa uchumi, na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.” 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema ni faraja kituo hicho kufunguliwa Ilala ambayo ni kitovu cha Mkoa wa Dar es Salaam wenye wakazi milioni 1.6 ukilinganisha na idadi yote ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao jumla  yao ni milioni 5.3.

Tafiti za huduma hiyo zimeonyesha magari ya CNG husaidia kuondoa kaboni kwa kiwango cha asilimia 25 dhidi ya mafuta pamoja na nafuu wa asilimia 60 ikilinganisha na mafuta.