Machungu ya huduma za magari ya gesi Tanzania

Muktasari:
- Kwa mujibu wa takwimu za kituo hicho, kuhudumia zaidi ya magari 800 kwa siku ikilinganishwa na magari 100 kwa miaka miwili iliyopita huku kituo kidogo cha Tazara chini ya Kampuni ya Enric Gas Technology Tanzania Limited pia kikielemewa pia na uwezo wa kuhudumia wateja kwa siku.
Dar es Salaam. Madereva wa magari yanayotumia mfumo wa gesi wanatumia wastani wa saa nne katika foleni ya kujaza gesi eneo la Kituo mama cha Ubungo (CNG) huku wakiitupia lawama Serikali kwa kuhamasa bila uimarishaji wa miundombinu ya huduma hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za kituo hicho, kuhudumia zaidi ya magari 800 kwa siku ikilinganishwa na magari 100 kwa miaka miwili iliyopita huku kituo kidogo cha Tazara chini ya Kampuni ya Enric Gas Technology Tanzania Limited pia kikielemewa pia na uwezo wa kuhudumia wateja kwa siku.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mradi wa Kampuni ya TAQA Arabia, Eslam Yehia amesema wanatarajia kuanza kutoa huduma kabla ya Novemba 20, mwaka huu katika kituo kipya eneo la Uwanja wa Ndege, kitakachokuwa na uwezo wa kutoa huduma ya gesi kwa magari 1,200 kwa siku.
Hatua hiyo inachagizwa na kasi ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) kufunga wastani wa magari 400 kwa siku ikilinganishwa na magari mawili miaka miwili iliyopita huku vikiibuka vituo vingine zaidi mitaani kwa ajili ya kufunga kwa kwa mikopo yenye riba wastani wa Sh300,000 kwa mtungi.
Wakizungumza na gazeti hili leo Novemba 2, 2023 eneo la kituo hicho, wamemuomba Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko kutembelea maeneo hayo ili kujionea changamoto wanayoipata.
“Tunaomba angalau basi waongeze pampu kwenye hiki kituo ili kuongeza kasi,”ameshauri dereva wa usafiri wa abiria William Mlekwa huku meneja wa kituo hicho John Samwel amedai eneo halitoshi.
Kituo hicho kwa sasa kina pampu mbili zinazotoa huduma ya magari mawili kwa wakati mmoja katika wastani wa dakika tano kwa kila gari, sawa na magari 12 kwa kila saa moja.
Eliah Mkongwe, dereva aliyefika saa 12 asubuhi na kuondoka saa 3:30 asubuhi amesema unafuu wa gharama za gesi unakosa mantiki kutokana na muda mwingi unaopotea kusubiri kituoni hapo.
Dereva mwingne Juma Thomas amedai kusubiri zaidi ya saa sita, huku wengine wakigombana katika foleni kwa kukosa uvumilivu.
“Mimi nilifunga silinda ya kilo 17 kwa Sh2.8 milioni Aprili mwaka huu, nikaanza kuingiza faida ya Sh750,000 kwa mwezi kutoka Sh200,000 lakini kwa foleni hii inakatisha tamaa kama unakuja kukaa kusubiri masaa manne,”amesema dereva mwingine aliyeshuhudia manufaa yake.
Mohamed Mauda amehoji ucheleweshaji wa mradi wa vituo vipya vilivyoahidiwa na Serikali huku Mkurugenzi wa Kampuni ya kufunga mifumo hiyo, Said Masaka akishauri Serikali kuondoa VAT kwa vitendo ili kuwapunguzia mzigo wanaohitaji kufunga gesi.
Maandalizi ya ujenzi
Mkurugenzi wa Biashara za Mafuta na Gesi wa Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Emmanuel Gilbert aliyefanya mahojiano na gazeti hili sikuchache zilizopita alisema maandalizi ya ujenzi wa vituo vipya umeshaanza.
Amesema TPDC itajenga mradi wa wa kituo mama eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vituo vidogo viwili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Kiwanda cha Vifaa vya madawa cha Kairuki kilichopo eneo la Viwanda Zegereni Pwani.
Uchambuzi wa gazeti hili umebaini uwezo wa kuzalishaji kilogramu 70,000 cha CNG katika kituo cha UDSM kwa siku, utawezesha wastani wa magari 6,000 aina ya IST kujaza kila siku zenye ujanzo wa mahitaji ya kilogramu 11.
“Tayari mkataba kati ya TPDC na mkadarasi umesainiwa. Tayari kazi za awali za maandalizi ya ujenzi zinaendelea baada ya mkandarasi kukabidhiwa eneo la mradi. Ujenzi wa mradi unategemewa kukamilika kabla ya Juni mwakani 2024,”alisema.
“Uwekezaji upo katika maeneo mawili.Eneo la kwanza ni kujenga vituo vya CNG. Eneo la pili ni kampuni binafsi kujenga na kuendesha vituo vya CNG. Hadi sasa kampuni binafsi 23 tayari yameruhusiwa kujenga vituo vya CNG. Hii itaongezeko idadi ya vituo na kuondoa kikwazo kwa wananchi,” amesema.
Kuhusu utayari wa kufunga pampu za CNG katika vituo vya mafuta, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Mafuta ya Rejareja Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi amesema suala hilo linabakia mikononi mwa kampuni husika.
“Sisi tuko tayari kufunga CNG lakini unaifunga na magari yako wapi, kibiashara ni suala ambalo tumeliacha kwa wafanyabiashara atakayekuwa tayari,” amesema.