Mfumuko wa bei wabaki asilimia 4.9
Muktasari:
Ongezeko la bidhaa za vyakula na nyingine kumeufanya mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Novemba 2022 kubaki asilimia 4.9 iliyokuwapo Oktoba 2022.
Dar es Salaam. Ongezeko la bidhaa za vyakula na nyingine kumeufanya mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Novemba 2022 kubaki asilimia 4.9 iliyokuwapo Oktoba 2022.
Kiwango cha mfumuko wa bei kubaki kama kilivyokuwa mwezi uliopita huenda ikawa ni ahueni kwa wananchi baada ya kupanda kwa miezi 60 mfululizo. Kiwango cha juu zaidi katika kipindi hicho kilikuwa ni asilimia 5.1 cha Oktoba 2017.
Taarifa iliyotolewa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inazitaja baadhi ya bidhaa zilizopunguza mfumuko wa bei kwa kipindi hicho ni saruji iliyoshuka kutoka asilimia 3.2 hadi 2.5, gesi ya kupikia kutoka asilimia 13.8 hadi 11.8, mafuta ya taa kutoka asilimia 43 hadi asilimia 41.7.
“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Novemba 2022 umeongezeka hadi asilimia 9.5 kutoka 9.1 kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2022. Mfumuko ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Novemba 2022 umepungua hadi asilimia 3.1 kutoka 3.3,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo bei ya baadhi ya bidhaa zilipanda hivyo kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba. Bidhaa hizo ni ngano zilizopanda kutoka asilimia 4.3 hadi 7.2, mchele kutoka asilimia 25.9 hadi 31.2 na, ulezi kutoka asilimia 1.6 asilimia 2.5.
Unga wa mtama uliongezeka kutoka asilimia 3.0 hadi 3.5, samaki wabichi kutoka asilimia 4.3 hadi nane, dagaa wabichi kutoka asilimia 10.5 hadi 20.7, karanga kutoka asilimia nane hadi 8.3, mbogamboga kutoka asilimia 0.6 hadi 0.7.
Maharage yaliongezeka kutoka asilimia 12.2 hadi 16.6, soya kutoka asilimia 9.8 hadi 17.6, kunde kavu kutoka asilimia nne hadi 6.2 na mihogo mikavu kutoka asilimia 15.2 hadi 16.6.