Mgogoro wa Iran, Marekani mlango wa Hormuz wapandisha tena bei mafuta ghafi
Muktasari:
- Pamoja na ongezeko hilo, bei ya mafuta bado iko chini ya kiwango cha juu cha karibu Dola 120 (takribani Sh324,000) kwa pipa kilichowahi kufikiwa wakati wa vita.
Iran. Bei ya mafuta ghafi imetajwa kuongezeka leo Jumanne Julai 14, 2026 baada ya mapigano kuongezeka Mashariki ya Kati, huku masoko ya hisa duniani kupanda kufuatia kushuka mwanzoni mwa biashara.
Kwa mujibu wa tovuti ya AP, Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 2.3 na kufikia Dola 85.18 (takribani Sh230,000) kwa pipa, baada ya kupaa kwa karibu asilimia 10 ikilinganisha na siu ya Jumatatu. Wakati huohuo, mafuta ghafi ya Marekani (WTI) yalipanda kwa asilimia 2.5 na kufikia Dola 80.15 (takribani Sh216,000) kwa pipa.
Hata hivyo, wasiwasi kuhusu uthabiti wa usambazaji wa mafuta umeongezeka baada ya Marekani na Iran kila upande kudai kuwa unadhibiti Mlango wa Hormuz.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Serikali ya UAE pamoja na ripoti za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, mashambulizi yaliyofanyika Mlango wa Hormuz yamesababisha kifo cha mfanyakazi mmoja raia wa India aliyekuwa ndani ya meli ya Mombasa, huku watu wengine wanane wakijeruhiwa, wanne kati yao wakiwa katika hali mbaya.
Meli mbili zilishika moto kabla ya vikosi vya dharura vilivyokuwa ndani ya meli hizo kufanikiwa kuudhibiti.
Mashambulizi hayo yamekuja wakati mvutano wa kijeshi katika Mashariki ya Kati ukiongezeka upya kufuatia kuendelea kwa operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran sambamba na mashambulizi ya Israel, hali iliyowafanya wafanyabiashara wa mafuta duniani kuongeza tahadhari kuhusu usalama wa njia za usafirishaji wa mafuta.
Wachambuzi wa masoko wanaeleza kuwa kuendelea kwa mashambulizi katika Mlango wa Hormuz kunaweza kuongeza gharama za bima za meli, usafirishaji wa mafuta na hatimaye kusukuma bei za mafuta kupanda zaidi katika soko la dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE, meli hizo zilikuwa zikisafiri katika njia ya kusini ya Mlango wa Hormuz ndani ya maji ya Oman zilipolengwa na makombora mawili ya cruise.
Serikali hiyo imelilaani shambulio hilo na kulieleza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na uhuru wa usafiri wa baharini, huku ikisisitiza kuwa inahifadhi haki ya kuchukua hatua zinazofaa kulinda usalama wa taifa, raia wake na maslahi yake ya kimkakati.
Mlango wa Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi za biashara ya mafuta duniani, ukipitisha takribani theluthi moja ya mafuta yanayosafirishwa kwa njia ya bahari kutoka nchi za Ghuba kuelekea Asia, Ulaya na maeneo mengine.
Kutokana na umuhimu huo, shambulio lolote katika eneo hilo huibua hofu ya kuvurugika kwa usambazaji wa mafuta, kupanda kwa gharama za usafirishaji na kuongezeka kwa bei katika soko la kimataifa.
Ripoti za Reuters na vyombo vingine vya habari vya kimataifa zinaonyesha kuwa bei ya mafuta ilianza kupanda baada ya kurejea kwa mashambulizi hayo, huku wafanyabiashara wakihofia kwamba mzozo unaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa zaidi usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz.
Hali hiyo imeanza kufuta matumaini yaliyokuwapo katika wiki za karibuni kwamba mvutano wa Mashariki ya Kati ungepungua na kuruhusu soko la mafuta kurejea katika utulivu.
Macho ya dunia yameelekezwa katika Mlango wa Hormuz, huku serikali mbalimbali, wafanyabiashara wa mafuta na masoko ya fedha yakifuatilia kwa karibu maendeleo ya mzozo huo ambao unaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia iwapo mashambulizi yataendelea au kuongezeka.