Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvutano mpya waibuka Marekani, Iran

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema asilimia 20 inayopendekezwa na Trump kwa meli zinazopita Hormuz ni kubwa.

Tehran/Washington. Mvutano kati ya Iran na Marekani umechukua sura mpya baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, kujibu pendekezo la Rais wa Marekani, Donald Trump la kutoza ada ya asilimia 20 kwa meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X, Araghchi amesema pendekezo hilo ni kubwa, huku akisisitiza kuwa Iran ndiyo imekuwa ikihakikisha usalama wa njia hiyo muhimu ya baharini kwa miaka mingi.

"Rais wa Marekani yuko sahihi kabisa. Yeyote anayehakikisha meli za kibiashara zinapita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz anapaswa kulipwa kwa huduma hiyo," ameandika.

Hata hivyo, amesema kiwango cha asilimia 20 kilichopendekezwa na Trump ni kikubwa kupita kiasi.

"Asilimia 20 bila shaka ni kubwa. Tutatoza ada za bei nafuu," amesema kwa kejeli.

Araghchi pia amesisitiza kuwa Iran itaendelea kulinda Mlango wa Hormuz, akieleza kuwa imekuwa mlinzi wa njia hiyo ya kimkakati kwa muda mrefu.

Kauli hiyo imekuja baada ya Trump kupendekeza meli za mizigo zinazopita katika Mlango wa Hormuz zilipie ada ya asilimia 20, akieleza kuwa Marekani imekuwa ikibeba gharama kubwa za kulinda usalama wa eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Trump amesema mataifa ya Ghuba ya Uajemi yanapaswa kuchangia gharama za ulinzi unaotolewa na Marekani dhidi ya vitisho vinavyotokana na Iran.

"Nataka tulipwe kwa sababu tunalinda sehemu tajiri sana ya dunia. Tunatumia fedha nyingi, hivyo nchi tunazozilinda zinapaswa kutulipa kwa ulinzi huo," amesema.

Aliyataja mataifa ya Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Qatar, Bahrain na Kuwait kuwa miongoni mwa nchi zinazofaidika na ulinzi huo wa Marekani.

Trump pia amedai Iran ilikaribia kutengeneza silaha za nyuklia kabla ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu yake, akisisitiza kuwa Washington itaendelea kuchukua hatua za kijeshi endapo itaona kuna ulazima.

Aidha, amedai Iran ilirusha makombora kuelekea baadhi ya mataifa ya Ghuba na kuitaja Tehran kuwa tishio kwa usalama wa eneo hilo.

Katika kauli nyingine, Trump amesema Marekani ilikuwa imepanga kufanya shambulio jingine kubwa dhidi ya Iran, huku akidai viongozi wa Tehran sasa wanataka kufikia makubaliano baada ya miaka mingi ya mazungumzo.

Kwa upande wake, Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani na imekuwa ikipinga mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu yake.

Mlango wa Bahari wa Hormuz ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta ghafi na gesi asilia duniani, hivyo mabadiliko yoyote ya usalama au tozo katika eneo hilo yanaweza kuwa na athari kwa biashara na masoko ya nishati duniani.

Hadi sasa, Marekani haijatoa tamko rasmi kujibu kauli za Araghchi, huku mabadilishano hayo yakiongeza wasiwasi kuhusu kuendelea kwa mvutano kati ya Washington na Tehran katika eneo la Ghuba ya Uajemi.