Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyanzaga inavyochochea uchumi kabla uzalishaji wa dhahabu

Kamishina wa Madini, Dk Abdulrahman Mwanga (katikati) akitoa cheti cha ushiriki katika Jukwaa la tano la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini(LCCF 2026) kwa ofisa kutoka mgodi wa Sotta Minning, Dk Richard Ojendo wakati wa kufunga jukwaa hilo hivi karibuni jijini Mwanza.

Muktasari:

  • Kongamano la Tano la Uzingatiaji wa Maudhui ya Ndani (Local Content Compliance Forum – LCCF 2026) lililofanyika jijini Mwanza liliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo na kujadili mchango wa sekta kwa wananchi.

Mwanza. Mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga unaotekelezwa na Kampuni ya Sotta Mining Corporation Limited umesema uwekezaji mkubwa unaofanyika ndani ya mradi huo na maeneo ya karibu utaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi hata kabla ya kuanza uzalishaji wa kibiashara.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa tayari mradi huo uliopo wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, umechangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia ajira, ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wazawa, ulipaji wa kodi na uwekezaji katika maendeleo ya jamii.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja wa Sotta Mining nchini, Isaac Lupokela, baada ya kumalizika kwa Kongamano la Tano la Uzingatiaji wa Maudhui ya Ndani (Local Content Compliance Forum – LCCF 2026) lililofanyika jijini Mwanza.

Amesema ushiriki wa kampuni katika kongamano hilo unaakisi dhamira ya kuendesha shughuli kwa uwazi, kuimarisha utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani na kujenga ushirikiano wa karibu na Serikali, jamii zinazozunguka mradi, pamoja na wafanyabiashara wa Kitanzania.

Amesema kati ya Julai 2024 na Machi 2026, mradi huo umeingiza Sh457.7 bilioni katika uchumi wa Tanzania. Fedha hizo zimetokana na ununuzi wa bidhaa na huduma, malipo kwa Serikali, mishahara ya wafanyakazi, pamoja na uwekezaji unaofanyika katika jamii zinazozunguka mradi.

Kwa mujibu wa Lupokela, kati ya kiasi hicho, Sh371.6 bilioni zimetumika kununua bidhaa na huduma kutoka kwa wasambazaji wa Kitanzania.

Hatua hiyo, amesema, imeongeza fursa kwa wafanyabiashara wa ndani kushiriki kikamilifu katika shughuli za sekta ya madini, huku ikijenga uwezo wa biashara za wazawa kukua na kushindana katika miradi mikubwa ya kimataifa.

Amesema sera ya kampuni ni kuwapa kipaumbele wazabuni na wasambazaji wa ndani pale inapowezekana, kwa kuwa hatua hiyo huchochea ajira, huongeza mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi na kuimarisha uwezo wa kampuni za Kitanzania kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Lupokela amesema kwa sasa, zaidi ya watu 3,600 wanafanya kazi katika eneo la Mradi wa Nyanzaga. Kati ya hao, wafanyakazi 281 wameajiriwa moja kwa moja na Sotta Mining Corporation Limited, huku wengi wao wakiwa Watanzania wanaotoka katika maeneo yanayouzunguka mradi huo.

Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa mgodi huo umefikia takribani asilimia 50, huku zaidi ya Dola za Marekani milioni 250 (sawa na Sh675 bilioni) zikiwa tayari zimewekezwa katika utekelezaji wa mradi.

Amesema uzalishaji wa kibiashara wa dhahabu unatarajiwa kuanza katika robo ya kwanza ya mwaka 2027.

Pia, utaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayotambua sekta ya madini kuwa moja ya nguzo muhimu za mageuzi ya uchumi wa Tanzania.

Lupokela amesema Sotta Mining itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali, jamii zinazozunguka mradi na wadau wengine wa sekta ya madini ili kuhakikisha uwekezaji huo unaendelea kuleta manufaa ya muda mrefu kwa Watanzania.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akifungua kongamano hilo, alisema Watanzania sasa wameongeza ushiriki wao katika sekta ya madini, wakishika nafasi mbalimbali za ajira, uongozi na utoaji wa bidhaa na huduma.

"Kilikuwa kilio cha Watanzania kwamba wanakosa fursa za kusambaza bidhaa na huduma migodini. Kulikuwa na wakati hata kuku na mayai vilikuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi, jambo lililoonyesha Watanzania hawakushiriki kikamilifu katika uchumi wa sekta ya madini," alisema Mavunde.