Rais Mwinyi awaangukia wafanyabiashara kushusha bei vyakula

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameeleza kuguswa kwake na bei ya awali ya mchele na kueleza hata kama isifikie ilikotoka kutokanana sababu mbalimbali za mabadiliko ya kiuchumi lakini isiwe kwa bei ya Sh3,000 ambayo ni kubwa zaidi.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewasihi wafanyabiashara nchini kupunguza bei za bidhaa hasusani vyakula ili kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa kipato cha chini.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Januari 31, 2023 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na wafanyabiashara mbalimbali na kujadili kupanda kwa bei ya chakula nchini.
Amesema bidhaa za vyakula ikiwemo mchele zimepanda maradufu hali, iliyozusha taharuki na kuongeza ugumu wa maisha.
Amesema haijawahi kutokea mchele kupanda bei kiasi kikubwa kama ilivyo sasa na kuongeza kuwa ni bidhaa yenye uhitaji mkubwa kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa sasa kilo moja ya mchele ni Sh3,400 ambapo bei iliyozoeleka ilikuwa Sh2,700.
“Zanzibar mchele ndio kila kitu, ni sawa na wenzetu Uarabuni ukiadimika unga, kukosekana mkate kunakuwa na vurugu mitaani, hapa Zanzibar watu wetu ni wakarimu, lakini sasa hivi wamefikishwa pabaya sana, kilo moja zaidi ya Sh3,000, haijawahi kutokea, tujitahidi Ramadhani inakuja na hili ni ombi langu kwenu,” amesema.


“Tukubaliane ndugu zangu wafanyabiashara hali ya ndani sio nzuri, mchele huu huu miaka miwili iliyopita sisi tunaingia madarakani ilikua kilo Sh1,700, leo tunakaribia mara mbili ya bei, inaumiza watu,” amesema Rais Mwinyi.
Ameeleza kuguswa kwake na bei ya awali ya mchele na kueleza hata kama isifikie ilikotoka kutokanana sababu mbalimbali za mabadiliko ya kiuchumi lakini isiwe kwa bei ya Sh3000 ambayo ni kubwa zaidi.
Aliwashauri wafanyabiashara hao kushirikiana kuchukua meli kubwa zitakazobeba zaidi ya tani 30,000 badala ya kuchukua meli ndogo za tani 5,000.
 kwa nia ya kuwasaidia watu kuondokana na ugumu wa Maisha uliopo, ilizingitiwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unakaribia.
Aliwaeleza wafanyabiashara hao kuchukua meli kubwa kutapunguza utitiri wa meli ndogo zenye kubeba tani kidogo, hali aliyoieleza kwamba inaongeza msongamano bandarini.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wameeleza changamoto kubwa iliyosababisha bidhaa kupanda bei kuwa ni mkwamo wa utoaji mizigo bandarini pamoja na gharama kubwa za mizigo zinazotozwa.
Pia, wameiomba serikali likiwemo Shirika la Bandari kufanya juhudi za ziada kupunguza mkwamo wa utoaji mizigo na kutoa kipaumbele kwa bidhaa zenye mahitaji ya haraka kwa wananchi.
Mfanyabiashara Bopar Interprize amesema: “wananchi hawaelewi nini kinaendelea lakini ukweli hasa bandari yetu imezidiwa sasa mahitaji yameongezeka, lazima zitumike njia mbadala za kuwahisha mizigo, siku 30 nyingi sana mzigo kukaa bandarini.”