Sababu Wafanyabiashara kukimbia masoko mapya

Mwonekano wa soko la Bwawani lililopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam ambapo wafanyabiashara wameondoka kwa madai ya soko hilo halikidhi mahitaji yao. Picha na Elias Msuya

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka za Mkoa wa Dar es Salaam zikipambana kuwaondoa wafanyabiashara ndogo katika maeneo yasiyoruhusiwa, yapo masoko mapya yaliyojengwa kwa nyakati tofauti, lakini hayatumiki.

Masoko hayo yaliyojengwa kwa mabilioni ya fedha, yameshindwa kukidhi matakwa ya wafanyabiashara wa maeneo husika ikiwa pamoja na ufungaji wa mita za umeme wa pamoja, kuwekwa kwa tozo kubwa na kukosekana kwa mikakati ya kuvutia wateja.

Kukosekana kwa wafanyabiashara katika masoko hayo, kunatajwa kuwa kumesababishwa na wafanyabiashara kutoshirikishwa kabla ya ujenzi na au kujengwa maeneno ambayo si rafiki kwao.

Hayo yamebainika hivi karibuni wakati wa kukagua miradi inayotekelezwa na Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Katika Manispaa ya Temeke mradi huo umewezesha kujengwa kwa masoko manne kikiwemo kituo cha biashara cha Kijichi ambako pia imewekwa stendi ya mabasi ya kuelekea mikoa ya kusini.

Hata hivyo, mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh3.9 bilioni ukijumuisha soko, mall na stendi, umekimbiwa na wafanyabiashara.

Biashara katika kituo hicho inasuasua kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuondoka huku wamiliki wa mabasi nao wakikikwepa kukitumia licha ya kuagizwa wakitumie.

Akizungumza na Mwananchi katika stendi hiyo, Meneja wa stendi hiyo Rose Emmanueli alisema, baada ya uzinduzi wa stendi hiyo, uwezekano wa mabasi yaliyokuwa yanaingia na kutoka hayakupungua 80 kwa siku lakini hivi sasa hayazidi 30.

“Baada ya kuzindua daladala zilizokuwa zinafika kituoni hapa zilikuwa ni kati ya 200 na 250 lakini ilipofika Desemba idadi ilipungua ambapo hadi sasa mabasi yanayoingia hayazidi 30,” alisema.

“Wamiliki wa magari hayo wanadai hakuna abiria na sababu nyingine wanasema kituo hiki kiko mbali,” alisema Rose.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa mabasi yaendayo Kusini na mmiliki wa mabasi ya Baraka, Oliver Baraka alisema hawapati abiria katika stendi hiyo.

“Hata abiria wenyewe wa kusini hawataki kwenda Kijichi, tunaishauri Serikali watafute stendi nyingine itakayokuwa karibu na mazingira yawe rafiki,” alisema Baraka.

Akieleza sababu ya kusuasua kwa stendi ya mabasi ya mikoani tangu ilipoanzishwa Oktoba 17, 2022, Ofisa Masoko, Manispaa ya Temeke, Anzameni Mandari alisema ni kutokana na utaratibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu (Latra).

“Kwa utaratibu wa Latra, mabasi yanayokwenda nje ya mkoa yanaweza kusimama eneo moja, kwa hiyo kama yanasimama stendi ya Magufuli, hayalazimiki kuingia kwenye stendi hii kama abiria hawapo.

“Awali ilitarajiwa kuwa stendi ya daladala, lakini ikaongezewa matumizi ya kuwa stendi ya mabasi yaendayo mikoani yanayopita Temeke, baada ya kuwa na msongamano eneo la Mbagala Rangitatu,” alisema.

Hata hivyo, alisema wanaendelea kufanya maboresho kwenye eneo hilo, ikiwemo kujenga kwa zege.

“Pia kutakuwa na huduma mbalimbali, kama utoaji wa Vitambulisho vya uraia (Nida), ofisi za kodi (TRA) na huduma nyinginezo, kwa hiyo tunatarajia kitakuwa kituo kikubwa ukanda huu,” alisema.

Mbali na kituo hicho, soko la Mbagala Kuu mtaa wa Shimbwe nalo limefungwa kwa kukosa wafanyabiashara.

Juma Hassan aliyekuwa akifanya biashara eneo hilo, alisema awali eneo hilo kulikuwa na soko lisilo rasmi, lakini soko lilipojengwa wafanyabiashara hao walihama.

“Wafanyabiashara wamehamia Barabara ya Ng’ombe kwa sababu hapa hakuna biashara. Ilitakiwa wapitishe angalau daladala hapa ili wateja waje.

“Kule Barabara ya ng’ombe ni eneo la mtu binafsi, lakini kuna daladala zinapita, kuna biashara,” alisema.

Wakati masoko hayo yakikimbiwa na wafanyabiashara, Manispaa ya Temeke inaendelea na ujenzi wa soko la Mbagala Zakhiem litakalogharimu Sh2.48 bilioni litakalokuwa na maduka 150 na vizimba 136 na jengo dogo litakalochukua wauza kuku.

Awali, soko hilo lilikuwa na wafanyabiashara, ila wamehamishwa kwa muda kupisha ujenzi huo.

Soko jingine ni la Mtoni Mtongani lenye wafanyabiashara 228.


Wakimbia soko la Bwawani Kinondoni

Zaidi ya wafanyabiashara 150 waliokuwa wamechukua vizimba na maduka katika soko la Bwawani lililopo Mwananyamala Dar es Salaam wameondoka kwa madai ya soko hilo jipya kutokidhi matakwa yao.

Soko hilo limegharimu zaidi ya Sh1.2 bilioni ikiwa ni sehemu ya zaidi ya Sh215.9 bilioni zimetumika kujenga miradi ya Kuendeleza jiji la Dar es Salaam (DMDP) kwa manispaa ya Kinondoni.

Wakizungumza sokoni hapo, baadhi ya wafanyabiashara wachache waliobaki, walisema licha ya mwonekano mzuri wa soko, matakwa yao hayakutekelezwa.

“Changamoto ni kwamba wateja hakuna ndiyo maana wenzetu waliamua kuondoka na kutafuta maeneo mengine,” alisema Elizabeth Felix anayeuza asali sokoni hapo.

“Mimi nipo hapa tu kwa sababu sijapata pa kwenda,” aliongeza.

Alisema soko hilo lilipofunguliwa Juni 2021 wafanyabiashara walikuwa wengi na walijaa vizimba vyote, lakini ghafla wakaanza kupungua.

“Kwa kuwa hakuna wateja mtu ana familia atafanya nini? Ndiyo maana watu karibu wote wameondoka,” alisema.

Alitaja sababu nyingine iliyowaondoa wafanyabiashara hao kuwa ni mfumo wa umeme uliofungwa mita moja kwa wafanyabiashara wote.

“Tuliomba watufanyie mpango wa kutuletea ruti za daladala kuwe na watu wengi na watuletee biashara za jumla kama Mabibo, wanashusha ndizi matunda na viazi, itasaidia watu wa Mwananyamala, Kijitonyama watakuja, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema.

Naye mfanyabiashara Mariam Juma aliunga mkono kauli hiyo akisema licha ya biashara kuwa ngumu, Manispaa ya Kinondoni ilianza kuwatoza ushuru mara baada ya kupewa vizimba.

“Tuliomba asitutoze ushuru ili kwanza tujiimarishe kibiashara, lakini walianza kututoza ushuru tangu siku ya kwanza, hadi sasa hakuna tunachofanya, biashara zimekufa,” alisema.

Akizungumzia kero za wafanyabiashara, Meneja soko hilo, Damali Jonathan alisema Manispaa ya Kinondoni inazijua kero hizo na inazifanyia kazi,

“Soko letu lina mwonekano mzuri na linavutia, lakini changamoto ni watu kuchukua vizimba na kushindwa kufanya biashara, hivyo tunawaomba waliochukua vizimba na frame wafungue biashara zao waendelee,” alisema.

Kuhusu kero ya umeme, alisema amepata malalamiko ya wafanyabiashara na wanayafanyia kazi.

“Hilo jambo ni kweli lipo, lakini chini ya usimamizi ya soko tunafanya mabadiliko ili kila mfanyabiashara atumie umeme uliopo. Ni vitu ambavyo viko ndani ya usimamizi wa soko tutaifanyia kazi, haitachukua muda mrefu,” alisema.

Kuhusu kuwekwa kwa biashara itakavyovutia watu wengi kuja soko hilo, alisema wanalifanyia kazi kwa kuwaomba wafanyabiashara wa jumla.


Malalamiko soko la Bombom

Katika Manispaa ya Ilala (Halmshauri ya Jiji) iliyopewa zaidi ya Sh120.7 bilioni (DMDP), miongoni mwa masoko yaliyoboreshwa ni soko la Bombom lililopo Kiwalani.

Licha ya maboresho hayo, wafanyabiashara hawana raha, wakisema maboresho kwanza hayajakamilika na pia yameathiri biashara zao.

Veronica Kahesya mwenye duka eneo hilo, alisema kwanza wamewekewa tozo kubwa ya Sh45, 000 kwa mwezi.

“Tozo ni kubwa mno, watu hatuna hela halafu tumekuja kufungwa hapa. Tumeshawasilisha malalamiko yetu kwa viongozi husika lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Ndiyo maana unaona maduka haya yote yamefungwa kwa sababu wameshindwa kulipa hiyo kodi,” alisema.

Kuhusu umeme, alisema soko hilo limefungiwa mita moja, hali inayowaletea shida kwenye matumizi na malipo.

“Kabla ya soko hili mimi nilikuwa nimeunganishiwa umeme kwenye duka langu, lakini walipojenga Tanesco walichukua mita yangu.

“Nimeshapeleka malalamiko kwa Mkurugenzi wa Manispaa, lakini nimeambiwa Tanesco watakuja kuweka, huu ni mwezi wa tatu. Ukiangalia maduka mengi hapa yamefungwa kwa sababu ya shida ya umeme,” alisema.

Kwa upande wake, Masoud Mohamed anayeuza samaki katika soko hilo alisema baada ya ujenzi huo kumekuwa na maji yanayotuama na kuwa kero kwenye biashara zao.

“Tumeshaeleza uongozi wa soko, lakini hatuoni utekelezaji wowote.

“Tuna kero ya ushuru wa soko, tumeomba tuwe tunalipa kwa siku, siyo kwa mwezi,” alisema.

Naye Theresia Maro alisema,“kwa ujumla biashara ni mbaya tofauti na mwanzo, wateja hatupati, sisi wenyewe tunashangaa.

“Biashara inakwenda tofauti na mwanzo, tunashindwa kulipa hata kodi, tunaomba watupunguzie kodi iwe Sh500 na wachukue kila siku kwa sababu mauzo ni mabovu,” alisema.

Mkuu wa masoko ya mradi wa DMDP kwa Manispaa ya Temeke anayesimamia masoko ya Bombom, Kigilagila na Minazi mirefu, Titus Telesphori alisema changamoto hizo wameshazisikia.

“Kwa mfano kuna baadhi ya maeneo mvua ikinyesha maji yanatuama, walishakuja wataalamu wakafanya tathmini wakashughulikia na changamoto nyingine zinashughulikiwa kulingana na bajeti,” alisema.

Kuhusu ushuru, alisema wanatoza kutokana na sheria za masoko zinavyoelekeza.

“Kwa mfano samaki na kuku wanapaswa kulipa Sh500 kwa siku, watu wa fremu wanalipa Sh1,500 kwa siku (Sh45,000 kwa mwezi), kwa babalishe na mamalishe Sh1,000 kwa siku (Sh30,000 kwa mwezi),” alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu soko hilo, alisema kuna kitengo cha samaki na kuku chenye watu 26, vizimba 136 vya matunda na mboga mboga, kuna maduka 64 na kuna mama na baba lishe wawili.

“Hili soko hali ilivyokuwa mwanzo ni tofauti na sasa, awali biashara ilikuwa inafanyika kwa shida, wakifanyia juani na mvua, lakini sasa majengo yameboreshwa.

“Halmashauri imefanikiwa kukusanya Sh10 milioni kwa mwaka wa fedha kuanzia Julai 2022 hadi Januari na tunatarajia kuongeza hadi Sh17 milioni hadi mwaka ukiisha,” alisema.


Soko la Machinga Complex

Yanayojitokeza kwa masoko hayo ya DMDP ni sawia na Soko la Machinga Complex lililobuniwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuwaweka mahali pamoja wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya 10,000 walio zagaa katika mitaa na kuweka usafi katika jiji hilo.

Halmashauri ya Jiji hilo liliingia makubaliano na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mwaka 2007 lililotoa fedha na kusimamia ujenzi wa jengo la mradi wa biashara wa Jiji (Machinga Complex)

Jengo la mradi wa biashara wa Jiji (Machinga Complex) linapatikana Mtaa wa Lindi, katika Manispaa ya Ilala lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 4,206.

Lengo kubwa la mradi huu ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao kwenye eneo rasmi na kuweza kukuza uchumi binafsi hatimaye waweze kukuza uchumi wa Taifa.

Vijana takribani 300 kutoka vyuo mbalimbali vya taasisi za ufundi wamejiajiri ndani ya jengo la biashara la Machinga Complex.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inawasisitiza wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao rasmi kwenye jengo hili na kuondoka katika mitaa ya Dar es Salaam kwani jengo hili limejengwa kwa ajili yao.

Hata hivyo, kinyume na matarajio, baada ya soko hilo kukamilika, wafanyabiashara waliotarajiwa kuingia wakiwamo wa soko la Mchikichini, waligoma wakidai kuwa hawapati wateja na hivyo kurudi kwenye masoko holela.

Mbali na changamoto hiyo, kumekuwa na utata wa deni la NSSF iliyotoa fedha za ujenzi.

Wakati uongozi wa Jiji la Dar es Salam ukisema ulikabidhiwa soko hilo deni likiwa limefikia Sh12 bilioni kutoka Sh9 bilioni zilizokuwa kwenye makubaliano ya awali, NSSF inasema fedha zilizotumika kulikopesha Jiji katika ujenzi huo kati ya mwaka 2007 na 2012 zilikuwa Sh15.9 bilioni na riba ni asilimia 14.44 kwa mwaka.

Aidha, NSSF imedai kuwa Jiji la Dar es Salaam limesharejesha Sh80 milioni kwenye sehemu ya deni wanalodaiwa na majadiliano yanaendelea ya mfuko huo, Jiji na Serikali.


Soko la Job Ndugai

Miongoni mwa masoko makubwa yaliyojengwa nchini ni soko la Job Ndugai lililopo jijini Dodoma.

Akiweka jiwe la msingi wakati wa ujenzi wa soko hilo, aliyekuwa Rais, John Magufuli alisema soko hilo lingetarajiwa kutumiwa na wakazi wa Dodoma na mikoa mingine.

Hata hivyo, kinyume na matarajio, miaka miwili baada ya kuzinduliwa, wafanyabiashara wamelisusa soko hilo.

Wakizungumza na Mwananchi mwaka jana, baadhi ya wafanyabiashara wa ndizi na viazi katika soko la Majengo walilalamika kulazimishwa na uongozi wa jiji hilo kushushia bidhaa zao kwenye soko la Job Ndugai.

Walisema kusafirisha bidhaa hizo huwapa hasara, kwani hupoteza fedha nyingi kufikisha kwenye masoko ya mjini.

Alisema bei ya kusafirisha viazi kutoka Mbeya hadi Dodoma, kisha kushusha soko la Majengo huwa tofauti ukilinganisha na kushusha bidhaa hiyo kwenye soko la Job Ndugai.

Kutokana na hali ya baadhi ya wafanyabiashara hao kusitisha na kushusha bidhaa hizo kwenye soko la Job Ndugai, bei ya bidhaa za vyakula zilipanda na kusababisha usumbufu kwa wananchi.