Serikali kuwanyima leseni wanunuzi mazao wasiowalipa wakulima
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo akizungumza jana Jumamosi Juni 6, 2026 wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya kahawa uliofanyika jijini Dodoma.
Muktasari:
- Serikali imeagiza wanunuzi wote wenye madeni kwa wakulima wa kahawa na mazao mengine kutoruhusiwa kushiriki ununuzi wa mazao msimu ujao.
Dodoma. Serikali imeziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa na wilaya kuhakikisha wanunuzi wote wenye madeni kwa wakulima wa kahawa na mazao mengine hawaruhusiwi kushiriki katika ununuzi wa mazao msimu ujao, hatua inayolenga kulinda maslahi ya wakulima na kuondoa migogoro ya malipo katika sekta hiyo.
Akizungumza leo Jumamosi Juni 6, 2026 katika mkutano wa wadau wa sekta ya kahawa uliofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema Serikali haitatoa leseni kwa mnunuzi yeyote ambaye hajalipa madeni ya wakulima.
Amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) zinapaswa kuchukua hatua dhidi ya watu binafsi au vyama vinavyosababisha migogoro ya malipo kwa wakulima ili kuimarisha uwazi na uaminifu katika biashara ya kahawa.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 16 wa tasnia ya kahawa wakiwa katika mkutano huo wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) unaofanyika jijini Dodoma leo, Juni 6, 2026.
Chongolo amesema Serikali imepokea taarifa za mafanikio katika kudhibiti utoroshwaji wa mazao kutoka Wilaya za Misenyi na Kyerwa na kuwapongeza viongozi wa maeneo hayo kwa usimamizi mzuri wa mazao ya wakulima.
Amesema kahawa imeendelea kuwa moja ya mazao muhimu ya biashara nchini, ikiiingizia Tanzania zaidi ya Dola za Marekani 400 milioni ambayo ni takribani Sh1.024 trilioni mwaka uliopita na kuwa zao la pili kwa kuingiza fedha za kigeni baada ya tumbaku.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mahitaji ya kahawa katika soko la dunia yanaendelea kuongezeka huku Tanzania ikiendelea kujijengea sifa ya kuzalisha kahawa bora yenye ushindani mkubwa kimataifa.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji sambamba na ubora wa kahawa, matumizi ya miche bora, kuimarisha huduma za ugani na uwekezaji katika uchakataji wa kahawa ili kuongeza thamani kabla ya kuuzwa.
“Hatutaki kuona ofisa ugani akiwa nyuma ya mkulima katika maarifa. Tunahitaji wataalamu wenye uwezo wa kuwasaidia wakulima kutumia teknolojia na mbinu bora za kisasa,” amesema.
Katika hatua nyingine, TCB kwa kushirikiana na PASS Trust wamezindua Mpango wa Dhamana ya Mikopo ya Mbolea kwa Wakulima wa Kahawa (FCGS), unaolenga kurahisisha upatikanaji wa pembejeo na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa PASS Trust, Adam Kamanda amesema taasisi hizo zimewekeza jumla ya Sh12 bilioni katika mpango huo ambapo TCB imechangia Sh6 bilioni na PASS Trust kiasi kama hicho.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 16 wa tasnia ya kahawa wakiwa katika mkutano huo wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) unaofanyika jijini Dodoma leo, Juni 6, 2026.
Amesema fedha hizo zitatumika kama dhamana ya mikopo kwa wakulima na zinatarajiwa kuwezesha utoaji wa mikopo ya mbolea yenye thamani ya zaidi ya Sh75 bilioni kila mwaka.
“Mpango huu unalenga kuondoa vikwazo vinavyowakabili wakulima katika kupata pembejeo kwa wakati na kuongeza tija katika uzalishaji wa kahawa,” amesema Kamanda.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCB, Profesa Aurelia Kamuzora amesema wadau wa sekta hiyo wamejadili masuala mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa masoko, uzalishaji wa miche bora, ushiriki wa vijana na wanawake pamoja na ufuatiliaji wa zao la kahawa.
Amesema Tanzania inalenga kufikia uzalishaji wa tani 300,000 za kahawa kwa mwaka kutoka tani 86,000 za sasa kupitia maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta hiyo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Khalid Nsekela amesema mafanikio ya sekta ya kahawa hayapaswi kupimwa kwa ongezeko la uzalishaji pekee bali kwa namna yanavyoboresha maisha ya wakulima na kuongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania katika soko la dunia.