Serikali yashtuka mbolea ya ruzuku kuuzwa nchi ya Malawi

Mkuu wa wilaya ya Ileje Farida Mgomi akizungumza na mwananchi Leo Agosti 12,2024 walivyojipanga kuzuia utoroshaji wa mbolea za ruzuku unaofanya na bodaboda. Picha na Denis Sinkonde
Muktasari:
- Madereva wa bodaboda wamedaiwa kujigeuza wasafirishaji wa mbolea hiyo kwenda nchi ya Malawi.
Songwe. Serikali imesema inaanza operesheni ya kuwakamata watu wanaodaiwa kutorosha mbolea ya ruzuku na kwenda kuiuza nchi jirani ya Malawi huku ikitoa onyo kwa madereva pikipiki wanaotajwa kutumika kuisafirisha.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 12, 2024 baada ya kupata taarifa za utoroshwaji wa mbolea hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi amesema Serikali ilishapiga marufuku lakini kuna watu wameamua kuendelea na mchezo huo aliouita mchafu.
“Taarifa hizo hata sisi tunazo, kuna vijana waendesha bodaboda wamejiajiri wanafanya utoroshaji huo, tunaanza msako tutawakamata wote kwa sababu wanavunja na kukiuka utaratibu wa nchi,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Amesema madereva hao wamejigeuza wasafirishaji wa mbolea hiyo ambayo miaka ya hivi karibuni mchezo huo ulikuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu waliokuwa wakiisafirisha kwa kutumia magari.
Amesema baada ya kubaini wanakamatwa, wameanza kuwaajiri vijana wa bodaboda kuifanya kazi hiyo haramu.
“Nitoe wito kwa wananchi wa vijiji vyote wilayani Ileje, tuwe walinzi na tutoe taarifa pindi tuwaonapo watu wanaosafirisha pembejeo za kilimo hususani mbolea ambayo Serikali yetu imeweka ruzuku kwa kila mfuko ili kuwanufaisha wakulima kununua kwa bei ndogo, wao wanaisafirisha na kwenda kuwauzia wakulima wa nchi nyingine, hili halikubaliki,” amesema Mgomi.
Amesema wakati Serikali ikiendelea kudhibiti utoroshwaji wa mbolea unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu, “kuna watu wanajifanya wana akili zaidi ya Serikali, tutawakamata na tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.”
Agosti 2, 2024, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Agustino Senga alisema wamejipanga kufanya operesheni ya kuwakamata madereva bodaboda wanaojihusisha na usafirishaji wa mbolea ya ruzuku kwenda nchi jirani na kuwaonya kuacha tabia hiyo mara moja.
“Tumeanza kupokea taarifa kutoka kwa raia wema juu ya wizi wa mbolea ya ruzuku kwenda nchi jirani na wanaisafirisha kwa pikipiki badala ya magari, tunajipanga kukabiliana na wizi huo unaorudisha nyuma mpango wa Serikali wa kuwakomboa wakulima kununua pembejeo kwa bei rahisi,” amesema Kamanda Senga.
Mwananchi imezungumza na baadhi ya madereva bodaboda walioomba hifadhi ya majina yao ambao walikiri pikipiki kutumika kusafirisha mbolea hiyo ya ruzuku.
Mmoja wa madereva hao, amesema madereva bodaboda hutumwa na baadhi ya wafanyabiashara za pembejeo kufanya kazi hiyo.
“Hawa bodaboda wanaagizwa tu kuivusha hiyo mbolea halafu wanalipwa hela ya nauli, na sasa hivi mbolea inavushwa sana na madereva wanalipwa hela nzuri ndiyo maana wengine wameifanya kazi hiyo kama ajira kabisa,” amesema kijana huyo.
Dereva mwingine amesema kama Serikali ina nia ya kukomesha utoroshaji huo, iwashirikishe madereva bodaboda kuwabaini wahusika.
“Ila (Serikali) ikija na vitisho vya kuwakamata, hawatawajua wahusika hasa ni kina nani, Jeshi la Polisi likae vizuri tu na hawa madereva watawatajia matajiri wote wanaowatuma,” amesema dereva huyo.