Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh500 milioni za Stanbic kuwakomboa watoto Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla (katikati) akizindua Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dk Hussein Ali Mwinyi kilichopo Mwanakwerekwe, Zanzibar. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Maalim, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Saada Mkuya Salum na Afisa Mkuu wa Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, Derick Lugemala.

Muktasari:

  • Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dk Hussein Ali Mwinyi kina uwezo wa kuhudumia watoto hadi 60 kwa siku, kikitoa huduma za malezi, elimu ya awali, lishe, afya na ulinzi , huku kikiwawezesha wazazi, hususan wanawake, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

Unguja. Wanawake wafanyabiashara katika Soko la Mwanakwerekwe sasa wameondolewa hofu ya kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kutokana na jukumu la kulea watoto wadogo, baada ya kujengewa Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dk Hussein Ali Mwinyi.

Kituo hicho kilichojengwa kwa gharama ya Sh500 milioni ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Benki ya Stanbic Tanzania na kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia watoto 60.

Kufuatia kukamilika kwa mradi huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameipongeza Benki ya Stanbic Tanzania wakati wa uzinduzi wa Programu ya Malezi na Makuzi ya Mtoto na ufunguzi rasmi wa kituo hicho.

Akizungumza katika hafla hiyo, Hemed amesema uwekezaji katika malezi na makuzi ya mtoto katika umri wa awali ni msingi wa kujenga taifa lenye rasilimali watu bora, na kuzitaka taasisi za kifedha pamoja na sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwekeza kwenye maendeleo ya watoto.

Aliipongeza Benki ya Stanbic Tanzania kwa kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kuimarisha huduma za malezi ya watoto na kuzihimiza benki nyingine kuiga mfano huo.

"Tunaipongeza Benki ya Stanbic kwa uwekezaji huu wa kimkakati na mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Nazihimiza taasisi nyingine za kifedha kuiga mfano huu wa kushiriki katika ujenzi wa taifa," amesema.

Kituo hicho cha malezi ni miongoni mwa miradi ya kwanza inayotekelezwa kupitia mpango wa 'Adopt an ECD Centre', unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Benki ya Stanbic Tanzania na Save the Children International kwa lengo la kupanua huduma bora za malezi na makuzi ya watoto katika umri wa awali.

Kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia watoto hadi 60 kwa siku, kikitoa huduma za malezi, elimu ya awali, lishe, afya na ulinzi wa mtoto, huku kikiwawezesha wazazi, hususan wanawake, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya Salum amesema programu hiyo itaunganisha huduma za afya, lishe, elimu ya awali, malezi na ulinzi wa mtoto kwa watoto wenye umri wa kuzaliwa hadi miaka minane.

Amesema utekelezaji wa programu hiyo ya miaka mitano unakadiriwa kugharimu Sh205.2 bilioni, zitakazotolewa na Serikali, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Fedha na Uzalishaji Thamani wa Benki ya Stanbic Tanzania, Derick Lugemala amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuwekeza kwenye miradi yenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii.

"Kwa zaidi ya miaka 30 benki hii imekuwa mshirika wa maendeleo ya Tanzania na kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa imekuwa sehemu ya safari ya maendeleo ya Zanzibar. Tanzania ni nyumbani kwetu, nasi tunachochea maendeleo yake," amesema.

Lugemala amesema Sh150 milioni zilizobaki kutoka katika ahadi ya benki ya Sh500 milioni zitatumika kujenga vituo vingine vya malezi na makuzi ya watoto katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kuongeza upatikanaji wa huduma hizo.

Amesema uwekezaji huo unaonyesha mafanikio yanayoweza kupatikana pale Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo wanaposhirikiana katika kuboresha ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.