Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri ya ubilionea wa matajiri wakubwa duniani

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa duniani kuna mabilionea wa Dola za Marekani (wenye ukwasi unaozidi Sh2.7 trilioni) takribani 3,200. Kati ya hao, zaidi ya 1,000 wanatokea Amerika ya Kaskazini, zaidi ya 900 wanatokea Ulaya, Asia wana zaidi ya 800, huku Afrika ikiwa nao chini ya 50.

Katika kila bara duniani, kuna mtu mmoja ambaye ni tajiri zaidi katika bara hilo. Watu hawa si tu kwamba wamejipatia mali nyingi, bali pia wamejijengea hadhi na ushawishi mkubwa kupitia biashara na uwekezaji wao.

Katika bara la Afrika, kuna Aliko Dangote wa Nigeria, mmiliki wa Dangote Group inayohusika na bidhaa mbalimbali; Asia kuna Mukesh Ambani wa India, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Reliance Industries; Ulaya kuna Bernard Arnault wa Ufaransa, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa LVMH (Louis Vuitton Moet Hennessy); Amerika Kaskazini ni Elon Musk wa Marekani, Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla na SpaceX; Amerika Kusini kuna Jorge Paulo Lemann wa Brazil, mwekezaji na mwanzilishi mwenza wa 3G Capital; na Australia ni Gina Rinehart, Mwenyekiti wa Hancock Prospecting, kampuni ya madini.

Kila mmoja wao ana historia ya kipekee ya jinsi walivyopanda ngazi za mafanikio na kuunda himaya kubwa za biashara.


Amerika Kaskazini: Elon Musk (Marekani)

Elon Musk ni mmoja wa wajasiriamali wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani, alizaliwa Jumatatu ya Juni 28, 1971 huko Pretoria, Afrika Kusini. Baada ya kuhamia Canada kwa masomo ya chuo kikuu, Musk hatimaye alienda Marekani ambako alisoma katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania.

Mwaka 1999 kampuni hii iliuziwa kampuni ya Compaq kwa dola milioni 307, na kumuwezesha Musk kuanza miradi mingine mikubwa. Elon Musk alianzisha X.com mwaka 1999, ambayo ni kampuni ya huduma za kifedha mtandaoni, ambayo hatimaye ilibadilika kuwa 'PayPal' baada ya kuungana na kampuni nyingine. PayPal ilipata umaarufu mkubwa na kununuliwa na kampuni ya eBay kwa dola bilioni 1.5 mwaka 2002.

Mwaka 2002, Musk alianzisha SpaceX (Space Exploration Technologies Corp.), akilenga kupunguza gharama za safari za anga na hatimaye kuwezesha mwanadamu kuishi kwenye sayari nyingine. SpaceX imepata mafanikio makubwa, ikiwa kampuni ya kwanza binafsi kurusha na kurejesha roketi kutoka angani, na pia kuwa na mikataba na Mamlaka ya Taifa ya Usafiri wa Anga za Juu (NASA) kwa ajili ya safari za anga.

Elon Musk pia alijiunga na kampuni ya Tesla Motors mwaka 2004 kama mwenyekiti na baadaye kuwa Mtendaji Mkuu. Mbali na SpaceX na Tesla, Musk pia amewekeza katika miradi mingine kama vile SolarCity, kampuni ya nishati ya jua, na The Boring Company, inayolenga kutatua matatizo ya msongamano wa magari mijini kwa kujenga barabara za chini ya ardhi.

Elon Musk amewekeza biashara zake katika nchi nyingi tofauti, ikiwamo Marekani, China na nchi za Ulaya. Kwa mujibu wa Forbes, utajiri wa Elon Musk unakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 200, akishika nafasi za juu katika orodha ya matajiri wakubwa zaidi duniani. Utajiri huu unatokana na thamani ya hisa zake katika Tesla, SpaceX na kampuni nyingine alizozianzisha au kuwekeza.

Kampuni yake ya huduma za intaneti kwa njia ya Setelaiti (Starlink) hivi sasa inatoa huduma katika nchi zaidi ya 100 duniani.


Ulaya: Bernard Arnault (Ufaransa)

Bernard Arnault, mmoja wa matajiri wakubwa zaidi barani Ulaya na duniani kote, alizaliwa Jumamosi ya Machi 5, 1949 huko Roubaix, Ufaransa. Alikulia katika familia yenye mazingira ya biashara, ambapo baba yake alimiliki kampuni ndogo ya ujenzi. Baada ya kumaliza masomo yake, Arnault alijiunga na biashara ya familia na hatimaye kuigeuza kuwa kampuni kubwa ya mali isiyohamishika. Hata hivyo, ndoto zake zilikuwa mbali zaidi ya biashara ya mali isiyohamishika.

Mwaka 1984, alipochukua uongozi wa kampuni ya kutengeneza nguo iliyokuwa ikiporomoka, Boussac Saint-Freres, aliona fursa kubwa katika bidhaa za kifahari. Arnault alifanya uamuzi wa kimkakati kununua kampuni ya Christian Dior, mojawapo ya majina maarufu katika ulimwengu wa mitindo.

Arnault aliendelea kununua na kuunganisha kampuni mbalimbali chini ya mwavuli wa LVMH (Louis Vuitton Moet Hennessy), ambayo sasa inamiliki zaidi ya bidhaa 70 maarufu duniani katika sekta za mitindo, vinywaji, manukato na vito vya thamani.

Mojawapo ya siri za mafanikio ya Arnault ni uwezo wake wa kuona thamani katika bidhaa za kifahari na kujua jinsi ya kuziboresha na kuziuza kwenye masoko mbalimbali duniani. Alikuwa na uwezo wa kipekee wa kuchanganya ubunifu na biashara, hivyo kuvutia wateja wa hadhi ya juu kutoka pande zote za dunia.

Bidhaa zake zinauzika katika miji mikubwa kama New York, Tokyo, Paris na London. Hii imeifanya LVMH kuwa jina maarufu kwa bidhaa za kifahari na mtindo wa maisha wa hali ya juu.

Utajiri wa Bernard Arnault umemuweka katika nafasi za juu za orodha za matajiri wa dunia. Kwa mujibu wa Forbes, thamani yake inakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150. Bernard Arnault pia ni mpenzi wa sanaa na amekuwa akikusanya kazi za wasanii maarufu kama Pablo Picasso, Andy Warhol na Claude Monet.


Asia: Mukesh Ambani (India)

Mukesh Ambani alizaliwa Ijumaa ya Aprili 19, 1957 mjini Aden, Yemen. Yeye na Dangote walipishana wiki moja tu katika kuzaliwa kwao. Mukesh ni mtoto wa kwanza wa mfanyabiashara maarufu Dhirubhai Ambani na mkewe Kokilaben Ambani. Familia yao ilihamia Mumbai, India, ambapo Mukesh aliendelea na masomo yake.

Alipata shahada ya kemia katika Taasisi ya Teknolojia ya Kemia ya Mumbai na baadaye akaenda Chuo Kikuu cha Stanford kwa masomo ya juu. Mukesh Ambani alijiunga na biashara ya familia, Reliance Industries, mwaka 1981. Reliance Industries ilianzishwa na baba yake, Dhirubhai Ambani, na imeshamiri kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi nchini India.

Reliance Industries imewekeza katika nchi nyingi duniani, na hivyo kufanya jina la Mukesh Ambani kuwa maarufu kimataifa. Mojawapo ya mafanikio yake makubwa ni uzinduzi wa 'Reliance Jio', kampuni ya mawasiliano ya simu, mwaka 2016.

Reliance Jio ilibadilisha kabisa sekta ya mawasiliano nchini India kwa kutoa huduma za mtandao wa kasi kwa bei nafuu, jambo lililomfanya kupata wateja wengi na kuongoza soko la mawasiliano nchini humo. Mbali na mawasiliano, Reliance Industries pia imewekeza katika sekta ya nishati na miundombinu.

Utajiri wa Mukesh umemuweka kwenye orodha ya watu matajiri zaidi duniani. Kwa mujibu wa jarida la Forbes, thamani yake inakadiriwa kufikia zaidi ya dola bilioni 80. Anamiliki jumba la kifahari la makazi, lijulikanalo kama 'Antilia', ambalo ni mojawapo ya majengo ya gharama kubwa zaidi duniani. Likiwa na orofa 27, Antilia lina huduma zote za kifahari kama vile bustani za kutua helikopta, kumbi za michezo na maduka ya kifahari.


Amerika Kusini: Jorge Paulo Lemann (Brazil)

Jorge Lemann wa Brazil, aliyezaliwa Jumamosi ya Agosti 26, 1939, ni mmoja wa wajasiriamali wenye ushawishi mkubwa na tajiri zaidi duniani. Alianza safari yake ya kibiashara baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Harvard, ambapo alisomea masuala ya biashara.

Mwaka 1971 alianzisha kampuni ya uwekezaji ya Banco Garantia, ambayo aliiweka kwenye soko la biashara la Brazil. Kwa kutumia maarifa yake na uzoefu katika uwanja wa fedha, Lemann alianzisha kampuni ya 3G Capital pamoja na wenzake, Marcel Telles na Beto Sicupira.

Kampuni hii imewekeza katika mashirika mbalimbali, ikiwamo Anheuser-Busch InBev, ambayo ni kampuni kubwa ya vinywaji inayojulikana kwa kutengeneza bia maarufu kama Budweiser na Corona.

Lemann amewekeza biashara zake katika nchi nyingi tofauti, ikiwa ni pamoja na Marekani, Canada na nchi za Ulaya. Kwa mujibu wa Forbes, utajiri wa Lemann unakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 20, akishika nafasi ya juu katika orodha ya matajiri wa dunia.


Australia: Gina Rinehart

Gina Rinehart ni mmoja wa wanawake wenye utajiri mkubwa zaidi duniani na Mwenyekiti wa Kampuni ya Madini ya Hancock Prospecting nchini Australia. Gina amekuwa mfano wa kuigwa katika ulimwengu wa biashara, akionesha jinsi juhudi na maono vinavyoweza kuleta mafanikio makubwa.

Gina amewekeza katika nchi nyingi tofauti kupitia kampuni ya Hancock Prospecting na kampuni nyingine anazosimamia. Uwekezaji wake umejikita katika sekta ya madini, ambayo ni msingi wa utajiri wake.

Kwa mujibu wa Forbes, utajiri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 30. Hii inamfanya kuwa mmoja wa wanawake tajiri zaidi duniani. Utajiri wake unajumuisha mali za madini, hisa katika makampuni mbalimbali, na uwekezaji mwingine wa kimkakati.

Matajiri hawa katika kila bara wamejenga himaya zao za kifedha kupitia juhudi, uvumilivu na uwekezaji wa kimkakati, na wote wameonesha njia tofauti za kufanikisha malengo yao na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa dunia.

Kupitia sekta mbalimbali kama vile uzalishaji wa saruji, mawasiliano, mitindo ya kifahari, teknolojia, uwekezaji wa kifedha na madini, matajiri hawa wameweka alama yao kwenye historia ya biashara na kuonesha kuwa inawezekana kufikia mafanikio makubwa kwa kuzingatia maono na bidii.

Kwa kuzingatia mfano wao, tunaweza kujifunza thamani ya ubunifu, usimamizi bora, na uwekezaji wenye tija kama nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi.


Afrika: Aliko Dangote (Nigeria)

Tukianza na Aliko Dangote, yeye alizaliwa Jumatano ya Aprili 10, 1957 katika mji wa Kano, Nigeria. Kutoka katika familia ya kibiashara, aliendeleza haraka shauku yake ya ujasiriamali. Dangote alihitimu masomo ya biashara kutoka Chuo Kikuu cha Al-Azhar jijini Cairo, Misri, na baada ya kurudi nyumbani alianzisha Dangote Group mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 20 tu.

Dangote Group, ambayo ilianza kama biashara ndogo ya kuuza nafaka, imekua na kuwa mojawapo ya makampuni makubwa zaidi barani Afrika. Kampuni hii imewekeza katika sekta mbalimbali, ikiwamo saruji, sukari, chumvi na unga. Hata hivyo, mafanikio makubwa yalikuja kupitia sekta ya saruji ambapo Dangote Cement imekuwa mtengenezaji mkubwa zaidi wa saruji barani Afrika.

Uwekezaji wa Dangote haubakii Nigeria pekee, bali umesambaa katika nchi nyingi barani Afrika. Kampuni ya Dangote Cement ina viwanda vya uzalishaji katika nchi kama vile Ethiopia, Zambia, Tanzania na Senegal. Hii imefanya jina la Dangote kuwa maarufu si tu nchini Nigeria, bali kote barani Afrika na duniani kote.

Mbali na sekta ya saruji, Dangote pia amewekeza katika sekta ya mafuta na gesi. Mradi wake wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta huko Lagos, Nigeria, unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya nishati barani Afrika.

Kiwanda hiki kinatarajiwa kusafisha mapipa milioni 650 ya mafuta kwa siku, na hivyo kupunguza utegemezi wa Afrika kwa mafuta kutoka nje. Kwa mujibu wa Forbes, utajiri wa Dangote unakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 14.