Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanesco yaingia mkataba uzalishaji megawati 100 umeme wa jua

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi akishuhudia utiaji saini kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange (kushoto), na mwakilishi wa kampuni za Sagemcom Energy & Telecom SAS na STEG International Services, João Jiria (kulia), ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu. Picha na Hellen Mdinda.

Muktasari:

  • Unatekelezwa kuanzia sasa Julai, 2026 na utachukua miezi 17 na kugharimu Sh 204.4 bilioni

Kishapu. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesaini mkataba wa utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100, utakaotekelezwa eneo la Ngunga wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga.

Hafla hiyo ya utiaji saini mkataba wenye thamani ya Sh204.7 bilioni, kati ya Tanesco na kampuni za Sagemcom Energy & Telecom SAS na STEG International Services, imeshuhudiwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo leo Jumatatu Julai 27, 2026, Waziri Ndejembi amesema mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mseto wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme, ukiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, wa gharama nafuu na unaotokana na vyanzo vya nishati jadidifu.

Amefafanua kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati 150.

Amesema awamu ya kwanza yenye uwezo wa megawati 50 iligharimu Sh118.3 bilioni na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji.

Aidha, Waziri Ndejembi amesema awamu ya pili yenye uwezo wa megawati 100, ambayo utekelezaji wake umeanza rasmi kupitia utiaji saini wa mkataba, utagharimu Sh204.7 bilioni.

 Jumla ya gharama za utekelezaji wa awamu zote mbili ni Sh323 bilioni.

“Huu ni uwekezaji mkubwa na Serikali imeamua kwenda hatua nyingine ya kuongeza ‘energy mix.’ Mradi huu unahakikisha upatikanaji wa umeme muda wote, pia, bado tuna safari ya kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

“Tanesco ihakikishe mradi huu unakamilika ndani ya muda uliowekwa na wananchi wanufaike wakati wa utekelezaji na baada ya mradi kukamilika,” amesema Ndejembi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange katika hafla fupi ya utiaji saini utekelezaji mradi wa awamu ya pili amesema: “Mradi huu wa awamu ya pili utatekelezwa kwa muda wa miezi 17 kuanzia sasa na kipindi cha uangalizi cha miezi 24, pia, utagharimu Sh204 bilioni pamoja na kuwaletea wananchi wa Ngunga maji pamoja na zahanati.”

Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Kishapu, Josephat Limbe amesema katika awamu ya kwanza takribani wananchi 300 wamenufaika na mradi wa umeme jua huku akiwaita wawekezaji kwenda kuwekeza Kishapu hasa katika viwanda.

“Mradi huu utahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hasa katika sekta ya viwanda, kwa sababu umeme tunao na unaongezwa, kwa awamu ya kwanza takribani wananchi 300 wamenufaika na mradi huu,” amesema Limbe.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngunga, Musa Masesa amesema, “ujio wa mradi huu umeweka kijiji chetu katika hali ya kutambulika, maana kilikuwa kimesahaulika, hivyo tunashukuru kwa sasa wananchi hawateseki na umeme, changamoto iliyopo ni upatikanaji wa maji.

“Tunaomba mkandarasi anayekuja atunufaishe na mradi huu wa awamu pili kwa kutuletea maji, wananchi wa Ngunga tuna changamoto kubwa ya maji na zahanati ambavyo tumeahidiwa inakwenda kutekelezwa.”

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema fedha ambazo mkoa wake umepokea kutoka serikalini kwa ajili ya miradi mbalimbali ni Sh1.63 trilioni.

Pia, amesema kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga anashukuru kwa ajili ya mradi huo utakaoongeza uwekezaji.