Tanzania kufikisha uchumi wa buluu COP28
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kufungua mkutano wa kitaifa wa wadau wa mazingira jijini Arusha.
Muktasari:
- Mkutano huo wa kila mwaka unaolenga kujadili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, utafanyika kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023 ukishirikisha zaidi ya mataifa 200 duniani zilizosaini makubaliano ya awali ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa mwaka 1992.
Arusha. Serikali imepitisha uchumi wa buluu Tanzania kuwa moja ya ajenda zitakazowalishwa na wataalamu wa hapa nchini kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaotarajiwa kufanyika Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mkutano huo wa kila mwaka unaolenga kujadili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, utafanyika kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, mwaka huu ukishirikisha zaidi ya mataifa 200 duniani zilizosaini makubaliano ya awali ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa mwaka 1992.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga baada ya kufungua mkutano wa kitaifa wa wadau wa mazingira jijini Arusha amesema wanaibeba ajenda ya uchumi wa buluu kwenye mkutano huo kwa ajili ya majadiliano ya kupata uzoefu wa nchi zilizoendelea zinafanyaje kunufaika nao zaidi kwa ajili ya kuiga na kuja kuzitekeleza.
Mbali na hilo alisema kuwa pia watawasilisha kanuni mpya waliyoipitisha mwaka 2022 na kuifanyia maboresho mwaka huu juu ya biashara ya kaboni inayoonyesha jinsi Tanzania tumehifadhi misitu kwa ajili ya kunyonya ya kupunguza hewa ya ukaa angani.
“Ajenda ya uchumi wa buluu na hiyo kanuni mpya ya biashara wa kaboni tutaiwasilisha kwa ajili ya kuwaeleza nchi zilizoendelea jinsi Tanzania tunavyowekeza kwenye misitu na bahari pia kiasi cha hewa chafu tunachonyonya angani kwa ajili ya kupatania malipo tunayostahili kupata kutoka kwenye mifuko inayodhamini biashara hii,” amesema.
Alisema kuwa mbali na hilo pia Tanzania imepitisha ajenda ya kilimo cha kisasa kisichosababisha tatizo la mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya nishati safi ya gesi na umeme yasiyotumia kuni na mkaa.
“Hizi ajenda tumeridhia kuziwasilisha katika mkutano huo baada ya majadiliano na wadau wa ndani ambao nao wameleta hadi maandiko hivyo tunakwenda kuzifikisha huko kwa wenzetu kubadilishana uzoefu kwa wao wamewezaje kukabiliana lakini pia waone namna ya kushirikiana na sisi hata kifedha katika kuzitekeleza na kwetu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi,”
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dk Omar Dadi Shajak amesema mkutano huo wa COP28 utakuwa ni mkusanyiko muhimu kwa Tanzania kuwasilisha changamoto zake lakini pia kupata majibu ya athari zake wanazokabiliana nazo kama nchi.
“Hili ni jukwaa muhimu kama nchi hivyo tunavyokwenda kuwasilisha hizi ajenda muhimu ni kwa ajili ya kusaidia Tanzania kimanufaa ya namna ya kupaisha uchumi wa buluu lakini pia biashara ya hewa ya ukaa,”
Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Paul Deogratius ametaja dhamira kuu ya wajumbe hao kukutana jijini Arusha ni kujadili kwa pamoja yaliyojiri kwenye COP27 iliyofanyika nchini Misri mwaka 2022 ikiwemo mafanikio, changamoto na mwelekeo wan chi kuelekea COP28.