Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tira yatoa kauli kuongezeka kwa ofisi za bima nchini

Meneja wa mipango na usuluhishi kutoka Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Edger Shao

Muktasari:

  • ‎Kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu huduma za bima kutachochea matumizi yake, kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

‎Dodoma. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), imesema kuongezeka kwa ofisi za kampuni za bima nchini kutarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza matumizi ya bima na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Meneja wa Mipango na Usuluhishi wa Tira, Edgar Shao amesema hatua hiyo pia itasaidia kufikia lengo la kuongeza mchango wa sekta ya bima katika pato la Taifa kutoka asilimia 2.18 za sasa hadi asilimia tatu ifikapo mwaka 2030.

Shao ameyasema hayo leo Alhamisi, Julai 2, 2026, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa ofisi ya mauzo ya Alliance Life Assurance.

Amesema kufunguliwa kwa ofisi hiyo kutawawezesha wakazi wa Dodoma na maeneo jirani kupata huduma mbalimbali za bima kwa urahisi, zikiwemo bima za maisha, moto na kilimo, huku ikichochea pia ongezeko la uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima.

Amesema pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma, elimu kwa umma inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuongeza matumizi ya bima nchini.

"Tunawaomba waandishi wa habari muwe mabalozi wa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima. Tunaamini kupitia elimu na kuendelea kufunguliwa kwa ofisi za kampuni za bima tutafikia lengo la kuongeza mchango wa sekta ya bima katika pato la Taifa hadi asilimia tatu ifikapo mwaka 2030," amesema Shao.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Alliance Life Assurance, Byford Mutimusakwa, amesema bima ya maisha ni moja ya nyenzo muhimu za ulinzi wa kifedha kwa kuwa huwasaidia wanufaika kukabiliana na changamoto za kiuchumi pale mteja anapofariki dunia au kupata ulemavu wa kudumu.

Aidha, amesema sekta ya bima ina mchango mpana katika maendeleo ya uchumi kwa kuwa fedha zinazokusanywa kupitia huduma hizo huwekezwa katika sekta mbalimbali na hivyo kuongeza mitaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Meneja wa banassurance na Maendeleo ya biashara za bima ya maisha wa alliance life, Tumaini Pyanisa akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa ofisi Jijini Dodoma leo Julai 2, 2026. Picha na Rachel Chibwete

Mbali na hilo, amesema Alliance Life Assurance imeendelea kuchangia ajira kwa Watanzania, ambapo idadi ya wafanyakazi imeongezeka kutoka 16 mwaka 2016 hadi 94 mwaka 2025.

Naye Meneja wa Bancassurance na Maendeleo ya Biashara za Bima ya Maisha wa Alliance Life Assurance, Tumaini Pyanisa, amesema pamoja na kupanua mtandao wa huduma, kampuni hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu bima ya maisha kutokana na uelewa mdogo uliopo kuhusu manufaa yake.

Amesema bima ya maisha hutoa kinga ya kifedha kwa familia au wanufaika pale mteja anapofariki dunia, anapopata ulemavu wa kudumu au kukumbwa na changamoto nyingine zinazotambuliwa katika mkataba wa bima.