Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TPA kuwekeza Sh12.1 trilioni kuboresha bandari, kuongeza uwezo wa kupokea shehena  

Muktasari:

  • Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepanga kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Sh12.1 trilioni kuongeza uwezo wa bandari hadi tani milioni 62 ifikapo 2030/31.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepanga kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Sh12.1 trilioni ndani ya miaka 5, ikiwa ni mkakati wa kuongeza uwezo wa bandari kukidhi ongezeko la shehena kutoka tani milioni 32.8 hadi tani milioni 62 ifikapo mwaka 2030/31.

Kati ya fedha hizo, Sh1.7 trilioni zitatoka serikalini kupitia TPA, huku Sh5 trilioni zikitarajiwa kupatikana kupitia ushirikiano wa sekta binafsi (PPP).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Machi 03, 2026.

Akizungumza leo Jumanne, Machi 3, 2026 wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alisema miradi hiyo inalenga kupanua miundombinu, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za usafirishaji.

Mbossa amesema miongoni mwa miradi mikubwa ni ujenzi wa magati manne mapya namba 12 hadi 15 katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi kwa wakati mmoja.

Mwonekano wa eneo la mradi wa ujenzi wa Matanki ya Kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Pia, TPA inaendelea na ujenzi wa gati mbili katika eneo la majahazi zenye urefu wa mita 500, mradi unaotekelezwa kwa fedha za ndani katika mwaka wa fedha 2025/26.

Aidha, kuna maandalizi ya ujenzi wa kituo cha reli na mtandao wake ndani ya bandari hiyo ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa reli na kupunguza msongamano wa malori.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuweka jiwe la msingi Mradi wa Ujenzi wa Matanki ya kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni, jijini Dar es Salaam,  Machi 03, 2026.

Katika kuimarisha bandari za mikoa, TPA imeanza ujenzi wa bandari ya Kisiwa Mgao katika Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kuhudumia shehena chafu. Pia kuna mipango ya ujenzi wa gati la mafuta Dar es Salaam, pamoja na maandalizi ya miradi katika Bandari ya Tanga, Bagamoyo (Mbegani) na Mwambani mkoani Tanga.

Kwa upande wa miundombinu unganishi, TPA kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania inapanga ujenzi wa barabara maalumu ya mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze na Morogoro, pamoja na barabara ya lami kutoka Tanga hadi Tabora kupitia Singida.

Mwonekano wa eneo la mradi wa ujenzi wa Matanki ya Kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Wakati huohuo, TPA inatekeleza ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhi mafuta katika eneo la Tungi, Kigamboni. Mradi huo unaotekelezwa na makandarasi kutoka China, ulikuwa umefikia asilimia 41 ya utekelezaji hadi Machi 2, 2026 na unatarajiwa kukamilika Februari 3, 2027.

Matanki hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000 (lita milioni 378) za dizeli, petroli na mafuta ya ndege. Mradi umejumuisha mifumo ya kisasa ya kuzuia moto, kupima na kupampu mafuta moja kwa moja kutoka melini hadi kwenye matanki.

Kwa sasa, meli za mafuta hutumia hadi siku 22 kusubiri kupakua mzigo na siku saba kushusha mafuta, hali inayosababisha gharama za ucheleweshaji za dola 25,000 kwa siku. Mbossa amesema mradi ukikamilika, muda wa kusubiri utapungua hadi siku saba na upakuaji kufanyika ndani ya saa 24.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kushughulikia shehena za mafuta kutoka tani milioni sita hadi tani milioni 12 kwa mwaka, pamoja na kuongeza ajira kwa wazawa na fursa za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka eneo la mradi.