TPC yavunja rekodi ya uzalishaji kwa miaka 93

Shehena ya sukari ikiwa imepangwa katika Kiwanda cha TPC, Moshi. Picha na Omben Mjema

Muktasari:

  • Kiwanda cha Sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro kimeweka rikodi mpya baada ya kuzalisha tani 116,500 za sukari kwa kipindi cha mwezi Juni 2022  hadi Machi mwaka huu  ikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930's.

Moshi. Kiwanda cha sukari cha TPC, kimeweka rikodi mpya baada ya kuzalisha tani 116,500 za sukari kwa kipindi cha Mwezi Juni 2022 hadi Machi mwaka huu  ikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930's.

 Msimu uliopita wa mwaka 2022 kiwanda hicho kiliweza kuzalisha sukari tani 108,000 huku miwa ikizalishwa tani 1.1 milioni kwa msimu, ambapo pia pamoja na mambo mengine kina uwezo wa kuzalisha tani 600 za sukari kwa siku.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu Utawala wa TPC, Jaffary Ally wakati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alipotembela kiwanda hicho wakati wakifunga msimu wa uzalishaji wa sukari.

Amesema kwa kipindi cha mwezi Juni mpaka Machi mwaka huu wameweza kuzalisha miwa tani 1,150,000 ambazo ziliweza kuzalisha sukari tani 116,500 ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kulinganisha na miaka mingine.

"Kiwanda cha sukari TPC tumefanya uzalishaji mkubwa kuliko kipindi chochote toka tumeanza kuzalisha sukari mwaka 1936, kwa hiyo tumezalisha miwa tani 1,150, 000 na kuzalisha tani za sukari tani 116,500 ambapo hiki ni kiwango cha juu zaidi na imekuwa ni faraja kwetu kama wazalishaji wa sukari hapa nchini,"

"Tunaishukuru serikali kwa kutuwekea mazingira mazuri ya uzalishaji na kuweza kusaidia wazalishaji kuongeza uwezo wao wa kuzalisha sukari zaidi hapa nchini, lakini hatujaweka rikodi tu ya kuzalisha sukari tumekuwa na rikodi nzuri ya ulipaji wa kodi pamoja na kulipa gawio serikalini," amesema Ally.

Amesema kiwanda hicho kimeweza kutoa gawio la zaidi ya Sh99 bilioni serikalini ikilinganishwa na kipindi cha miaka mingine ambayo walikuwa wakichangia Sh2 bilioni kama sehemu ya gawio na kodi.

Amesema wakati huu wakifunga msimu wa uzalishaji wa sukari wameweza kuweka akiba ya tani 25,000 za sukari ambazo zitauzwa kwa kipindi  kiwanda kimesimama kuzalisha bidhaa hiyo ya sukari.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amekipongeza kiwanda hicho kwa kuweza kufanya vizuri katika uzalishaji wake wa sukari pamoja na kutoa gawio kubwa serikalini la zaidi ya Sh99 bilioni.

Babu amesema kwa kuwa kiwanda hicho kimeweka hifadhi ya kutosha ya sukari zaidi ya tani 25,000 katika msimu huu wa miezi mitatu ambayo kiwanda kimesimamisha uzalishaji wake, wafanyabiashara wanapaswa kuuza sukari kama kawaida kwa bei ambayo ipo masokoni.

"TPC ina sukari ya kutosha naomba niwaondoe wasiwasi wananchi wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani, kwamba kiwanda chetu kina uwezo mkubwa na kina sukari ya kutosha katika kipindi cha miezi mitatu mpaka watakapoanza uzalishaji, wafanyabiashara wawauzie wananchi sukari kwa bei iliyopo sokoni," amesema