Wafanyakazi benki I & M wajitolea damu

Wafanyakazi benki I & M wajitolea damu

Muktasari:

Zaidi ya wafanyakazi 30 wa Benki ya I&M wameongoza kampeni ya kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wengine.

Dar es Salaam. Zaidi ya wafanyakazi 30 wa Benki ya I&M wameongoza kampeni ya kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wengine.

Wafanyakazi hao wameamua kufanya kampeni hiyo ya uchangiaji damu ikiwa ni njia ya kuwasaidia Watanzania kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Akizungumza  mwishoni mwa wiki katika shughuli hiyo meneja masoko na mawasiliano wa benki hiyo,  Anitha Pallangyo amesema wafanyakazi wameonyesha mwitikio wa kipekee na kuishukuru MNH kwa kukubali kushirikiana ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi wenye uhitaji wa damu.

“Niwashukuru wafanyakazi wa benki ya I&M chini ya mpango wa ‘im for you’ wameonyesha mwitikio wa kipekee katika zoezi hili pia niishukuru hospitali ya Muhimbili kwa kukubali kushirikiana ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi wenye uhitaji,” amesema Pallangyo.

Kwa upande wa meneja mkuu wa kitego cha uboreshaji huduma za benki,  Deepali Ramaiya amesema mpango huo ni moja ya mikakati ya aina yake iliyoanzishwa na wafanyakazi wenyewe kwa kujitolea huduma bure kwa jamii.

Ofisa uhamasishaji damu wa MNH, John Bigambalaye amesema kitengo cha damu katika hospitali hiyo kimehamasika na kampeni hiyo.

“Tunashauri na taasisi nyingine ziwe mstari wa mbele kuhamasisha wafanyakazi wake kujitolea kwa jamii ili kusaidia Watanzania wenye uhitaji wa damu,” amesema Bigambalaye.