Wakulima wa Korosho Lindi, Mtwara wapata neema

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua kampeni maalum kwa wakulima wa zao la korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi inayofahamika kama ' Vuna zaidi na NBC Shambani' huku serikali ikiahidi kuunga mkono na kuutumia mkakati huo katika kufanikisha adhma yake ya kuzalisha tani 700,000 za zao hilo kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa zao hilo wakiwemo viongozi wa kiserikali, viongozi vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika, Mkuu wa mkoa wa Mtwara Brig. Jenerali Marco Gaguti alisema mkakati huo umekuja wakati muafaka kipindi ambacho serikali imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka matarajio ya tani 280,000 ya mwaka huu hadi kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

“Ni wazi kwamba NBC Shambani imekuja eneo sahihi kwa wakati sahihi! Serikali ilipojiwekea lengo la kuzalisha tani 700,000 ilifahamu fika kwamba kitovu cha kufanikisha adhma hiyo kipo Mtwara. Imekuwa vema zaidi benki ya NBC imeliona hili pia na sisi wana Mtwara tunawahakikishia kwamba tupo tayari kuupokea mpango huu kwa kuwa umekuja kutushika mkono. Rai yangu kwa wana Mtwara naomba tuipokee NBC Shambani ili kwa pamoja tufanikishe hili’’ alisema.

Aidha, Brig. Jenerali Gaguti alilisisitiza suala zima la nidhamu ya fedha miongoni mwa wakulima wa zao hilo huku akitoa wito kwa viongozi vyama vya msingi (AMCOS). vyama vikuu vya ushirika na wakulima kwa ujumla kutumia vema mafunzo yanayotolewa na benki hiyo kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba, matumizi ya bima mbalimbali ikiwemo bima ya afya pamoja na kuwekeza kwenye zana za kisasa za kilimo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa benk ya NBC, Theobald Sabi alisema kampeni hiyo ya miezi mitatu ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kujidhatiti kwenye kuinua kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo zao la Korosho kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Tunashukuru kuona kwamba adhma yetu hii tayari imepokelewa vyema na walengwa ambao ni wakulima na hiyo ndio sababu hadi leo hii tunapozindua kampeni hii ya NBC Shambani tayari zaidi ya AMCOS 40 na wakulima wa korosho zaidi 11,000 wamejiunga na huduma hii.  Tunashukuru kwa mapokeo haya na kupitia kampeni hii pamoja na kutoa zawadi mbalimbali tutaendelea kutoa elimu na hamasa kwa wakulima zaidi ili tufikie malengo yetu kwa pamoja,’’ alisema.

Akizungumza zaidi kuhusu kampeni hiyo, Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa alisema kupitia kampeni hiyo wakulima wa zao hilo wataweza kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo baiskeli, pikipiki, pampu za kupulizia dawa na zawadi za kifamilia ikiwemo kanga, mabegi na madaftari.

“Kwa upande wa wa vyama vya msingi (AMCOS) vinaweza kujishindia zawadi kubwa zaidi ikiwemo maguta (Toyo) pamoja na matrekta. Ili walengwa hawa wote waweze kujishindia zawadi hizi wanatakiwa wafungue akaunti benki ya NBC na wapitishe fedha za malipo yao kwenye akaunti hizo na moja kwa moja watakuwa wameingia kwenye droo ya kujishindia zawadi hizi,’’ alifafanua.

Wakizungumzia kampeni hiyo pamoja na mpango wa NBC Shambani kwa ujumla, viongozi wa AMCOS katika mkoa huo Salum Ngumbo na Habiba Kambutu walisema umekuwa na tija kubwa kwa wakulima huku wakionesha kuvutiwa zaidi na suala la kutokuwepo kwa makato ya fedha zao pindi wanapopitisha fedha hizo kupitia akaunti zao za NBC Shambani.

“Pamoja na uwepo wa zawadi mbalimbali kwenye kampeni hii ambazo kimsingi zitavutia wakulima wengi zaidi kujiunga na benki ya NBC zaidi tunavutiwa na kutokuwepo kwa makato ambayo yamekuwa yakituumiza sana hasa sisi viongozi wa AMCOS pindi tunapopitisha fedha za wanachama wetu kupitia akaunti zetu…kupitia akaunti za NBC Shambani tunashukuru kuona kwamba  changamoto hii imekwisha kabisa,’’ alisemaNgumbo.