Wakulima wa tumbaku wagoma kusaini mkataba na kampuni ya ununuzi

Muktasari:

  • Wakulima wa tumbaku wa Chama cha Msingi Magunga (AMCOS) wakataa kufunga mkataba na kampuni ya Mkwawa.

Katavi. Wakulima wa zao la tumbaku 748 wa Chama cha Msingi Magunga (Amcos) Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wamekataa kufunga mkataba wa uzalishaji na ununuzi na Kampuni ya Mkwawa kwa  msimu wa kilimo 2023/2024 kwa madai  kuwa hawajalipwa malipo yao ya mauzo.

 Akizungumza kwa niaba ya wanachama kwenye kikao cha kutiliana saini mikataba hiyo Mwenyekiti wa (Amcos) ya Magunga, Hamza Nelson amesema wamefikia uamuzi huo kwa  kuwa  hali hiyo  imewaathiri kimaisha.

"Tumeuza tumbaku yetu musimu uliopita lakini hatujalipwa, tuna watoto wanasoma tumekosa mahitaji, tunaishi maisha magumu," amesema Nelson akaongeza…

"Watu wanapata matatizo ikiwemo wagonjwa wanakosa fedha ya kuwatibisha hali hii imesababisha tukae mkutno mkuu tukaridhia kuikataa na leo sijasaini mkataba wao kwa niaba ya wanachama," amesema.

Meneja wa Bodi ya Tumbaku Mkoa wa Katavi, Genuin Swai amekiri kupokea malalamiko ya wakulima wa Chama cha Msingi Magunga (Amcos) na hatua alizochukua.

"Ni kweli waliniandikia barua niliipokea nikaipeleka ngazi husika lakini hadi sasa sijapata majibu," amesema.


"Utaratibu wa musimu huu wakulima wanatakiwa kuuza tumbaku kwenye kampuni walizouzia wakati uliopita, maelekezo haya yametoka kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,"amesema.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Peter Nyakunga amesema (Amcos) zilizopo ni 21 kati yake 21 hazijalipwa malipo ya mauzo ya tumbaku kwa musimu wa 2022/2023.

"Hizi (Amcos) ambazo hazijalipwa imo ya Magunga iliyokataa kusaini mkataba kwa utaratibu uliokuwepo awali walikuwa na haki ya kubadilisha mnunuzi,"amesema Nyakunga.


Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko aliyeshuhudia utiaji saini mikataba hiyo, ametoa onyo kali kwa makampuni yanayonunua tumbaku pasipo kuwalipa wakulima.

"Hatutakubali makampuni ambayo yanachukua tumbaku ya wakulima na kutokomea nayo bila kuwalipa chochote wakulima wetu," amesema Mrindoko.

Mkoa wa Katavi umeongeza uzalishaji wa tumbaku kutoka kilo milioni 6 hadi kufikia kilo milioni 11 kwa sasa umeanzisha utaratibu mpya wa kutiliana saini mikataba na wanunuzi ili kujenga taswira ya kuaminiana.