Zanzibar yaanza safari ya kujitegemea umeme

Mkurugenzi wa Kampuni ya Generation Capital, Bikash Subba (kushoto) na Meneja Mkuu wa Zeco, Mshenga Haidar Mshenga wakitia saini mkataba wa uzalishaji umeme jua wa megawatt 180. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Kampuni ya Generation Capital Limited (GCL) ya nchini Mauritius kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Group zimesaini mkataba na Serikali ya Zanzibar kuanza uzalishaji wa umeme megawagi 180 kwa njia ya nishati safi kuanzia mwaka 2024.

Unguja. Katika kuhakikisha Zanzibar inakuwa na umeme unaojitosheleza na wa uhakika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetia saini na Kampuni zenye ubia za Taifa Group na Generation Capital Ltd, kuzalisha umeme wa nishati jadidifu wa megawatt 180.

 Kwasasa Zanzibar inapokea megawatt 125 kutoka Tanzania Bara- kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambapo uwezo wake umefikia zaidi ya asilimia 90.

Akizunguma wakati wa kusaini mkataba huo ambao unagharimu zaidi ya Sh330 bilioni mjini Unguja leo Jumatatu, Mei 15, 2023, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Nishati na Madini, Joseph Kilangi amesema mradi wa kuzalisha umeme huo utakweda kwa awamu.

“Kwa kuazia mradi huu utazalisha megawatt 30, kwahiyo kila baada ya muda kutakuwa na uzalishaji mpaka zitafikia megawatt 180 ndani ya kipindi cha miaka 25,” amesema Kilangi

Amesema kutokana na hali ya uwekezaji ilivyo kwa sasa na kuongezeka kwa mahitaji, kiwango hicho kinachopokewa ni kidogo hivyo kuhitaji mikakati sio tu kuongeza uzalishaji bali kujitegemea,” amesema

Kwa upande wake, Waziri wa wizara hiyo, Shaibu Hassan Kaduara amesema hatua hiyo inadhihirisha Zanzibar ipo tayari kimaendeleo na kabla ya kufikia makubalino hayo kulikuwa na kampuni zaidi ya 80 zilizoonyesha nia ya kuwekeza katika mradi huo lakini hazikuwa wazi.

“Kampuni hii ya Taifa Group kwa ubia na kampuni ya Generation (ya nchini Mauritius) mmeonyesha uwezo mkubwa mpaka kufikia hapa, haikuwa kazi ndogo kwa hiyo tuendelee kutoa ushirikiano kwa maendeleo ya Zanzibar," amesema

Awali, Mkurugenzi wa Kampuni ya Taifa Group, Rostam Aziz amesema bila kuwa na umeme wa uhakika Zanzibar haiwezi kuwa na uchumi wa uhakika na unaovutia wawekezaji.

Amesema katika kutekeleza mradi huo, Zanzibar itakuwa ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na umeme wa nishati jadidifu wenye kiwango hicho cha megawatt 180.

Rostam amesema,"ninafuraha kubwa sana kwa hatua hii tuliyofikia ya kusaini mkataba muhimu utakaoihakikishia Zanzibar umeme na hatimaye Zanzibar kujitegemea kabisa."

"Nina hakika, Zanzibar itafikia hatua ya kujitegemea kabisa. Bila umeme ni vigumu kufikia uchumi imara. Tena utakuwa umeme utakaohifadhi mazingira," amesema Bilionea huyo

Mfanyabiashara huyo amesema, Zanzibar inakwenda katika ramani ya dunia ya uzalishaji wa umeme wa jua yaani nishati safi.

Pia, ameishukuru Kampuni ya Generation kwa kuwaona na kuwachagua kuwa wabia kwenye utekelezaji wa mradi huo,"mkubwa wa sola katika ukanda huu, yaani Zanzibar imeipiku Tanzania bara."

"Nitoe ahadi hapa kwamba kuanzia mwakani umeme utaanza kuzalishwa," amesema

Akihitimisha, Rostam amesema,"nilianza kuwekeza kwenye simu, nimekuja kwenye ndege na karibuni nitawekeza kwenye hoteli. Tutegemee mambo mazuri sana kwa Zanzibar."