Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Sikushangaa kusikia Ngeleja anataka Urais’

> Mbunge wa Sengerema,William Ngeleja.

Muktasari:

Rafiki wa Ngeleja ambaye alisoma naye katika shule ya msingi Bitoto kati ya mwaka 1976 na 1982, Juma Magina anasema amemfahamu Ngeleja kama mwanakijiji mwenzake na mwanafunzi mwenzake, lakini kikubwa ni kipaji chake cha uongozi alichonacho.

U ongozi ni kipaji alichozaliwa nacho mtu ambacho mwingine hawezi kulazimisha kuwa nacho. Hayo ni maneno ya baadhi ya marafiki wa Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (pichani), aliyeamua kujitosa kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Rafiki wa Ngeleja ambaye alisoma naye katika shule ya msingi Bitoto kati ya mwaka 1976 na 1982, Juma Magina anasema amemfahamu Ngeleja kama mwanakijiji mwenzake na mwanafunzi mwenzake, lakini kikubwa ni kipaji chake cha uongozi alichonacho.

Magina anasema anakumbuka alivyokuwa akisoma naye akiwa darasa la tatu Ngeleja alichaguliwa kuwa kiongozi (kiranja) na alipofika darasa la tano alichaguliwa kuwa kiranja mkuu wa shule.

“Mtu huwezi kuwa kiongozi wa juu kama mchezo wa kuigiza, lazima uwe na kipaji cha uongozi katika nafasi yoyote ile, siyo urais tu. Ngeleja nimesoma naye shule ya msingi Bitoto na

tulipokuwa shule alikuwa machachari, kwani tukiwa darasa la tatu alichaguliwa kuwa kiongozi ambaye alikuwa anawaongoza hadi darasa la saba,” anasema Magina.

“Kati ya wanafunzi wa ajabu tuliowahi kusoma nao, Ngeleja ni mmojawapo, kwani licha ya kuwa kiongozi tulikuwa tunashiriki naye kazi za kilimo kama ilivyokuwa desturi yetu Wasukuma, hivyo sitashangaa kusikia anataka kuwa rais.”

Magina anasema Ngeleja ni mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi ambaye hapendi kuona wanyonge wanaonewa au kunyanyaswa kwa sababu ya hali zao za maisha.

“Mimi sijawahi kuona mtu kasoma anarudi likizo tena kijijini anachunga ng’ombe, anajumuika na vijana wenzake kama mtu wa kawaida, hivyo kwa kuwa hana moyo wa ubaguzi wala kujivuna anaweza kuwatumikia Watanzania kama rais bila kikwazo chochote,” anasema.

Wazee wampa baraka

Mzee mmoja maarufu wa Kijiji cha Butoto, Buswelu Sangija (70) anasema kuwa wao kama wazee tayari walishambariki agombee nafasi hiyo, kwani sifa zote anazo na amewaomba ridhaa ya kufanya hivyo.

Sangija anasema kati ya vijana jasiri kijijini hapo Ngeleja ni mmoja wapo. “Mimi kama ningekuwa mtu ambaye napitisha mgombea urais na uzee wangu huu, ningempitisha William,” anasema Sangija na kuongeza:

“Amezaliwa namuona, amesoma namuona na anakua namuona kwa macho yangu, kila jambo alilokuwa anafanya hapa kijijini nilikuwa namuona, kwa kweli bila unafiki sisi wazee tunamuombea safari yake hiyo iwe ya mafanikio kwa masilahi ya Watanzania wenzake.”

Nilimshawishi agombee ubunge

Sangija anasema mwaka 2005 alimshawishi William agombee Ubunge, kwani aliamini kutokana na kipaji chake anaweza kushika nafasi hiyo.

“Ngoja nikwambie kijana…, William mimi najua uwezo wake, alikuwa anafanya kazi kwenye kampuni kubwa kila kukicha yupo Ulaya, lakini mimi nilimuomba arudi nyumbani agombee ubunge na niliamini atashinda kweli ikawa hivyo, sasa hata kwenye urais sina shaka naye,” anasema Sangija.

Mwalimu amzungumzia

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bitoto ambayo ndiyo shule aliyosoma mbunge huyo wa Sengerema, Renatus Nyanda anasema kuwa kila anapofundisha amekuwa akimtumia Ngeleja kama mfano.

“Ngeleja alisoma hapa mimi huwa namtumia kama mfano ninapo fundisha kuna muda nawaambia wanafunzi mnafahamu kama mbunge wenu alisoma hapa, hivyo muongeze bidii muwe kama yeye,” anasema Nyanda na kuongeza;

“Licha ya kuwa mwalimu hapa kwa muda wa miaka minane, mimi sikumfundisha. Lakini sifa zake nimezikuta. Namfahamu kwa misimamo yake, siyo mtu wa mchezo, anapenda elimu na kujitoa kuwasaidia wengine, hivyo nadhani anaweza kuwatumikia Watanzania akiwa rais.”

Mchungaji amuelezea

Mchungaji wa Kanisa la African Inland Church (A.I.C) Bitoto ambalo ndilo anasali Ngeleja, Mussa Gembe anasema moja ya mambo anayompendea William Ngeleja ni ucha Mungu wake.

“Ngeleja katusaidia kujenga Kanisa, akija tunasali naye, lakini anashiriki kutoa misaada mbalimbali kwa madhehenu mengine na dini nyingine, hivyo siyo mbaguzi jambo ambalo ni jema kwa kiongozi,” anasema Gembe.

Baba mzazi afunguka

Baba mzazi wa mbunge huyo, Mganga Ngeleja anasema hajashituka kusikia mwanawe anataka kugombea urais, kwani kila jambo analofanya lazima amshirikishe.

Ngeleja anasema, “Unajua mwaka 2005 wakati ananiambia kwamba baba nataka kugombea ubunge nilishituka, nikamuuliza unaamini utaweza akanijibu baba nitaweza nikamwambia sawa kagombee na matokeo yake aligombea akashinda.”

Anaongeza: “Wakati huu amerudi tena na kuniambia anataka nafasi ya juu zaidi, kwa sababu ni uamuzi mzuri mimi sina cha kumzuia na kwamba nimempa baraka zote kwenye safari yake hiyo mpya anayoitaka.”

Ngeleja anasema William ni mtoto wake wa tano kati ya watoto saba.

William ni mkulima hodari

“Mwanangu licha ya kuwa na sifa nyingi, msomi, ana kipaji cha kucheza mpira, lakini ni mkulima hodari. Kuna wakati nakumbuka alikuwa akienda shamba anashinda hukohuko hadi jioni. Mimi nafanya kazi ya kumpelekea chakula,” anasema Mganga na kuongeza:

“Naamini mwanangu anao uwezo wa kuwa kiongozi mzuri tu wa taifa hili, akiteuliwa kuwania urais nitafurahi, lakini nitamshauri atimize wajibu wake kama alivyokuwa hapa nyumbani na sehemu zote alizopitia.”

Dada yake amuelezea

Dada mkubwa wa mbunge huyo, Kefrini Mganga anasema hatashangaa kusikia mdogo wake amekuwa rais, kwani amekuwa katika mazingira ambayo yanamfanya awe na sifa zote.

“Mdogo wangu alikuwa anapenda shule tulikuwa tunatofautiana hasa pale akitaka karo ya shule, alikuwa mkali, lakini nilijitaidi kuhakikisha namsaidia kufanikisha malengo yake ambayo kwa sasa tunaona faida ya kile alichokuwa anakitaka. William ni mtu ambaye anathamini elimu kwa kiasi kikubwa,” alisema Kefrini.

Chadema: Ngeleja hawezi kutekeleza ahadi

Katibu wa Chadema Wilaya ya Sengerema, Deogratias Mwigara anasema Ngeleja hafai kuwa rais, kwani sio mtekelejazi wa hadi anazotoa.

“Mtu utawezaje kuwa rais wakati ubunge tu umemshinda, Sengerema aliahidi kujenga barabara ya Kamanga feri, imemshinda leo apewe urais sitageuza nchi kuwa jangwa,”anasema Mwigara .