‘Ex’ amtorosha bibi harusi baada ya kufunga ndoa

Francois Uwihoreye aliyekumbwa na masahibu ya kukimbiwa mkewe baada ya kufunga naye ndoa.

Muktasari:

  • Francois Uwihoreye amebaki na huzuni baada ya mkewe kutoroka na mpenzi wake wa zamani saa chache baada ya kufunga naye ndoa ya kiserikali.Rwanda. Ukistaajabu nya Mussa utayaona ya Firauni! Mwanaume aliyefahamika kwa jina Francois Uwihoreye wa nchini Rwanda, amekumbwa na masahibu baada ya mkewe aliyefunga naye ndoa ya kiserikali kutoroshwa na mchumba wake wa zamani, Jean de Dieu muda mfupi baada ya kukamilisha ahadi yao ya ndoa.

Mashuhuda wa tukio hilo ambao ni majirani zake, wameeleza jinsi mwanaume aliyefika nyumbani hapo na kuondoka na bibi harusi muda mfupi baada ya mume wake kutoka nyumbani kwenda kutafuta riziki.

“Mume wake amekuwa na huzuni baada ya mkewe kutoroka na mwanaume mwingine muda mfupi baada ya kutoka kufunga ndoa yao siku hiyo hiyo,” amesema shuhuda huyo.

Imeelezwa kwamba wawili hao waliotoroka ni wapenzi wa miaka mingi, walirejea eneo hilo baada ya wiki, huku mwanamke akiwa na msimamo tofauti kutaka kuolewa na ‘ex’ wake.

Hata hivyo mwanamke huyo alijitosa kufungua kesi ya talaka ili aishi na mwanaume huyo, ambaye alikuwa akihudumu katika kanisa moja nchini humo.

Imeelezwa Uwihoreye hakuwa na namna zaidi ya kukubali kuachana na mwanamke aliyempenda na kuanza kuishi naye kama mke wa maisha yake.

Ndoto za kijana huyo zilizimwa na mkewe kutokana kufanya uamuzi baada ya kufunga ndoa ya kiserikali.

Akizungumzia tukio hilo, bwana harusi Francois amesema mkewe alimsaliti siku waliyotoka kufunga ndoa ya kiserikali kwa kuamua kuondoka na mwanaume mwingine.

"Nilimwacha mke nyumbani Butare, ameniachia huzuni kwa kitendo alichokifanya,” amesimulia kwa huzuni kijana huyo.

“Walikwenda pamoja Gisenyi. Walitumia wiki mbili kwenye ufukwe. Walikuwa na uhusiano wa kimapenzi," amesema Uwihoreye katika mahojiano na mtandao wa Afrimax English.

Wanandoa hao Warwanda siku hiyo walifunga ndoa ya kiserikali ambayo haikuchukua muda wala gharama kisha kurudi nyumbani.

Siku hiyo ilivyokuwa, Uwihoreye aliondoka nyumbani kwenda katika utafutaji baada ya kukamilisha kufunga ndoa, akiwa na malengo ya kutafuta fedha ili aweze kufanya harusi ya kifahari ya ukumbini, huku nyuma mkewe akitoroshwa na mwanaume mwingine.