Kanisa laaihirisha ndoa baada ya watarajiwa kukiri kuzini

Muktasari:

  • Kanisa la Tana River la nchini Kenya limesitisha ibada ya ndoa iliyokuwa mbioni kufungwa baada ya watarajiwa kukiri kuzini jambo ambalo linasemekana ni kinyume na imani yao kufanywa kabla ya kufunga ndoa. Tovuti ya Daily Nation ya nchini humo imeripoti.

Kenya. Bibi na Bwana harusi watarajiwa wamejikuta wakishindwa kufunga pingu za maisha baada ya Kanisa kukataa kuwafungisha ndoa kutokana na kile kinachodaiwa walishiriki tendo kabla ya kufunga ndoa kitu ambacho ni kinyume na taratibu za dini.

Watarajiwa hao kutoka Kaunti ya Tana River nchini Kenya walikiri kuwa walikuwa wakifanya mapenzi kabla ya ndoa sababu ambayo ililifanya kanisa kuwafukuza na kutaka wakatubu.

Inaelezwa kwamba wakati wa kikao cha ushauri na maungamo kwa wanandoa hao watarajiwa, bwana harusi alikiri lakini bibi harusi mtarajiwa alikana kuwahi kushiriki tendo hali ambayo ilimfanya Mchungaji kuwaita ofisini na baadae kukiri.

Hatua hiyo ilimfanya Mchungaji Eli Mwakisha, kukasirika na kutishia kuwalaani wawili hao. Mwakisha aliwafukuza ofisini kwake na kuita timu ya maombezi kwa ajili ya sakata hilo.

Baada ya saa mbili za maombi mazito, aliwaita tena ofisini na kuwaambia watengane na kusimamisha mipango ya harusi kwa muda wa miezi 12 huku akisema hayo yalikuwa ni maagizo ya Mungu.

Kiongozi wa maombi katika kanisa hilo Helida Kase, amesema wawili hao waliagizwa kutumia muda huo kutubu na kuomba, lakini pia wahakikishe wanahudhuria ushauri wa wanandoa kila Jumatano, Ijumaa na Jumapili.

Wanandoa hao watarajiwa walikataa kuzungumzia suala hilo huku baadhi ya waumini wa kanisa wakiona kuwa hio haitakuwa harusi ya kwanza kusimamishwa au kufutwa, kama ilivyo kawaida wakati watarajiwa walio katika uchumba wakigundulika wamefanya mapenzi kabla ya ndoa.


Imeandaliwa na Sute Kamwelwe.