Mchungaji, muumini watupwa jela kwa kughushi cheti cha ndoa

Muktasari:

  • Mchungaji na muumini wake kutoka jijini Nairobi wamefungwa gerezani baada ya kughushi cheti cha ndoa wakiwa na lengo la kulaghai mali za urithi.

Kenya. Wingu jeusi bado linaonekana kutanda kwa wachungaji nchini Kenya hii ni baada ya Mchungaji Christopher Mutira wa kanisa la International Pentecostal Holiness Church Africa, na muumini wake kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani na Mahakama ya Nairobi kwa kosa la kughushi cheti cha ndoa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Taifa leo ya nchini humo imesema Mutira alitenda kosa hilo Julai 2018 kwa kughushi cheti kuwa muumini wake aitwaye Mercy Wanjiru ameolewa na Singh Chadda (76) ambaye kwa sasa ni marehemu.

Hakimu mkazi wa mahakama hiyo ya Milimani Ben Enkubi amesema lengo la Mchungaji huyo na Wanjiru lilikuwa ni kudhurumu mali za Singh Chadda ikishaonekana kwamba yeye ni mkewe.

Naye ndugu wa marehemu Chadda aitwaye Parminder Singh alifichua ukweli mbele ya mahakama kwamba ndugu yao hakuwa ameoa tangu kuzaliwa kwake “Chadda hakuwa na mke mhindi, mzungu wala mwafrika,” alisema Parminder.

Kwa mujibu wa Mahakama imesema Wanjiru alikabiliwa na shtaka la kupeleka cheti feki cha ndoa na kumkabidhi msajili wa ndoa akiandike katika shajala la waliofunga ndoa kwa mujibu wa sheria.

Baada ya hapo alifungua kesi mahakama kuu ili atambuliwe kuwa mrithi wa mali ya Chadda.

Mali alizozodai Wanjiru inadaiwa ni nyumba ambayo Chadda alikuwa anaishi, shamba la ekari saba na hati za dhamana katika benki.