Gachagua aligawa eneo Mlima Kenya

Muktasari:

  • Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua amekiri uteuzi wake kuwa mgombea mwenza wa urais wa Kenya Kwanza umeligawa eneo la Mlima Kenya.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua amekiri uteuzi wake kuwa mgombea mwenza wa urais wa Kenya Kwanza umeligawa eneo la Mlima Kenya.

Mei 24, 2022, Gachagua akizungumza kwenye mahojiano ya moja kwa moja na Redio Inooro FM, alisema kuna watu wamemgeuka kwa sababu yeye ameteuliwa kuwa mgombea mwenza.

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto alimteua Gachagua kuwa mgombea mwenza wake, lakini uamuzi huo ulikwenda tofauti na matakwa ya wabunge wa Mlima Kenya.

Awali, baada ya Mlima Kenya kutajwa kama kigezo kikuu cha kupata mgombea mwenza, wabunge waliopo Kenya Kwanza walipiga kura na Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi, Kithure Kindiki, alishinda kwa asilimia 80.

Hata hivyo, Ruto alipofanya uamuzi wake, hakumpa nafasi Kindiki, badala yake alimchukua Gachagua na hivyo kuibua mgawanyiko Mlima Kenya.

“Nimewaongoza hawa watu kwa miaka minne na tulikuwa sawa. Tumetofautiana baada ya kuja hili suala la mgombea mwenza,” alisema.

Gachagua alisema, yeye na wabunge wa Mlima Kenya pamoja na Seneta Kindiki walikuwa na uhusiano wa kaka na dada, walishirikiana vizuri kwa mambo mengi mpaka lilipoibuka suala la mgombea mwenza.

Hata hivyo, Gachagua alisema tofauti na mgawanyiko uliopo Mlima Kenya hasa kwenye kambi ya Kenya Kwanza ni jambo la kawaida, kwani hata familia hutofautiana kwa sababu ya masilahi fulani.

Gachagua alitaka watu waliokasirishwa na yeye kuteuliwa mgombea mwenza wa Ruto, watambue kwamba mgombea mwenza ni kama kuchagua mke, lazima mtu amwelekee yule anayeendana naye.

“Ni uamuzi binafsi kwa yule anayewania urais. Anayepewa nafasi ya kuwa mgombea mwenza lazima awe mtu ambaye mgombea urais anamjua vizuri, anayeendana naye, wanayefanana mawazo na urafiki wenye misingi inayokubalika. Vigezo hivyo ndivyo vimefanya niwashinde,” alisema Gachagua.

Kingine, Gachagua aliutambua mchakato wa kura Mlima Kenya, ambao katika wabunge 30 wa eneo hilo, waliopo Kenya Kwanza, 24 walimpigia kura Seneta Kindiki kuwa mgombea mwenza. Kura 24 kati ya 30 ni sawa na asilimia 80.

Gachagua anasema kuwa vigezo binafsi vya Ruto ndivyo vilimpa yeye nafasi kuliko Seneta Kindiki na wengine waliokuwa wanatajwa.

Upande mwingine, Kindiki amekuwa akiubeza uteuzi wa Gachagua na kueleza kwamba yeye ndiye alikuwa anakubalika zaidi ndani ya Kenya Kwanza, vilevile kwa wananchi.

Hata hivyo, mwisho alimuunga mkono Gachagua.

“Nataka niwe mkweli kabisa. Mimi ni maudhui yenye matokeo. Tangu lini mawazo ya wengine kuhusu mgombea mwenza yakawekwa mezani na kuchambuliwa na mgombea urais. Niliona mantiki ya Gachagua kuteuliwa kuwa mgombea mwenza,” alisema Seneta Kindiki.

Muhimu zaidi ni kwamba Gachagua alisema hivi sasa mkazo wake ni kuunganisha viongozi wote wa Kenya Kwanza waliopo Mlima Kenya ili washirikiane kutafuta ushindi wa pamoja.

Alisema, kwa sasa yeye ndiye naibu nahodha wa Kenya, lakini kwa kuwa anatokea Mlima Kenya anasimama kuwa nahodha wa viongozi wote wa eneo hilo, kwa hiyo jukumu la kuwaunganisha ni lake.